Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jua Linawezaje Kuangaza Katikati ya Usiku?

Jua Linawezaje Kuangaza Katikati ya Usiku?

Jua Linawezaje Kuangaza Katikati ya Usiku?

“JUA linawezaje kukosa kutua?” Nikiwa mmishonari kutoka Finland ambaye anatumika katika nchi ya Papua New Guinea, mara nyingi nilisikia swali hilo. Katika nchi za Kitropiki saa za mchana hubaki zilezile kila mwezi. Kwa hiyo, wakazi wa nchi za Kitropiki hushangaa sana kusikia kwamba katika sehemu ya Aktiki, jua halitui kwa miezi kadhaa. Na nilipojaribu kueleza kwamba wakati wa majira ya baridi kali jua halichomozi kamwe, wengi walishangaa hata zaidi.

Basi, jua huangazaje katikati ya usiku? Jambo hilo lenye kushangaza hutukia kwa sababu dunia inapozunguka jua kila mwaka, mhimili wa dunia huwa umeinama kwa digrii 23.5 kutoka kwa jua. Hivyo, wakati wa kiangazi katika Kizio cha Kaskazini, Ncha ya Kaskazini huinama kuelekea jua na wakati wa majira ya baridi kali ncha hiyo huinama mbali na jua. Kwa kuwa dunia huzunguka juu ya mhimili wake mara moja kwa siku, kwenye Mzingo wa Aktiki usiku mmoja kwa mwaka, yaani, karibu Juni 21, jua halitui. Vivyo hivyo, siku moja kwa mwaka, yaani, karibu Desemba 21, jua halichomozi, ingawa mchana huenda kukawa na nuru hafifu kama wakati wa mapambazuko.

Kwa kweli, kadiri unavyoelekea upande wa kaskazini juu ya Mzingo wa Aktiki, ndivyo jua linavyokosa kutua usiku wakati wa kiangazi na ndivyo jua hukosa kuchomoza siku nyingi wakati wa majira ya baridi kali. Kwenye ncha za Kaskazini na Kusini za dunia, kuna miezi sita ya mchana na miezi sita ya usiku. *

Watu wanaoishi kwenye ncha hizo za dunia hulalaje wakati wa kiangazi, nao hukabilianaje na siku nyingi ambazo jua halichomozi wakati wa majira ya baridi kali? Zamani, katika jamii fulani, watu walilala saa maradufu katika miezi ambayo jua halikuchomoza kuliko walivyolala katika miezi ambayo jua halikutua. Kuishi maisha ya kisasa kumewawezesha wengi kulala kwa muda uleule kila usiku. Lakini wakati wa kiangazi ambapo jua halitui, bado wakazi wa Kaskazini huwa na nguvu za ziada za kufanya kazi. “Inapokuwa mchana kabisa saa 5:00 usiku, sijisikii kwenda kulala,” asema Patrick, anayeishi Alaska. “Nyakati nyingine mimi hutoka na kwenda kukata nyasi au kufanya kazi nyingine.”

Kwa upande mwingine, miezi ambayo jua halitui au kuchomoza inaweza kuchosha kimwili na kisaikolojia. Hivyo, watu fulani hujaribu kuzuia nuru isipenye kwenye chumba chao cha kulala katika miezi ambayo jua halitui na kutumia taa wakati jua halichomozi, ili kusawazisha wakati wao wa kulala na kuzuia uchovu na kushuka moyo. Hata hivyo, licha ya magumu hayo, wakazi na wageni wanakubali kwamba kushuhudia jua likiangaza katikati ya usiku ni jambo lisiloweza kusahaulika.—Tumetumiwa makala hii.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Huko Antaktiki, hali huwa sawa na hiyo, lakini majira huenda kinyume cha yale ya Aktiki.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 31]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mhimili wa dunia ulioinama hufanya maeneo yaliyo kwenye ncha za Kaskazini na za Kusini yapate nuru ya jua daima wakati wa kiangazi na kuwa na giza daima wakati wa majira ya baridi kali (Huu ni mfano wa kizio cha Kaskazini)

Vuli ←

● ● ● ● ●

Majira ya ● ◯ ● Kiangazi

baridi kali ● ● ● ● ● Dunia huzunguka

kwenye mhimili wake

→ Masika mara moja kwa siku

[Picha katika ukurasa wa 31]

Upigaji picha wa hatua za tukio ukionyesha jua katikati ya usiku

[Hisani]

© Paul Souders/WorldFoto