Je, Kweli Unahitaji Kufanya Mazoezi?
Je, Kweli Unahitaji Kufanya Mazoezi?
“Fanya mazoezi mara mbili kwa juma ili uwe na afya nzuri. Fanya mazoezi dakika 30 kwa siku. Epuka kileo ili kuzuia kansa. Tumia kileo ili kupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo. Je, unahisi kwamba kuna mashauri mengi sana mazuri? Siku moja magazeti yanasema jambo moja, na juma linalofuata yanasema jambo tofauti kabisa. . . . Kwa nini wanasayansi hawakubaliani? Kwa nini juma moja inasemekana kwamba kahawa inadhuru na juma lingine inasemekana kuwa haina madhara?”—Barbara A. Brehm, profesa wa mafunzo ya mazoezi na michezo, mwenye Shahada ya juu ya Ualimu.
MARA nyingi, wataalamu wa afya huwa na maoni tofauti kuhusu ulaji na kufanya mazoezi. Watu wengi hutatanishwa na habari nyingi kuhusu yale wanayopaswa kufanya na wasiyopaswa kufanya ili kuwa na afya nzuri. Hata hivyo, kuhusiana na uhitaji wa kufanya mazoezi kwa kiasi, wanasayansi wanakubaliana kwamba ukitaka kuwa na afya nzuri lazima ufanye mazoezi kwa ukawaida!
Kutofanya mazoezi ya mwili ya kutosha kumekuwa tatizo kubwa leo, hasa katika nchi zilizoendelea kiviwanda. Kwa miaka mingi, watu wengi katika nchi hizo walifanya kazi ngumu kama vile kulima, kuwinda, au kujenga. Ni kweli kwamba kazi ngumu walizofanya ili tu kujiruzuku ziliwaletea mababu zetu mkazo, na hata kufupisha maisha yao. Kulingana na kichapo Encyclopædia Britannica, “katika Ugiriki na Roma za kale, watu waliishi kwa wastani wa miaka 28 hivi.” Tofauti na hilo, kufikia mwisho wa karne ya 20, katika nchi zilizoendelea, watu waliishi kwa miaka 74 hivi. Kwa nini kukawa na badiliko hilo?
Je, Teknolojia Ni Baraka au Laana?
Leo watu wana afya bora na wanaishi muda mrefu zaidi kuliko wale walioishi karne nyingi zilizopita. Mabadiliko ya kiteknolojia yamechangia jambo hilo. Vifaa vya kisasa vimebadili njia za kufanya mambo, na vimerahisisha kazi nyingi ngumu. Taaluma ya kitiba imepiga hatua kubwa katika kupigana na magonjwa, na hivyo kuboresha afya ya wengi. Hata hivyo, hilo limetokeza madhara fulani.
Ingawa teknolojia ya kisasa imeboresha afya, kadiri muda unavyopita, imefanya pia watu wengi waishi maisha ya kukaa tu bila kufanya mazoezi ya kutosha. Katika ripoti yao iliyochapishwa hivi karibuni yenye kichwa International Cardiovascular Disease Statistics, Shirika la Moyo la Marekani lilieleza kwamba “mabadiliko ya kiuchumi, watu kuhamia mijini, usitawi wa viwanda, na kuenea kwa biashara za kimataifa, huleta mabadiliko katika mitindo ya maisha ambayo huchangia ugonjwa wa moyo.” Ripoti hiyo inataja “kutofanya mazoezi na kula vyakula visivyofaa” kuwa mambo yanayochangia sana ugonjwa huo.
