Je, Unafahamu Gaucho wa Brazili?
Je, Unafahamu Gaucho wa Brazili?
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Brazili
HUENDA ukauliza, “gaucho ni akina nani?” Gaucho ni wachungaji wa ng’ombe wa Amerika Kusini. Kwa kawaida wao huishi Argentina, lakini kuna gaucho pia huko Uruguai, nchi iliyo kaskazini na mashariki ya Argentina. Na ukitembelea Rio Grande do Sul, jimbo lililo kusini kabisa mwa Brazili huenda ukawaona gaucho wanaoishi huko pia. Iwe wanavaa suruali za gaucho, zinazoitwa bombachas, na kufanya kazi kwenye shamba la farasi, ng’ombe na kondoo au la, leo huenda gaucho wa Brazili wakawa tofauti na vile ulivyotarajia. Walitoka wapi?
Gaucho walitambuliwa kwa sababu ya ukoloni. Katika karne ya 19 na 20 wahamiaji wengi kutoka Ulaya waliokuwa wakitafuta mahali pa kuishi na kufanya kazi, walikaa kusini mwa Brazili. Walileta ustadi wa kutengeneza vitu
kwa mikono na ukulima wa maua. Wahamiaji wengi wakawa gaucho na kuanzisha utamaduni wao. Wazao wa gaucho hula, huvaa na kujitumbuiza kama gaucho wa zamani, na hata wana mtazamo uleule kuhusu kazi. Acheni kwanza tuchunguze kitu fulani kinachotupendeza sote, yaani, chakula.Hawali Tu Nyama Choma na Maté
Usitarajie kukutana na gaucho wengi ambao hula mboga tu! Chakula kikuu cha gaucho ni churrasco, yaani nyama choma ya kondoo au ng’ombe. Mwanzoni hicho ndicho kilikuwa chakula kikuu kwenye ukanda wa malisho ambako walifuga wanyama hao. Isipokuwa uwe na kiwango cha juu cha kolesteroli au huli nyama, huenda ukapenda kujaribu chakula cha kienyeji, rodizio, yaani, nyama mbalimbali zinazouzwa kwenye mkahawa wa gaucho. Huenda pia ukataka kuonja café colonial, yaani, vyakula vinavyoliwa baada ya mlo mkuu na vinywaji, kama vile divai, chai, na kahawa. Bila shaka, kinywaji kinachopendwa sana ni chimarrão, au maté, chai ya majani yaliyosagwa ya mti wa holly. Ingawa ni chungu, unaweza kumwona gaucho akiinywa wakati wowote labda baada ya chakula.
Huenda usipendezwe na ladha chungu ya chimarrão. Hata hivyo, utafurahia hali ya utulivu na urafiki unapokula chimarrão na nyama choma pamoja na marafiki wazuri.
Mavazi na Muziki wa Gaucho
Gaucho walianza kuvalia suruali zinazoitwa bombachas, majoho, viatu, mishipi mipana, kofia, na skafu walipokuwa katika kanda za malisho. Kitabu Insight Guides
—Brazil kinasema: “Utamaduni wa pekee wa gaucho unatambulisha eneo la Rio Grande do Sul walikoishi wachungaji weusi wa ng’ombe kutoka kusini mwa ukanda wa malisho ambao walivalia kofia pana za pekee zenye mkanda, suruali ndefu zilizo pana, vitambaa vyekundu walivyofunga shingoni na viatu vya ngozi.” Wakati wa sherehe, wanawake wa eneo hilo huvalia mavazi yenye kupendeza na ya kiasi. Wageni na gaucho hufurahia dansi wakiwa wamevaa mavazi ya kitamaduni. Hata hivyo, iwe ni chakula, mavazi au vitumbuizo, utamaduni wa gaucho ni mchanganyiko wa utamaduni ulioletwa na wahamiaji kutoka nchi kama vile, Hispania, Italia, Ujerumani, na Ureno na pia kutoka Japani, Lebanoni, Poland, Siria, Ugiriki, Ukrainia, na Urusi na vilevile nchi za Afrika.Mwandishi wa Amkeni! alimhoji José Cláudio Paixão Côrtes, ambaye amechunguza mavazi na dansi za gaucho kwa miaka 50 hivi, naye alisema kuwa gaucho walioishi peke yao walipendezwa na muziki. Kwa hiyo haishangazi kwamba mara nyingi gaucho aliye tu na farasi, angefanya muziki uwe sehemu ya maisha yake. Baadaye, ala za nyuzi kama vile gambusi na gita zilichezwa pamoja na kodiani. Tofauti na vijana wengi katika sehemu nyingine za ulimwengu, vijana wengi gaucho hupenda muziki wao wa kitamaduni kuliko ule wa kisasa.
