Mchungi—Rafiki ya Mwanadamu na Mnyama
Mchungi—Rafiki ya Mwanadamu na Mnyama
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA
BILA shaka, hakujawahi kuwa na ukoloni wenye amani kama huo katika historia. Hakuna risasi iliyofyatuliwa; hakuna tone la damu lililomwagwa. Wenyeji hawakukandamizwa, na hakuna nchi iliyoporwa mali yake. Hata hivyo, wavamizi hao waliendelea kutwaa nchi moja baada ya nyingine.
Uvamizi huo ulitukia katika karne ya 20. Lakini uvamizi huo haukuonekana waziwazi kwa sababu wakoloni walikuwa ndege. Ndege hao werevu, ambao sasa wametwaa mabara matano, wanaitwa mchungi au katika jina la kisayansi Bubulcus ibis.
Ukoloni Usio na Kifani
Kwa karne nyingi mchungi alipatikana hasa katika maeneo ya tropiki ya Afrika. Lakini karne moja hivi iliyopita, alifaulu kuifanya Afrika Kusini kuwa koloni yake. Vichapo fulani vinasema kwamba katika miaka ya 1930, idadi kubwa ya ndege hao walivuka Bahari ya Atlantiki ili kufanya Amerika Kusini kuwa koloni yao. Kufikia katikati ya karne ya 20, walifika Florida, na miaka kumi baadaye eneo lao lilianzia Kanada iliyoko kaskazini hadi Argentina iliyoko kusini. Roger Tory Peterson aliandika hivi mnamo 1954: “Ikiwa mchungi . . . aliruka hadi Amerika akisaidiwa tu na upepo, basi yeye ndiye ndege pekee katika historia aliyetoka Ulaya na kuishi katika mabara ya Amerika bila msaada wa mwanadamu.”
Sasa wataalamu wanaochunguza ndege wamekata kauli kwamba kwa kweli ndege hao walifanya jambo hilo la ajabu. Inakadiriwa kwamba kwa msaada wa upepo unaovuma daima, mchungi angeweza kuvuka bahari iliyo kati ya Afrika Magharibi na Amerika Kusini kwa saa 40 hivi. Lakini ndege hao hawakuvuka tu Bahari ya Atlantiki. Wengine walielekea mashariki hadi New Zealand. Katika kipindi hichohicho, walipatikana katika sehemu nyingi za Ulaya na Asia, ambako eneo lao kubwa sasa linaanzia Rasi ya Iberia iliyoko magharibi hadi Japani iliyoko mashariki.
Mchungi huishi bila kuhama katika nchi ambako hali ya hewa ni nzuri; lakini katika maeneo yenye majira ya baridi kali, yeye huhamia maeneo yenye joto makinda yake yanapoweza kuruka. Yeye huendelea na safari zake ndefu na zenye kuvutia, naye huonekana mara nyingi katika visiwa vilivyo mbali vya Pasifiki au hata katika Antaktiki.
Kilichowawezesha Kuwa na Eneo Kubwa
Sababu kuu iliyomfanya ndege huyo afaulu kuwa na eneo kubwa ni uwezo wake wa kuishi maeneo mbalimbali na uhusiano wake na binadamu, hasa wafugaji ng’ombe. Ingawa yangeyange wengi hula viumbe wa majini, mchungi, ambaye ni wa jamii ya yangeyange hupendelea kula wadudu. Kwa kawaida yeye hufuatana na ng’ombe, ingawa anaweza pia kufuatana na tembo, kangaruu, trekta, au hata mioto ya misitu, yaani, atafuata kitu chochote kinachofichua wadudu anaokula.
Bila shaka, mchungi anaweza kujitafutia chakula bila kusaidiwa na yeyote, lakini ng’ombe wanapotembea kwenye nyasi, wao hufichua mahali ambapo panzi, nzi, na mbawakawa wamejificha. Mchungi anayetembea kando ya ng’ombe akiwa
chonjo anaweza kunyafua wadudu wanaoruka. Kwa hiyo ng’ombe huwasaidia mchungi kutafuta na kushika windo lao na kulingana na kadirio moja, mchungi anaweza kushika wadudu wawili au watatu hivi kwa dakika moja. Wataalamu wa ndege wanakadiria kwamba kushirikiana na ng’ombe kunaweza kupunguza nguvu ambazo mchungi hutumia kwa asilimia 30 na kuongeza idadi ya wadudu anaonasa kwa asilimia 50.Mchungi hakufaulu kumiliki ulimwengu kwa sababu tu alikuwa na mwenzi wa kumsaidia kuwinda. Mchungi ni ndege mwenye nguvu. Huenda wakaonekana kuwa wanaruka kwa shida sana hasa wanapolinganishwa na mabata au njiwa ambao huruka kwa nguvu na kwa njia ya moja kwa moja. Lakini mchungi anaweza kuvuka jangwa la Sahara na kama ilivyotajwa awali, amewahi kuruka kilometa 4,000 kutoka Afrika Magharibi hadi Amerika Kusini.