Miaka 50 tu iliyopita, katika nchi nyingi mwanamume alifanya kazi ngumu ya kulima kwa farasi na plau, kuendesha baiskeli hadi
kwenye benki, na kurekebisha vifaa vilivyoharibika nyumbani wakati wa jioni. Hata hivyo, mtindo wa maisha wa wajukuu wake ni tofauti sana. Leo, mfanyakazi anaweza kuketi mbele ya kompyuta karibu siku nzima, aende mahali popote atakapo kwa gari lake, na atazame televisheni jioni yote.Kulingana na uchunguzi mmoja, zamani wakataji miti wa Sweden walitumia kalori 7,000 hivi kwa siku wakikata miti na kubeba magogo, lakini leo wao hutumia mashini za hali ya juu kufanya baadhi ya kazi hizo ngumu. Zamani, barabara nyingi ulimwenguni pote zilijengwa na kudumishwa na watu waliotumia sururu na sepetu. Lakini sasa, hata katika nchi zinazoendelea, mashini kubwa hutumiwa badala ya sururu na sepetu.
Katika sehemu fulani za China, watu wengi zaidi wanapendelea kutumia skuta badala ya baiskeli. Nchini Marekani, ambako asilimia 25 ya safari zote hazizidi kilometa moja hivi, asilimia 75 ya safari hizo fupi hufanywa kwa gari.
Teknolojia ya kisasa pia imefanya watoto wakae tu bila kufanya mazoezi ya kutosha. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kadiri michezo ya video “inavyozidi kuwa yenye kufurahisha na halisi, ndivyo watoto . . . wanavyotumia wakati mwingi zaidi kuicheza.” Mikataa kama hiyo imefikiwa kuhusu kutazama televisheni na vitumbuizo vingine ambavyo huwafanya watoto wakae tu bila kufanya mazoezi ya kutosha.
Hatari za Kukaa Tu Bila Kufanya Mazoezi ya Kutosha
Kwa sababu ya kupunguza mazoezi wanayofanya, watu wengi wanapatwa na matatizo ya kimwili, kiakili, na kihisia. Kwa mfano, hivi karibuni shirika moja la afya nchini Uingereza liliripoti hivi: “Watoto wasiofanya mazoezi wanaweza kukabili hatari ya kutojiheshimu, kuwa na wasiwasi mwingi na mifadhaiko mingi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto hao watavuta sigara na kutumia dawa za kulevya kuliko watoto wanaofanya mazoezi. Wafanyakazi wasiofanya mazoezi hukosa kwenda kazini mara nyingi kuliko wale wanaofanya mazoezi. Wanapozeeka, watu wasiofanya mazoezi hupoteza nguvu na uwezo wa kunyumbulika katika shughuli za kila siku. Matokeo ni kwamba wengi hushindwa kujitegemea na afya yao ya akili huzorota.”
Cora Craig, rais wa Taasisi ya Utafiti wa Mazoezi na Mtindo wa Maisha ya Kanada, anaeleza kwamba “Wakanada wengi hawafanyi kazi ngumu kama hapo awali . . . Kwa ujumla, ni wachache wanaofanya kazi hizo.” Gazeti la Kanada
Globe and Mail linaripoti hivi: “Karibu asilimia 48 ya Wakanada ni wazito kupita kiasi, kutia ndani asilimia 15 ambao ni wanene kupita kiasi.” Gazeti hilo linaongezea kwamba huko Kanada, asilimia 59 ya watu wazima hawafanyi mazoezi. Dakt. Matti Uusitupa, wa Chuo Kikuu cha Kuopio, Finland, anaonya kwamba “ugonjwa wa kisukari ambao kwa kawaida huwapata watu wazima unaongezeka kwa haraka ulimwenguni pote kwa sababu watu wengi wamekuwa wanene kupita kiasi na hawafanyi mazoezi.”Nchini Hong Kong, uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba huenda asilimia 20 hivi ya vifo vyote vilivyotokea miongoni mwa watu walio na umri wa miaka 35 au zaidi, vilisababishwa na kukosa kufanya mazoezi. Uchunguzi huo ulioongozwa na Profesa Tai-Hing Lam wa Chuo Kikuu cha Hong Kong na kuchapishwa na jarida Annals of Epidemiology katika mwaka wa 2004, ulimalizia kwa kusema kwamba kwa Wachina wanaoishi Hong Kong, “hatari za kutofanya mazoezi zinapita zile za kutumia tumbaku.” Watafiti wanatabiri kwamba raia wengine wa China “watapatwa na madhara hayohayo.”