Pia gaucho hupenda kucheza dansi. Hata gaucho anapohamia eneo la mbali na kwao, bado yeye hupendezwa na dansi zao za kitamaduni. Mbali na dansi za mraba, gaucho hucheza dansi za kutumia upanga na za kurusha mipira mitatu inayoitwa bolas. Mipira hiyo hutengenezwa kwa udongo, mawe, au chuma, na kufungwa pamoja kwa kamba za ngozi. Anapolisha mifugo, gaucho anaweza kurusha mipira hiyo kwenye miguu ya mnyama na kumfunga na hivyo kumfanya asimame.
Wanapenda Nchi Yao
Bado utamaduni na desturi za gaucho hufuatwa katika eneo la Brazili linalopakana na Argentina na Uruguai. Kitabu kimoja cha usafiri kinasema: “Kotekote katika kanda za malisho zenye upepo mkali zinazosimuliwa katika hadithi, bado mchungaji wa ng’ombe gaucho huchunga ng’ombe na kondoo waliofanya eneo la Rio Grande do Sul litajirike.”
Hata hivyo, kuna mengi zaidi yanayoweza kusemwa kuhusu gaucho mbali na chimarrão na nyama choma. Kwa sababu ya kujivunia uzuri wa asili na vitu mbalimbali vinavyopatikana katika eneo lao, gaucho fulani husema kwa mzaha kwamba Mungu alipoumba dunia kwa siku sita, alitumia siku tano kuumba Rio Grande do Sul!
Hata gaucho akiishi na kufanya kazi jijini, yeye huthamini mahali alipozaliwa. Malezi yake, akiwa mhamiaji au mzao wa wahamiaji, yamemsaidia kusitawisha sifa kama kujitegemea, kusema bila woga, ujasiri, kusaidia wengine, na ukarimu.
Gaucho hukumbuka jinsi ambavyo maisha ya zamani ya kulisha mifugo yalivyokuwa rahisi. Hata ikiwa utamaduni wao ulitia ndani mambo yasiyo ya kisasa kama vile kuchunga ng’ombe na farasi, kutumia kamba yenye mipira mitatu, na kula vyakula kama vile mahindi, mizabibu, viazi, mchele, soya, na ngano, bado gaucho hupenda sana nchi yake. Bila shaka, mambo ya kuvunja moyo kama umaskini na ubaguzi huathiri maisha yake. Hata hivyo, gaucho wengi ambao wamejifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova wanaamini kabisa kwamba hivi karibuni dunia yote itakuwa paradiso yenye amani. Wewe pia unaweza kuwa na tumaini hilo.—Luka 23:43; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1-4.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
Kupika aina mbili ya vyakula vya gaucho
NYAMA ILIYOCHOMWA YA NG’OMBE
Kilo 2 za nyama ya ng’ombe, vikombe 21⁄4 vya chumvi ya mawe
Bana nyama hiyo kwa mshikaki na uinyunyizie chumvi. Iweke juu ya moto. Hakikisha upande wenye mafuta umeelekezwa chini hadi ugeuke rangi; kisha ugeuze. Hakikisha nyama hiyo ina mafuta kiasi fulani kwani yanapoyeyuka, hupenya ndani ya nyama na kuifanya iwe tamu zaidi na laini. Fanya hivyohivyo unapochoma nyama ya nguruwe, kuku, au kondoo.—Inatosha watu wanne.
WALI WA CARRETEIRO NA NYAMA YA NG’OMBE YENYE CHUMVI ILIYOKAUSHWA JUANI
Gramu 500 za nyama ya ng’ombe iliyokaushwa juani, kikombe 13⁄4 cha vitunguu vilivyokatwa-katwa, 1⁄4 ya kikombe cha mafuta, maji vikombe 21⁄2, mchele vikombe 21⁄2, vitunguu-saumu 2 vilivyokatwa-katwa
Osha nyama ya ng’ombe iliyokaushwa juani na kuilowesha majini kwa saa nane hivi. Badili maji hayo mara kadhaa. Ikate vipande vidogo-vidogo, ipike katika kikaango chenye mafuta, kitunguu-saumu, na kitunguu. Ongeza mchele kwenye nyama hiyo na uukoroge vizuri. Ongeza maji na kuacha yachemke. Kisha punguza moto na uache mchanganyiko huo uchemke, ukiukoroga mara kwa mara ili sehemu zote ziive vizuri. Wali ukiiva, ukoroge kwa uma na kuuandaa kwa maharagwe.—Kinatosha watu wanne.
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Rio Grande do Sul
[Hisani]
Inset photos: M.A. Decusati
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kucheza dansi ya muziki wa kitamaduni wa gaucho