Recife—Jiji Lililositawi kwa Sababu ya Sukari
Recife—Jiji Lililositawi kwa Sababu ya Sukari
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI
MABARA ya Amerika hayakufanywa kuwa koloni ili kutafuta “dhahabu, utukufu, au kuhubiri injili.” Watawala wa Ulaya walitamani sana sukari. Kuanzia miaka ya katikati ya karne ya 15, mapato yaliyotokana na miwa iliyokuzwa katika visiwa vya Atlantiki iliyokuwa ya bei ghali ilitajirisha sana serikali ya Ureno. Kwa hiyo, mnamo 1516, Mfalme Manuel wa Kwanza wa Ureno alianza kutokeza sukari katika maeneo ya mabara ya Amerika yaliyokuwa chini ya utawala wake.
Ingawa viwanda vya kwanza vya sukari vilijengwa kusini mwa Brazili, jimbo la Pernambuco, * lililokuwa kaskazini-mashariki mwa Brazili, lilikuja kuwa kituo kipya cha kutokeza sukari. Eneo hilo lilifaa kwa ukuzaji miwa kwa sababu ya hali ya hewa yenye joto, mvua nyingi, milima isiyo na miteremko mikali, na udongo wenye rutuba. Misitu ya pwani ilitoweka miwa ilipopandwa sana kwenye milima na nyanda zinazozunguka delta ya Mto Capibaribe.
Kufikia mwaka wa 1537, koloni ndogo ya mabaharia na wavuvi ilianzishwa. Ilikuwa kwenye ncha ya rasi nyembamba iliyoanzia kusini huko Olinda, lililokuwa jiji kuu la Pernambuco. Bandari hiyo ya asili, ambayo iliitwa Povo dos Arrecifes (Kijiji cha Matumbawe) na baadaye ikaitwa Recife, ilipakana na Mto Capibaribe upande wa magharibi, na upande wa mashariki kulikuwa na ukuta wa matumbawe ambayo yaliitenga na Bahari ya Atlantiki. Miwa iliyovunwa ilisafirishwa kupitia Mto Capibaribe na kuhifadhiwa hapo ikingojea kusafirishwa hadi Ulaya.
Habari za kusitawi kwa Pernambuco zilivutia wageni wasiotakikana. Kwanza, maharamia Wafaransa walitwaa na kupora jiji la Recife mnamo 1561, kisha mfanyabiashara Mwingereza Sir James Lancaster ambaye nyakati nyingine huonwa kuwa haramia, akafanya hivyohivyo katika mwaka wa 1595. Inasemekana kwamba Lancaster aliondoka baada ya kujaza nyara katika mashua zake na meli nyingine 12 alizotwaa kwa nguvu kutoka kwa wafanyabiashara Wafaransa na Wareno. Ngome zilijengwa kwenye rasi kati ya Recife na Olinda ili kuzuia uvamizi kama huo, lakini hazikufua dafu.
Vita vya Sukari
Mwanzoni mwa karne ya 17, Pernambuco, wakati huo likiwa chini ya Hispania, lilikuwa eneo kubwa zaidi na lililotokeza sukari kwa wingi zaidi ulimwenguni. Kwa kuwa lilikuwa na viwanda 121 vya sukari, Recife likawa bandari yenye shughuli nyingi zaidi katika maeneo ya Amerika yaliyomilikiwa na Ureno.
Watu barani Ulaya walifurahia kula vyakula vyenye sukari ya Brazili ambayo ilisafishwa Uholanzi. Mnamo 1621, makubaliano ya amani kati ya Uholanzi na Hispania yalipokwisha, biashara hiyo yenye kuleta faida kubwa ilihatarishwa. Mwaka huohuo, Kampuni ya Dutch West India ilipewa haki ya pekee ya kufanya biashara ya sukari na nchi za Afrika na Amerika. Kampuni hiyo ilitoa suluhisho katika hati iliyokuwa na kichwa kilichosema waziwazi, “Sababu Zinazofanya Kampuni ya West Indies Itwae Brazili Kutoka kwa Mfalme wa Hispania Haraka Iwezekanavyo,” ambayo iliambatana na “Orodha ya Vitu Ambavyo Brazili Inaweza Kutokeza.” Vita vya Sukari vilikuwa karibu kuanza!