Inaonekana kwamba ndege hao hupenda kuhama-hama, na tabia hiyo huwafanya wawe na eneo kubwa. Ni ndege gani anayekula wadudu ambaye angeweza kusafiri eneo la mbali sana kusini kama vile Antaktiki, ili tu kujionea maeneo hayo?
Walipokuwa wakihamia maeneo ya mbali, ndege hao walipata maeneo yaliyowafaa karibu kila mahali walipoenda. Kila bara walilofika, wakulima walikuwa wakifuga ng’ombe katika mashamba yao makubwa au kunyunyizia maji mashamba yaliyokuwa na wadudu wengi. Kwa hiyo mchungi walihamia mashamba hayo na kuongezeka.
Huwanufaisha Wanadamu na Wanyama
Ni rahisi kuwaona ndege hao kwani wana manyoya meupe, hupenda kushirikiana, nao hufuatana na ng’ombe. Mchungi weupe wanaoruka kwa mfuatano hurembesha mazingira na pia kufanya kazi muhimu ya kudhibiti wadudu wasumbufu. Pindi moja, mchungi 40,000 hivi walionekana huko Tanzania wakila kundi kubwa la panzi. Wakulima fulani huona mchungi kuwa ndege muhimu sana hivi kwamba wamewaleta kwenye mashamba yao ili wawasaidie kudhibiti wadudu wanaoharibu mazao yao. Mchungi mmoja anaweza kula zaidi ya panzi na chenene 600 kwa siku.
Pia ng’ombe hunufaika, kwa kuwa mchungi hula nzi na wadudu wengine ambao huwasumbua. Inaonekana kwamba ng’ombe hujua kuwa mchungi ni rafiki zao kwani wao huwavumilia ndege hao watundu ambao mara kwa mara hupanda juu ya migongo yao.
Kuishi Pamoja
Mchungi hupenda kuishi pamoja, iwe wanataga mayai, wanalala, au wanakula. Wakati wa majira ya kutaga mayai, wao hukubali kuishi katika mti mmoja mkubwa pamoja na ndege wengine wa jamii ya kulasitara au korongo. Inaonekana kwamba jamii zote hunufaika kwa kuishi mahali pamoja kwani kufanya hivyo huzuia wasivamiwe na adui. Ndege wanaotaga mayai huwa na kelele na shughuli nyingi. Mara nyingi mchungi huiba vijiti kutoka kwenye viota vilivyo karibu, jambo ambalo hufanya kuwe na ugomvi mwingi. Mchungi wengine huning’inia kwenye viota vyao huku wengine wakitafuta kwa bidii vijiti vilivyoanguka chini ya mti ambavyo wanaweza kutumia. Kwa kawaida, ndege wa jamii yao, yaani korongo na kulasitara, ambao hujenga viota vyao vikubwa kwenye matawi yaliyo juu zaidi, hupuuza fujo zinazoendelea karibu nao.
Uchumba wenye kuvutia wa mchungi unatia ndani kujinyoosha, kugonga-gonga midomo, na ndege wa kiume kuonyesha kwa madaha manyoya yake ya manjano wakati wa majira ya kutaga mayai. Mzazi mmoja anapowasili kwenye kiota, mwenzi wake humkaribisha kwa “salamu” zinazotia ndani kuonyesha kwa madaha manyoya yake ya mgongoni. Si vigumu kuona maonyesho hayo kwa kuwa ndege hao hawawaogopi wanadamu.
Iwe unatalii Afrika, unapita katika maeneo ya kufuga ng’ombe huko Amerika Kaskazini, au unatembelea mashamba ya mpunga katika nchi za Mashariki, huenda ukaona ndege hao wenye kuvutia. Huenda wakawa wanatembea kando ya miguu ya tembo, au wamepanda kwa ujasiri mgongoni mwa fahali, au wakawa wanarudi tu nyumbani wakalale jua linaposhuka. Popote utakapowaona, bila shaka wataongeza umaridadi wa mandhari unayotazama, huku pia wakiwanufaisha wanadamu na wanyama. Ukoloni wao wenye kuvutia umekuwa mojawapo ya ukoloni wenye kunufaisha zaidi ulimwenguni.
[Picha katika ukurasa wa 14, 15]
Mchungi wamefaulu kutwaa mabara matano, nao wana uhusiano mzuri na tembo na ng’ombe
Guyana
Australia
Kenya
Marekani
Hispania
[Hisani]
© Joe McDonald