Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia ya Saa za Mkononi

Historia ya Saa za Mkononi

Historia ya Saa za Mkononi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

JE, UNAJUA ni saa ngapi? Unaweza kujua ukitazama saa uliyo nayo mkononi. Lakini je, saa yako ni sahihi? Tunaweza kupuuza thamani ya saa zetu lakini ni tata kuliko zinavyoonekana.

Licha ya kwamba wakati si kitu halisi nao haudumu, sikuzote mwanadamu amependezwa na kuupima. Mabadiliko ya majira, mzunguko wa mwezi, mfuatano wa usiku na mchana, mambo yote hayo hupima wakati kiasili. Lakini mwanadamu amejitahidi kwa muda mrefu kupima wakati kwa vipimo vidogo zaidi na kwa usahihi zaidi.

Jinsi Ambavyo Saa Hufanya Kazi

Usanifu-saa, yaani, sayansi inayohusisha kutengeneza mashini zinazoonyesha wakati, ni miongoni mwa sanaa za kisayansi za kale zaidi. “Moyo” wa saa ni ile mashini inayoongoza utendaji wote. Hiyo huongoza kiasi cha nguvu inayotendesha mashini hiyo. Nguvu hizo zinaporuhusiwa kutenda kwa kadiri ndogo na kwa mwendo uleule, wakati unaweza kupimwa. Hakuna anayejua ni lini hasa saa ya kwanza ilipobuniwa, lakini hatua kubwa ilipigwa karibu mwaka wa 1500, saa zinazoweza kubebwa zilipotengenezwa mara ya kwanza.

Saa za mkononi zinazotumiwa sana leo, ni za karibuni sana. Zilianza kutumiwa sana mwishoni mwa miaka ya 1800 hasa kati ya wanawake. Wakati wa vita vya kwanza vya ulimwengu, askari wa kikosi cha mizinga waliona kuwa saa inayovaliwa mkononi inafaa zaidi kuliko inayobebwa mfukoni. Baada ya hapo, saa za mkononi zikawa maarufu.

Siku hizi, saa nyingi ni za elektroni nazo hutumia chembechembe za mawe meupe yanayong’aa. Kinapochongwa kwa njia maalum na kuwekwa katika mkondo unaofaa wa umeme, kipande cha jiwe hilo hutikisika kwa mwendo uleule, na kufanya kama penduli.

Ni vigumu sana kurekebisha saa za majira au za betri ili zionyeshe wakati kwa usahihi. Hata uwe na saa ya aina gani, ni wazi kuwa haitapima wakati kwa usahihi kabisa. Hata hivyo, leo kuna saa za betri zinazojirekebisha pindi kwa pindi kwa kutumia ishara kutoka kwa saa za atomi. * Watangazaji wa saa hizo hudai kwamba saa hizo zinazoongozwa na mawimbi ni sahihi sana hivi kwamba hupoteza sekunde moja tu baada ya miaka milioni moja!

Saa za Majira Zingali Zinavutia

Unapofikiria usahihi huo wa hali ya juu na kwamba mashini inayoongoza utendaji wote wa saa ilibuniwa zaidi ya miaka 200 iliyopita, huenda ukahisi saa za majira zimepitwa na wakati. Hata hivyo, bado watu wengi huvutiwa na saa ya majira. Kila mwaka mamilioni hutengenezwa. Katika miaka ya karibuni, faida inayotokana na kuuzwa kwa saa za majira za Uswisi ilizidi ile inayotokana na saa za betri. Mashini mpya zinazofanya kazi vizuri na zisizosuguana sana za kuongoza utendaji wote wa saa zimebuniwa, na watu wanaendelea kutafuta mafundi wa saa wenye ujuzi ili kurekebisha saa zao za majira.

Ni nini hufanya saa za majira zivutie? Michael, fundi wa saa mwenye uzoefu wa miaka 30, anaamini kwamba zinawavutia watu kwa sababu zinatumika kwa muda mrefu. Anasema kwamba ingawa saa za betri zinaweza kufanya kazi vizuri kwa miaka 15 hivi, saa nzuri ya majira inaweza kuonyesha wakati kwa usahihi kwa zaidi ya miaka 100. Saa hiyo ambayo mtoto hurithi kutoka kwa mzazi, inaweza kuwa yenye thamani sana.

Wengine huvutiwa na saa za majira kwa sababu ya miundo yake tata na usahihi unaohusika katika kuonyesha habari kuhusu wakati na astronomia kwa kutumia gia na springi ndogo sana. Pia, kwa kuwa saa hizo zinaweza kutengenezwa kwa mkono, fundi mwenye bidii anaweza kuelewa jinsi zinavyofanya kazi na kuzirekebisha.

Tofauti na mashini nyingine, saa hutarajiwa zifanye kazi kila siku, miaka nenda miaka rudi. Zaidi ya hayo, saa za mkononi hufanya kazi na kuonyesha wakati kwa usahihi katika mazingira mbalimbali na katika mkao wowote ule, hata mtu anapobadili-badili mwelekeo. Saa ambayo huongeza au kupoteza sekunde 20 hivi kwa siku ina kasoro ya asilimia 0.023 tu. Hicho ni kiwango cha usahihi ambacho hutarajiwa kwa kifaa chochote cha kisayansi kilichotengenezwa kwa makini. Basi si ajabu kwamba watu wengi hushangazwa na ustadi, ubunifu, na ufundi unaohusika katika kutengeneza saa ya mkononi ya majira.