Je, inafaa kuwa na wasiwasi kuhusu hali hiyo? Je, kweli kutofanya mazoezi kunaweza kudhuru afya yetu kuliko kuvuta tumbaku? Watu wengi hukubali kwamba watu wasiofanya mazoezi huelekea kupatwa na shinikizo kubwa la damu, hukabili hatari kubwa ya kupatwa na kiharusi na ugonjwa wa moyo, aina fulani za kansa, ugonjwa wa mifupa, na uwezekano mkubwa wa kuwa wanene kupita kiasi wanapolinganishwa na watu wanaofanya mazoezi. *
Gazeti The Wall Street Journal linaripoti hivi: “Katika kila bara ulimwenguni, kutia ndani
maeneo yaliyo na utapia-mlo mwingi, idadi ya watu wazito au wanene kupita kiasi inaongezeka kwa kasi sana. Tatizo hilo linasababishwa hasa na kula vyakula vyenye kalori nyingi na kutofanya mazoezi, jambo ambalo limefanya watu wengi nchini Marekani wawe wanene kupita kiasi.” Dakt. Stephan Rössner, ambaye ni profesa wa masuala ya afya katika Taasisi ya Karolinska huko Stockholm, Sweden, anakubaliana na jambo hilo naye alisema: “Hakuna nchi ulimwenguni ambako tatizo la kunenepa kupita kiasi haliongezeki.”Tatizo la Ulimwenguni Pote
Ni wazi kwamba ili tuwe na afya nzuri tunahitaji kuwa na ratiba nzuri ya kufanya mazoezi. Hata hivyo, ingawa hatari za kutofanya mazoezi zimezungumziwa sana, watu wengi ulimwenguni hawafanyi mazoezi yoyote. Shirikisho la Moyo Ulimwenguni linaamini kwamba kati ya asilimia 60 hadi 85 ya watu ulimwenguni “hasa wasichana na wanawake, hawafanyi mazoezi ya kutosha ili kupata manufaa ya afya.” Shirikisho hilo linadai kwamba “karibu thuluthi mbili ya watoto pia hawafanyi mazoezi ya kutosha ili kupata manufaa ya afya.” Huko Marekani, karibu asilimia 40 ya watu wazima hawafanyi mazoezi na karibu nusu ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 21 hawafanyi mazoezi magumu kwa ukawaida.
Utafiti uliochunguza kuenea kwa tabia ya watu ya kukosa kufanya mazoezi katika nchi 15 za Ulaya uligundua kwamba asilimia 43 ya watu nchini Sweden hawafanyi mazoezi, nayo Ureno ilikuwa na asilimia 87. Huko São Paulo, Brazili, karibu asilimia 70 ya watu hawafanyi mazoezi. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linaripoti kwamba “habari zilizokusanywa kuhusu uchunguzi wa afya ulimwenguni pote zinapatana.” Basi hatupaswi kushangaa kwamba watu milioni mbili hivi hufa kila mwaka kutokana na sababu zinazohusiana na kukosa kufanya mazoezi.
Wataalamu wa afya ulimwenguni wanaona mwelekeo huo kuwa hatari. Ili kukabiliana na tatizo hilo, mashirika ya kiserikali ulimwenguni yameanzisha kampeni za kuelimisha umma kuhusu manufaa ya kufanya mazoezi kwa kiasi. Kufikia mwaka wa 2010, Australia, Japani, na Marekani zinatumaini kwamba idadi ya raia wanaofanya mazoezi itaongezeka kwa asilimia 10. Scotland inatumaini kwamba kufikia mwaka wa 2020, asilimia 50 ya watu wazima nchini humo watakuwa wakifanya mazoezi kwa ukawaida. Ripoti moja ya WHO inaeleza kwamba “nchi nyingine zilizozungumzia kampeni zao za kitaifa za kufanya mazoezi zilikuwa Mexico, Brazili, Jamaika, New Zealand, Finland, Shirikisho la Urusi, Morocco, Vietnam, Afrika Kusini, na Slovenia.”