Februari 14, 1630, meli 65 zilizokuwa na bendera ya Kampuni ya West Indies zilionekana karibu na pwani ya Pernambuco na baada ya makabiliano mafupi, kampuni hiyo ikasimamisha bendera yake kwenye ardhi ya Brazili. Wavamizi hao waliona Recife iliyokuwa na ngome, visiwa vilivyoizunguka, na mito kuwa salama zaidi kuliko milima na nyanda za Olinda. Kwa hiyo, Novemba 25, 1631, Waholanzi waliteketeza kabisa Olinda na kuhamisha makao yao makuu hadi Recife. Huo ulikuwa wakati wa mabadiliko makubwa katika maendeleo ya Recife.
Kwa kuwa hakukuwa na ardhi ya kutosha, majengo ya orofa yalijengwa ili kukabiliana na ongezeko la watu. Majengo membamba ya orofa mbili au tatu yaliyoitwa sobrados, ambayo kwa kawaida yalijengwa katika majiji ya Ulaya, yalijengwa kwa vifaa vilivyotolewa kwenye magofu ya Olinda. Hata hivyo, kufikia mwaka wa 1637, hakukuwa na nafasi ya kujenga huko Recife. Wakati huo, gavana mkuu mpya, Mjerumani John Maurice wa Nassau, akaja na ramani za kujenga jiji ambalo lingekuwa la kisasa zaidi kotekote Amerika Kusini.
Mji Uliojengwa na Maurice
Mji huo ulioitwa Mauricia, ulijengwa kwa miaka saba tu, nao ulijengwa kama majiji ya Ulaya kwani ulikuwa na barabara za lami, soko, majumba ya kifalme, hifadhi ndogo za wanyama waliotolewa Afrika na sehemu za Brazili, bustani za maua, kituo cha kwanza katika mabara ya Amerika cha kuangalia mambo ya angani, jumba la makumbusho, hospitali, na maktaba. Nassau alijenga jiji lake kwenye Kisiwa cha Antônio Vaz
kilichokuwa zaidi ya meta 100 kutoka Recife na kuagiza madaraja mawili yajengwe—ujenzi uliokuwa wa ajabu wakati huo—ili kuunganisha Recife, Mauricia, na bara.—Ona sanduku, “Maurice wa Nassau na Ng’ombe Anayeruka.”Kwa kuwa Nassau hakuwa mfanyakazi wa kulipwa wa kikoloni, alisema hivi kuhusu makao yake mapya: “Brazili ni maridadi na haiwezi kulinganishwa na nchi nyingine chini ya mbingu.” Upendo wake kwa nchi hiyo, ambayo aliagizwa apore na Kampuni ya West Indies, unaonekana katika michoro ya Frans Post na Albert Eckhout, waliokuwa washiriki wa kikundi cha mambo ya kitamaduni ambao Nassau alileta kutoka Ulaya. Chini ya ufadhili wake, kikundi cha wasanii, wanasayansi, na wachongaji vinyago 46 walitokeza vitabu, michoro, na ramani nyingi sana za mandhari yenye kupendeza ya Pernambuco iliyowavutia watu wa Ulaya.
Serikali ya Nassau ilileta ukuzi wa kiuchumi huko Mauricia na Recife. Mikopo iliyotolewa na Kampuni hiyo iligharimia kujengwa upya kwa viwanda vya sukari vilivyoharibiwa wakati wa uvamizi. Baada ya muda, Recife ikajawa na maofisa Waingereza, watalii Wasweden, wauzaji kutoka Scotland, wafanyabiashara Wajerumani na Wafaransa—wote walivutiwa na biashara ya watumwa, sukari, na mbao za Brazili.
Uhuru wa ibada chini ya utawala wa Nassau uliwavutia pia wawekezaji Wayahudi na wakimbizi kutoka Ulaya na Afrika Kaskazini. Kwa muda mfupi Wayahudi wa asili ya Ureno na Hispania walikuwa wakikutanika kwa uhuru katika masinagogi mawili yaliyojengwa huko Amerika. Recife ilikuwa na Wayahudi wengi sana hivi kwamba kituo chake cha kibiashara kiliitwa Rua dos Judeus (Barabara ya Wayahudi).
