Kukanda Mtoto
Kukanda Mtoto
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA
ANITA, mama mchanga kutoka Nigeria, humwosha binti wake mchanga na kumkanda kwa uangalifu. Mama na mtoto hufurahia sana jambo hilo. Anita anasema hivi: “Kukanda watoto ni zoea la kawaida la mama wa Nigeria. Mama yangu alinikanda mimi na ndugu zangu. Kukanda ni njia nzuri ya kufanya misuli ya mtoto iwe na nguvu na kumfanya astarehe. Mimi humwimbia na kumzungumzia mtoto wangu ninapomkanda, naye hucheka na kutabasamu. Hilo ni jambo linalofurahisha sana!”
Kukanda mtoto ni jambo la kawaida katika nchi nyingi, nalo linaanza kupendwa katika nchi fulani za Magharibi. Kulingana na Shirika la Kukanda Watoto la Hispania, kukanda ni njia ya wororo na yenye kupendeza ya mzazi kuwasiliana na mtoto wake kimwili na kihisia. Inatia ndani kupapasa kwa wororo lakini kwa nguvu nyayo, miguu, mgongo, kifua, tumbo, mikono, na uso wa mtoto.
Mtoto hunufaikaje anapokandwa? Kwanza kabisa, yeye huhisi kwamba wazazi wake wanampenda na kumjali. Mtoto hahitaji tu kulishwa bali pia anahitaji upendo wa wazazi. Kwa kuwa mtoto anaweza kuhisi anapoguswa akiwa bado mchanga sana, anapokandwa kwa wororo na mama au baba anaonyeshwa kwamba anapendwa. Mambo mengi ya kimwili na ya kihisia yanaweza kupitishwa kwa mtoto. Kwa hiyo, kukanda kunaweza kuimarisha upendo kati ya wazazi na mtoto wao tangu anapozaliwa.
Mbali na kuwa njia ya kuonyesha upendo, kukanda kunaweza kumsaidia mtoto astarehe, na hilo linaweza kumfanya alale vizuri na kwa muda mrefu zaidi. Kukanda mwili kunaweza kusaidia misuli iwe na nguvu na pia kufanya mifumo ya kuzungusha damu, kumeng’enya chakula, na kupumua ifanye kazi vizuri zaidi. Watu fulani husema kwamba mfumo wa kinga wa mtoto hunufaika pia. Na kwa sababu hisi za mtoto za kugusa, kuona, na kusikia huwa zimechochewa, kukanda kunaweza pia kumsaidia kukumbuka mambo na kujifunza.
Hospitali fulani zimefanya utafiti kuhusu manufaa ya kukanda watoto. Kwa mfano, uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba vitoto vilivyozaliwa kabla ya wakati na ambavyo vilikandwa viliweza kuondoka hospitalini siku saba mapema kuliko vile ambavyo havikukandwa, na viliongeza uzito kwa asilimia 47 kuliko vile ambavyo havikukandwa.
Ni wazi kwamba si watu wazima tu hunufaika na kukandwa. Bila shaka, kukanda watoto hutimiza mengi zaidi ya kufanya misuli yao iwe na nguvu na wastarehe. Kukandwa pia ni njia ya kuonyesha mtoto upendo kwa mikono na vidole vyororo, na tabasamu.