Bila shaka, mambo mengine pia yanahusika. Michael, aliyetajwa mapema anasema kwamba watu fulani huchoshwa tu na kubadili betri za saa. Kwa hiyo, ni nini kinachoweza kukusaidia kuamua aina ya saa utakayovaa?

Uchague Saa Gani?

Bila shaka, ungependa kuwa na saa inayovutia. Kwa watu wengi hiyo inamaanisha kuwa na saa nzuri, inayofanya kazi, na yenye sura ya kupendeza. Isitoshe, Michael anapendekeza ufikirie kwa makini mambo yatakayoipata saa yako. Je, utaivaa kila siku au katika pindi za pekee tu? Je, itahimili kugongwa-gongwa au viwango tofauti vya joto? Kwa mfano, kemikali au maji ya chumvi yanaweza kuharibu mikanda na vifuniko fulani vya saa. Kwa hiyo ni jambo la hekima kufikiria mambo hayo.

Kuhusu bei, unapaswa kuwa na bajeti na kuifuata. Kwa kawaida, saa za majira ni ghali kuliko saa za betri. Hata hivyo, kumbuka kwamba utendaji uleule hutumika katika saa nyingi. Kwa kawaida, sehemu ya nje na ile sehemu ambayo huonyesha wakati huwa zimebuniwa na kuundwa vizuri. Mara nyingi, bei hutofautiana tu kwa sababu ya sehemu zisizofanya kazi kama vile kifuniko na mkanda. Kwa hiyo, ikiwa saa ni ya bei ghali haimaanishi kwamba ni sahihi zaidi au ni yenye kutegemeka.—Ona sanduku lililo juu.

Ukiwa na saa ya mkononi ni rahisi kujua ni saa ngapi. Kujua jinsi saa hutengenezwa kunaweza kukusaidia uthamini vifaa hivyo muhimu. Je, wewe huhisi kuwa umetatanika usipokuwa na saa yako?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Saa za atomi huonyesha wakati kwa usahihi kabisa kwa sababu zinatumia mitikisiko ya atomi kuiendesha kwa mwendo uleule.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Ni Saa Gani Inayokufaa Zaidi?

AINA: Kronografu ina vifaa fulani vya kuhesabia vipindi vifupi vya wakati, nacho ni chombo kinachofaa ikiwa unataka kurekodi matukio. Saa isiyopenya maji inafaa katika michezo. Ikiwa wewe husahau kuongeza majira, kumbuka kwamba saa ya betri haihitaji kuongezwa majira. Pia huhitaji kutia majira saa zinazojitia majira, ambazo huongezwa majira mvaaji anapotikisa mkono wake.

USAHIHI: Ikiwa unathamini sana saa sahihi, huenda ukafikiria kununua kronometa, saa inayopima wakati kwa usahihi na kutimiza viwango rasmi vinavyokubalika kimataifa. Jinsi saa za betri zilivyoundwa huzifanya ziwe sahihi zaidi. Saa ya kisasa ya majira inayopiga mara 28,800 kwa saa hutikisika mara nne kwa sekunde. Linganisha saa hiyo na saa ya betri ambayo hutikisika kati ya mara 10,000 na 100,000 kwa sekunde!

KUONYESHA WAKATI: Kuna saa ambayo huonyesha wakati kwa kutumia tarakimu. Nyingine hutumia mishale inayozunguka uso wa saa. Saa za tarakimu zinaweza kupiga kengele, kuonyesha tarehe, kanda fulani ya wakati, na vipindi vya muda vinavyopita. Saa zenye mishale huonyesha wakati katika njia rahisi na yenye kueleweka, kwa kutupia tu jicho mishale yake.

UTUNZAJI: Tofauti na saa ya betri, kwa kuwa saa ya majira huendeshwa kwa springi yenye nguvu, inaweza kuacha kufanya kazi kwa urahisi kwa sababu ya uchafu au vumbi. Hata hivyo, saa yako ya majira inahitaji utunzaji zaidi kuliko saa ya betri, ili iendelee kufanya kazi bila matatizo. Kwa kuwa saa za betri hazina sehemu zozote zinazosonga, hazihitaji utunzaji wowote isipokuwa tu kubadili betri.

[Chati/Picha katika ukurasa wa 23]

SAA MAARUFU ZA MKONONI

▪ 1810-1812

Saa ya kwanza ya mkononi, Abraham-Louis Breguet

▪ 1945

Tarehe yaonyeshwa kwenye uso wa saa, Rolex

▪ 1957

Saa ya mkononi yenye mota inayotumia umeme, Kampuni ya Saa ya Hamilton, Marekani

▪ 1960

Wakati unahesabiwa kwa kutumia elektroni, Bulova

▪ 1972

Saa ya mkononi ya tarakimu, Kampuni ya Saa ya Hamilton

[Hisani]

Second and fourth photos: Courtesy of Hamilton Watches

[Picha katika ukurasa wa 23 zimeandaliwa na]

OMEGA