Uhasama Wazuka Kati ya Brazili na Uholanzi
Licha ya sifa nzuri ya utawala wa Nassau, wakurugenzi wa Kampuni ya West Indies walilalamika kwamba upendezi wake kwa Brazili ulimwongoza kufanya maamuzi ya kifedha yasiyo ya hekima. Wawekezaji wa Kampuni hiyo hawakufaidika sana. Mnamo Mei 1644, Nassau alijiuzulu na kurudi Uholanzi. Kuondoka kwake kulihuzunisha wengi kutia ndani Wareno na kuashiria kuanguka kwa mamlaka ya Uholanzi huko Brazili. Kupungua kwa mazao ya miwa, kushuka kwa bei ya sukari katika soko la kimataifa, na Kampuni kudaiwa pesa nyingi kulifanya wamiliki wa mashamba wazushe ghasia zilizowatimua Waholanzi katika mwaka wa 1654. *
Bustani za Nassau na sehemu kubwa ya jiji alilojenga ziliharibiwa katika ghasia hizo, lakini kulikuwa na mabadiliko fulani. Tamaa ya sukari ya Waholanzi ilihamisha utendaji wa kibiashara wa Pernambuco kutoka Olinda hadi visiwa vilivyokuwa kando ya Mto Capibaribe na kuweka msingi wa jiji kuu jipya. Recife lilikuwa limesitawi na kuwa mji na kituo muhimu cha kibiashara.
Kumbukumbu za Wakati Uliopita
Jiji la kisasa la Recife, ambalo ni mojawapo ya majiji makubwa yaliyositawi kiviwanda, kifedha, na kiutalii nchini Brazili, lenye wakazi zaidi ya 1,300,000, halionekani hata kidogo kama ile koloni ndogo ya wavuvi iliyokuwapo huko Olinda katika karne ya 16. Mashamba ya miwa yaliyokuwa kwenye kingo za Mto Capibaribe yamejengwa makazi ya watu. Kwa sasa, majina ya mashamba hayo na nyumba chache za wamiliki wake ndizo zimebaki. Kituo cha kibiashara cha Recife kilichoko kwenye visiwa vya Recife na Santo Antônio na kwenye wilaya ya bara ya Boa Vista, kimepoteza majengo mengi ya kale ya kikoloni kwa sababu ya kutoyatunza na mabadiliko mengi ya kisasa.
Hata hivyo, mito, visiwa, na matumbawe yaliyowavutia Waholanzi bado ni sehemu muhimu ya Recife, na mabaki ya viwanda vya sukari vya kale huonekana katikati ya majengo ya kisasa. Forte do Brum, ngome yenye pembe nne iliyojengwa hapo awali na Waholanzi ili kulinda bandari, sasa iko kwenye nchi kavu kwa sababu ya sehemu fulani ya bahari kujazwa mchanga, nalo jengo hilo la kihistoria limezungukwa na majengo ya kisasa. Rua dos Judeus, ambayo sasa ni Rua do Bom Jesus (Barabara ya Yesu Mwema), bado ina majengo ya kikoloni yenye rangi nyingi ya karne ya 16, yaliyoitwa sobrados ambayo hayajafanywa kuwa ya kisasa.
Wale ambao wangependa kupata habari zaidi kuhusu historia ya Recife, kuna majumba ya maonyesho yenye ramani za Waholanzi na vitu vya ukumbusho kama vile vilivyo katika jengo la Forte das Cinco Pontas, lililojengwa na watu waliokodiwa na Kampuni ya West Indies mnamo 1630, na jengo la Taasisi ya Akiolojia, Historia, na Jiografia. Jumba la Makumbusho la Northeastern Man lina historia ya maendeleo ya viwanda vya sukari kuanzia mianzo yake midogo hadi viwanda vikubwa vya kisasa, na huonyesha maisha yenye kusikitisha ya watumwa, ‘waliowafanyia kazi matajiri wa sukari.’
Watu hawasisimuliwi sana na sukari kama katika karne zilizopita. Faida kubwa zilizowavutia maharamia wa sukari na Kampuni ya West Indies zimepungua. Wengi hawatamani matatizo yaliyopo ya kifedha, kijamii na ya mazingira yaliyosababishwa na mfumo wa zamani wa kutokeza sukari. Hata hivyo, bado sukari inakuzwa kwa wingi katika maeneo ya pwani ya Pernambuco. Nje tu ya Recife, wafanyakazi huvuna kiasi kikubwa cha miwa kama tu ambavyo wamefanya kwa karne tano zilizopita, kikumbusha kwamba jiji la Recife lilisitawi kwa sababu ya sukari.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Mfalme John wa Tatu wa Ureno aligawanya Brazili katika majimbo 15, na kuweka watawala wa kurithishwa walioitwa donatários.
