Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuiba Vitu Dukani—Ni Nani Hupata Hasara?

Kuiba Vitu Dukani—Ni Nani Hupata Hasara?

Kuiba Vitu Dukani—Ni Nani Hupata Hasara?

HUKO Japani, mwenye duka mmoja alimkamata mvulana akiiba na kuwaita polisi. Polisi walipofika, mvulana huyo alikimbia. Polisi walimkimbiza. Mvulana huyo alipokuwa akivuka reli, aligongwa na gari-moshi, akafa.

Kwa sababu wengi walijua jambo hilo, watu fulani walimshutumu mwenye duka kwa kuwaita polisi. Alifunga duka lake hadi hasira za watu zilipopoa. Alipofungua duka lake tena, watu wengi wanaoiba vitu dukani walilivamia. Hata hivyo, alipokumbuka kisa kilichokuwa kimetokea mapema, aliogopa kuwakabili wezi hao. Watu waliona ni rahisi kuiba katika duka lake. Muda si muda, alilazimika kulifunga kabisa.

Ni kweli kwamba kisa hicho kilikuwa chenye kusikitisha sana kuliko visa vingine, lakini kinatufunza jambo fulani muhimu. Kuiba vitu dukani husababisha hasara kubwa kwa watu wengi na katika njia nyingi. Acheni tuchunguze habari zaidi kuhusu hasara kubwa inayosababishwa na uhalifu huo.

Hasara kwa Wenye Maduka

Wafanyabiashara ulimwenguni pote hupata hasara ya mabilioni ya dola kila mwaka kwa sababu ya wizi wa vitu dukani. Watu wengine wanakadiria kwamba nchini Marekani pekee, wafanyabiashara hupata hasara ya zaidi ya dola bilioni 40. Biashara nyingi zitafilisika iwapo zitapoteza kiasi kikubwa kama hicho cha fedha. Maduka mengi hayawezi kukabiliana na tatizo hilo. Wezi wanapoiba vitu katika njia hiyo, wafanyabiashara wanaweza kupoteza biashara ambayo wamekuwa wakifanya muda wote wa maisha yao.

Luke, mwenye duka huko New York City anasema hivi: “Mbali na mashindano kutoka kwa wafanyabiashara wengine, jambo lingine linalohangaisha ni wizi. Sijui tutaendelea na biashara hii kwa muda mrefu kadiri gani.” Luke hawezi kugharimia mfumo wa ulinzi. Anasema hivi kuhusu wezi hao: “Mtu yeyote anaweza kuiba vitu dukani hata wateja wa kawaida.”

Watu fulani wanaamini kwamba tatizo la Luke si kubwa. Wao husema: “Maduka hayo hupata pesa nyingi kwa hiyo sitasababisha hasara yoyote kwa kuiba.” Lakini, je, kweli maduka hupata faida kubwa sana?

Katika sehemu fulani, maduka huongeza bei ya vitu kwa asilimia 30, 40, au 50 lakini asilimia hiyo haiwakilishi faida wanayopata. Mfanyabiashara hutumia fedha za ziada anazopata kulipia gharama kama vile kodi ya nyumba, kodi ya mapato, mishahara na marupurupu ya wafanyakazi, gharama za udumishaji na za kurekebisha vifaa, bima, stima, maji, simu, mfumo wa ulinzi na gharama nyinginezo. Baada ya kulipia gharama hizo, huenda faida yake ikawa asilimia 2 au 3 tu. Kwa hiyo, mtu anapoiba, anamwibia mfanyabiashara sehemu ya riziki yake.

Vipi Kuiba Vitu Visivyo na Thamani Kubwa?

Akiwa dukani pamoja na mama yake, mvulana mdogo anaenda mahali peremende huwekwa na kufungua pakiti kisha anatumbukiza peremende moja mfukoni. Je, kuiba kitu hicho chenye thamani ndogo kunaweza kuathiri duka hilo?

Kichapo Curtailing Crime—Inside and Out, cha Shirika la Marekani la Biashara Ndogo kinasema hivi: “Huenda kuiba vitu visivyo na thamani kubwa kusionekane kuwa jambo kubwa kwa mwizi ambaye huiba vitu vidogo kama kalamu. Lakini wizi huo huleta hasara kubwa kwa biashara ndogo-ndogo.” Kwa sababu wafanyabiashara hupata faida ndogo sana, lazima mfanyabiashara rejareja auze peremende 900 au mikebe 380 ya supu kila siku ili kulipia hasara ya dola 1,000 inayosababishwa kila mwaka na wizi. Kwa hiyo, wafanyabiashara hupata hasara kubwa wavulana wengi wanapoiba peremende. Tatizo huanzia hapo.

Watu wengi sana, vijana kwa wazee, matajiri kwa maskini, kutoka jamii na malezi mbalimbali wanaiba vitu madukani. Kumekuwa na matokeo gani? Baraza la Kitaifa la Kuzuia Uhalifu nchini Marekani linaripoti kwamba karibu thuluthi moja ya wafanyabiashara nchini humo hulazimika kufunga biashara zao kwa sababu ya wizi huo. Bila shaka, biashara katika nchi nyingine zinakabili tisho hilohilo.