Licha ya jitihada za serikali na mashirika ya afya, kila mmoja wetu ana daraka la kutunza afya yake mwenyewe. Jiulize, ‘Je, mimi hufanya mazoezi ya kutosha? Ikiwa sivyo, ninaweza kufanya nini ili niongeze mazoezi yangu?’ Makala inayofuata itakuonyesha jinsi unavyoweza kufanya mazoezi zaidi.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 16 Kutofanya mazoezi kunaweza kuongeza sana hatari ya kupatwa na magonjwa fulani yanayotishia uhai. Kwa mfano, kulingana na Shirika la Moyo la Marekani, kutofanya mazoezi “huongeza maradufu hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo na huzidisha kwa asilimia 30 hatari ya kupatwa na shinikizo kubwa la damu. Pia huongeza maradufu uwezekano wa kufa kutokana na ugonjwa wa moyo na kiharusi.”
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Hasara za Kutofanya Mazoezi
Serikali na mashirika mengi ya afya yanafikiria kwa uzito hasara zinazoipata jamii kwa sababu ya watu kutofanya mazoezi.
● Australia - Nchi hiyo hutumia dola milioni 377 hivi kila mwaka kutibu matatizo ya afya yanayosababishwa na kutofanya mazoezi.
● Kanada - Kulingana na Shirikisho la Moyo Ulimwenguni, katika mwaka mmoja tu Kanada ilitumia dola zaidi ya bilioni mbili kutibu matatizo ya afya “yaliyosababishwa na kutofanya mazoezi.”
● Marekani - Katika mwaka wa 2000, Marekani ilitumia pesa nyingi sana, dola bilioni 76, kwa ajili ya gharama za matibabu yaliyosababishwa moja kwa moja na kutofanya mazoezi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
Watoto Wanahitaji Kufanya Mazoezi
Uchunguzi wa hivi karibuni umegundua kwamba idadi inayoongezeka ya watoto hawafanyi mazoezi kwa ukawaida. Tatizo hilo limeenea zaidi miongoni mwa wasichana kuliko wavulana. Inaonekana kwamba kadiri watoto wanavyokua, ndivyo wanavyofanya mazoezi kwa kiasi kidogo zaidi. Zifuatazo ni baadhi ya faida ambazo watoto wanaweza kupata kwa kufanya mazoezi kwa ukawaida:
● Kuwa na mifupa na misuli yenye nguvu na viungo vyenye afya
● Kuzuia kuwa mzito na mnene kupita kiasi
● Kuzuia au kuahirisha kupatwa na shinikizo kubwa la damu
● Kuzuia ugonjwa wa kisukari unaowapata watu wazima
● Kujiheshimu zaidi, kuzuia wasiwasi na kupatwa na mfadhaiko
● Kuwa na mtindo wa maisha wenye utendaji mwingi ambao unaweza kuwazuia wasifanye mazoezi wanapokuwa watu wazima
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Afya Bora kwa Wazee
Inasemekana kwamba kadiri unavyozeeka ndivyo unavyoweza kunufaika kwa kufanya mazoezi kwa kiasi. Hata hivyo, wazee wengi husita kufanya mazoezi kwa ukawaida kwa kuogopa kwamba wataumia au watakuwa wagonjwa. Ni kweli kwamba wazee wanapaswa kutafuta ushauri wa daktari kabla ya kuanza kufanya mazoezi magumu. Hata hivyo, wataalamu wanaamini kwamba kufanya mazoezi kunaweza kuboresha sana maisha ya wazee. Zifuatazo ni baadhi ya faida ambazo wazee wanaweza kupata kwa kufanya mazoezi:
● Kuwa chonjo kiakili
● Usawaziko na kunyumbulika
● Afya ya kihisia
● Kupona haraka ugonjwa au jeraha
● Kuboresha utendaji wa tumbo na ini
● Uyeyushaji wa chakula
● Mfumo wa kinga
● Mifupa yenye nguvu
● Kuwa na nguvu nyingi