^ fu. 18 Waholanzi walishindwa vita vya kuidhibiti Brazili lakini Vita vya Sukari viliendelea. Kwa kutumia ujuzi waliopata kutoka kaskazini-mashariki ya Brazili, Waholanzi walianza kulima huko Antilles. Kabla ya mwisho wa karne ya 17, sukari ya bei rahisi kutoka West Indies ilijaa katika soko la Ulaya na hivyo kukomesha haki ya kuuza sukari ambayo ilipewa tu Wareno.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
Maurice wa Nassau na Ng’ombe Anayeruka
“Hapo mwanzoni, mashua ndogo zilitumiwa kusafirisha watu kati ya Mauricia na Recife, lakini hilo lilizuia sana kusitawi kwa biashara. Wazo la kujenga daraja liliungwa mkono na wote, na kazi hiyo ilimalizwa haraka. Sherehe ya kulizindua ingefanywa Jumapili, na programu ilikuwa na tamasha ya ng’ombe anayeruka iliyokusudiwa kuamsha udadisi wa umma!
“Alasiri ya karamu hiyo, wanamuziki walicheza na barabara zilipambwa kwa karatasi ndefu za mapambo. Umati ulikusanyika darajani. Ingawa daraja jipya liliwavutia, wote walitaka sana kuona ng’ombe anayeruka. Wengine waliuliza, ‘Atakuwaje?’ Mwanamke mmoja mzee alisema, ‘Ni dhambi kusema ng’ombe anaweza kuruka kama malaika.’
“Wakati ulipofika, umbo la ng’ombe wa manjano mwenye pembe na mkia mrefu lilitokea katika dirisha la juu la nyumba iliyokuwa kwenye daraja hilo. ‘Ndiye yule!’ wote wakapaaza sauti. Watu mashuhuri, watu wa kawaida, na vilevile watumwa walitazama juu. Kwa ghafula, wakaangua kicheko. Ng’ombe huyo alikuwa tu puto la karatasi lililojazwa hewa moto!
“Kichekesho cha Mwana-Mfalme Maurice wa Nassau kiliwafurahisha watu na kutimiza kusudi jingine muhimu. Kila mtu aliyevuka daraja kumwona ng’ombe huyo akiruka alilipa ada ndogo, na pesa zilizokusanywa zilisaidia sana kugharimia mradi wake muhimu.”
[Hisani]
Terra Pernambucana (Nchi ya Pernambuco), na Mário Sette.
Maurice of Nassau: ACERVO FUNDAÇÃO JOAQUIM NABUCO--RECIFE
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
Venice ya Amerika
“Kama tu Venice, Recife ni jiji linaloibuka kutoka majini nalo huakisiwa majini; jiji ambalo katika sehemu zake za ndani huhisi nguvu za bahari.”—Joaquim Nabuco, mwanasiasa Mbrazili.
Kumekuwa na mapambano kati ya wajenzi, bahari, vinamasi, na mito tangu maeneo ya kwanza ya bahari na mito kufunikwa ili kutokeza nchi kavu katika karne ya 16, nayo yamefanya mji mkuu wa Pernambuco ugawanywe na mifereji 66 na kuunganishwa kwa madaraja 39. Recife ya leo iko kwenye delta iliyotokezwa na mito ya Capibaribe, Beberibe, Jiquiá, Tejipió, na Jaboatão. Kwa kuwa Recife iko meta mbili hivi juu ya usawa wa bahari, mara kwa mara mawimbi makubwa na mvua nyingi husababisha mafuriko kwenye baadhi ya barabara zake kuu. Kwa kushangaza, wilaya ya Old Recife, makao ya awali, ambayo kwa karne nyingi iliunganishwa na bara kwa sehemu ndogo, nyembamba ya mchanga, mwishowe ilitenganishwa kutoka kwenye bara ili kupanua bandari katika mwaka wa 1960.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Juu: Rua do Bom Jesus
[Picha katika ukurasa wa 23]
Chini: Rua da Aurora
[Picha katika ukurasa wa 24]
Meli za Kampuni ya Dutch West India zikivamia Olinda (kulia) na Recife (kushoto) mwaka wa 1630
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
“Kama tu Venice, Recife ni jiji linaloibuka kutoka majini nalo huakisiwa majini”
[Picha katika ukurasa wa 26]
Forte do Brum na (chini) Forte das Cinco Pontas
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Top: FOTO: NATANAEL GUEDES/P.C.R.; bottom: Bruno Veiga/Tyba/socialphotos.com; map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Fleet: ACERVO FUNDAÇÃO JOAQUIM NABUCO–RECIFE; bottom: MUNDOimagem