Hasara Ambayo Mteja Hupata

Bei za vitu huongezeka watu wanapoiba madukani. Kwa hiyo, katika sehemu fulani, wateja hulipa dola 300 zaidi kwa mwaka kwa sababu ya wizi. Hilo linamaanisha kwamba ikiwa unapata dola 60 kwa siku, mshahara wako wa juma moja hulipia vitu ambavyo watu wengine wanaiba. Je, una pesa nyingi hivyo za kupoteza? Watu waliostaafu ambao hutegemea malipo ya uzeeni au mama asiye na mwenzi ambaye anang’ang’ana kutegemeza familia yake, anaweza kuathiriwa sana akipoteza mshahara wa juma moja katika njia hiyo. Na kuna hasara nyingine zaidi.

Jamii nzima inaweza kuathirika duka moja linapofungwa. Inaripotiwa kwamba wizi ulifanya duka moja la dawa katika jamii fulani yenye umoja huko Marekani lifungwe. Sasa inawalazimu wazee na walio wagonjwa wasafiri umbali wa kilometa mbili na nusu hivi hadi kwenye duka lingine la dawa. Afisa mmoja alisema: “Wazia ukisafiri umbali huo ukitumia kiti cha magurudumu.”

Hasara Kubwa Ambayo Wazazi Hupata

Bruce ni mwanamume anayeshikilia viwango vya juu vya maadili ambaye huwafundisha watoto wake kuwa wanyoofu. Siku moja, binti yake alikamatwa akiiba. Anasema hivi: “Nilifadhaika sana. Hebu wazia ukipigiwa simu na kuambiwa kwamba binti yako amekamatwa akiiba vitu dukani. Tulitumia miaka mingi kumlea binti yetu awe mtu mzuri, na sasa ona jambo alilofanya. Hatukudhani kwamba angeasi kwa njia hiyo.”

Bruce alikuwa na wasiwasi mwingi kuhusu binti yake na wakati wake ujao. Pia alijiuzulu kuwa mwalimu wa kujitolea wa kidini. “Ningewezaje kuwafundisha wengine kutanikoni? Ningewezaje kuwafundisha kuhusu jinsi ya kuwalea watoto wao nikiwa na dhamiri safi? Nilihisi kuwa sistahili.” Inaonekana binti yake hakufikiria jinsi ambavyo uhalifu wake ungemwathiri baba yake.

Hasara Ambayo Wezi Hupata

Hapo zamani, wasimamizi wa maduka walipomkamata mwizi, mara nyingi walimwonya vikali na kumwachilia. Leo, mara nyingi wenye maduka huwakamata wezi na kuwaita polisi hata kama ni mara yao ya kwanza kuiba. Kwa kufanya hivyo, wezi hutambua kwamba uhalifu wao una matokeo mabaya. Mwanamke mmoja kijana anayeitwa Natalie alijionea ukweli wa jambo hilo.

Natalie anasema: “Kadiri nilivyoiba ndivyo nilivyopata ujasiri. Nilidhani kwamba hata nikikamatwa, pesa ambazo ningemlipa wakili na ada ya mahakama zingekuwa kidogo zikilinganishwa na nguo zenye bei ghali nilizoiba.” Natalie alikuwa amekosea.

Alikamatwa akiiba nguo na akatiwa pingu na polisi. Kwenye kituo cha polisi, alama zake za vidole zilichukuliwa na akafungiwa katika seli na wafungwa wengine. Alikaa humo kwa saa kadhaa huku wazazi wake wakitafuta pesa za kuja kumtoa.

Natalie anamshauri hivi mtu yeyote anayefikiria kuiba: “Fuata ushauri wangu, afadhali ununue nguo au jinzi hiyo.” Anasema kwamba ukiamua kuiba, “utajutia jambo hilo kwa muda mrefu sana.”

Mtu mwenye rekodi ya uhalifu hujuta. Huenda watu wanaoiba vitu dukani wakavunjika moyo wanapogundua kwamba kosa lao halitasahauliwa kabisa, lakini litaonekana tena na tena, kama tu doa kwenye nguo ama shati. Huenda mtu anayeiba vitu dukani akahitajika kutaja kosa lake anapotaka kujiunga na chuo kikuu. Inaweza kuwa vigumu kwake kuruhusiwa kufanya kazi kama daktari, daktari wa meno, au mchora-ramani za majengo. Huenda kampuni zikasita kumwajiri. Na matatizo hayo yanaweza kutokea hata ikiwa ameadhibiwa na korti na haibi tena.

Kuiba vitu dukani kunaweza kutokeza hasara kubwa hata ikiwa mwizi hatafungwa. Hector aliyetajwa mapema katika mfululizo huu, aligundua jambo hilo. Anasema hivi: “Sikuwahi kukamatwa nikiiba.” Lakini alipatwa na madhara. Anasema hivi anapokumbuka jambo hilo: “Nafikiri vijana wanapaswa kuelewa jambo moja: Unavuna unachopanda. Hata kama hutakamatwa na polisi, utapatwa na madhara.”

Kuiba vitu dukani huathiri watu wengine, na vitu ambavyo wezi huiba hutokeza hasara. Mtu yeyote aliye na zoea hilo, anapaswa kuliacha mara moja. Lakini mtu anayeiba vitu dukani anawezaje kupata nguvu za kuacha kuiba kabisa? Je, kuna wakati ambapo uhalifu huo utakomeshwa kabisa?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kuiba vitu dukani hufilisi biashara

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kila mtu hupata hasara watu wanapoiba vitu dukani

[Picha katika ukurasa wa 8]

Kuiba vitu dukani huathiri wakati wako ujao

[Hisani]

Fingerprints: © Morocco Flowers/Index Stock Imagery