Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mwingereza “Stadi Ambaye Alisahauliwa”

Mwingereza “Stadi Ambaye Alisahauliwa”

Mwingereza “Stadi Ambaye Alisahauliwa”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

ROBERT HOOKE, aliyetajwa na watu walioishi wakati mmoja naye kuwa “mtu aliyevumbua vitu vingi zaidi ambaye amepata kuishi,” sasa anasifiwa kuwa Leonardo da Vinci wa Uingereza. * Hooke alizaliwa mnamo 1635. Aliwekwa kuwa msimamizi wa majaribio ya kisayansi katika kituo cha Royal Society cha London mnamo 1662 kisha akawa katibu mwaka wa 1677. Alikufa mwaka wa 1703. Hata hivyo, licha ya umashuhuri wake wa kisayansi, Hooke alizikwa katika kaburi lisilojulikana kaskazini mwa London.

Katika miaka ya karibuni, wanasayansi na wanahistoria wamejitahidi sana kumrudishia sifa Hooke, ambaye mwandishi wa wasifu Stephen Inwood anamrejelea kuwa “stadi ambaye alisahauliwa.” Katika mwaka wa 2003, wakati wa kuadhimisha miaka 300 tangu Hooke afe, kituo cha kutazama angani kinachoitwa Royal Observatory Greenwich kilichoko London, kilikuwa na maonyesho ya baadhi ya uvumbuzi na ugunduzi wake wa pekee. Lakini Robert Hooke alikuwa nani, na kwa nini karibu asahauliwe kabisa?

Urithi wa Hooke

Hooke alikuwa msomi na mvumbuzi mwenye akili nyingi. Alibuni vitu vingi kama vile mtaimbo wa magari; mboni mwanga ambayo hudhibiti ukubwa wa tundu la kupitishia mwanga katika kamera; na springi ya gurudumu la kusawazisha saa. Pia, alibuni sheria ya Hooke, ambayo ni kanuni ya hesabu inayotumika hadi leo kufafanua jinsi ambavyo springi hujivuta. Isitoshe, alibuni kifaa cha kupiga hewa kwa ajili ya Robert Boyle, mwanafizikia na mwanakemia mashuhuri wa Uingereza.

Hata hivyo, mojawapo ya ubuni bora zaidi wa Hooke ulikuwa hadubini yenye lenzi mbili, ambayo baadaye iliundwa na Christopher Cock, mtengenezaji vifaa maarufu huko London. Kwa kutumia hadubini yake, Hooke alikuwa mtu wa kwanza kuona na kufafanua matundu kama ya sega katika kizibo. Baadaye, maelezo yake yalitumiwa kufafanua chembe za viumbe-hai.

Kitabu Micrographia (Michoro Midogo) cha Hooke, kilichochapishwa mnamo 1665, kilimfanya awe mashuhuri. Kilikuwa na michoro sahihi na maridadi ya wadudu ambao Hooke aliona kwa kutumia hadubini yake. Mchoro wake maarufu zaidi ni ule wa kiroboto. Mchoro huo uliokuwa na upana wa sentimeta 30 na urefu wa sentimeta 45 unaonyesha kucha, miiba, na mwili mgumu wa kiroboto. Matajiri waliosoma kitabu chake walishangaa kujua kwamba viumbe hao wadogo huishi katika miili ya wanadamu. Inasemekana kwamba wanawake walizimia walipoona picha hiyo!

Baada ya kutumia hadubini kuitazama ncha ya sindano iliyotengenezwa na wanadamu na kuilinganisha na vitu vya asili, Hooke aliandika hivi: “Hadubini hutuwezesha kuona vitu vingi vyenye ncha kalikuliko ya sindano. Alitaja vitu kama vile nywele, malaika, na kucha za wadudu, miiba, ndoana, na nyuzinyuzi za mboga. Alihisi kwamba ‘kazi hizo za Asili’ zinafunua kwamba yule aliyevifanya ni Mweza-Yote. Kichapo Encyclopædia Britannica kinasema kwamba “kwa mara ya kwanza” hadubini ilifunua kuwa “viumbe-hai ni vitu vyenye kutatanisha sana.”

Hooke alikuwa mtu wa kwanza kuchunguza visukuku kwa kutumia hadubini. Hilo lilifanya akate kauli kwamba vilikuwa mabaki ya viumbe waliokufa muda mrefu sana uliopita. Kitabu Micrographia kilikuwa na maelezo mengi zaidi yenye kustaajabisha ya kisayansi. Kwa kweli, mwekaji-kumbukumbu za kila siku Samuel Pepys, aliyeishi wakati mmoja na Hooke, alisema kwamba Micrographia “ndicho kitabu kilichoandikwa na mtu mwenye akili sana ambacho nimewahi kusoma.” Allan Chapman, mwanahistoria wa sayansi kwenye Chuo Kikuu cha Oxford, alisema kwamba kitabu hicho ni “mojawapo ya vitabu vyenye uvutano mkubwa zaidi katika ulimwengu wa sasa.”

Kujenga Upya London

Baada ya Moto Mkubwa kuteketeza jiji la London mnamo 1666, Hooke aliwekwa kuwa soroveya. Alishirikiana kwa ukaribu na rafiki yake, Christopher Wren, aliyekuwa mwanasayansi na soroveya wa mfalme kujenga upya jiji hilo. Mojawapo ya vitu vingi ambavyo Hooke alichora ni ramani ya ujenzi ya Nguzo ya London. Nguzo hiyo yenye kimo cha meta 62, ilijengwa ili kuwa ukumbusho wa moto huo. Hooke alinuia kutumia Nguzo hiyo, ambayo ndiyo nguzo ndefu zaidi ulimwenguni iliyojengwa kwa mawe tu, kujaribu nadharia zake kuhusu nguvu za uvutano.

Ingawa inasemekana kwamba Wren ndiye aliyechora ramani za ujenzi za kituo cha kutazama angani kinachoitwa Royal Observatory Greenwich, Hooke alichangia sehemu kubwa katika uchoraji wa kituo hicho. Kati ya majengo mengi ambayo Hooke alichora ramani zake ni Montague House, jengo lililotumiwa kama Jumba la Makumbusho la kwanza huko Uingereza.

Hooke alikuwa mwastronomia stadi sana na alikuwa kati ya watu wa kwanza kutengeneza hadubini inayorudisha nuru, ambayo aliipa jina la mwanahisabati na mwastronomia Mskoti James Gregory. Hooke aligundua kwamba sayari Sumbula huzunguka kwenye mhimili wake, na michoro yake ya Mihiri ilitumiwa karne mbili baadaye kukadiria sayari hiyo huzunguka kwa mwendo gani.

Kwa Nini Alisahauliwa?

Mnamo 1687, Isaac Newton alichapisha kitabu Mathematical Principles of Natural Philosophy. Kitabu hicho kilichochapishwa miaka 22 baada ya kitabu Micrographia cha Hooke, kilizungumzia sheria kuhusu mwendo, kutia ndani sheria ya uvutano. Lakini kama Allan Chapman anavyosema, Hooke ndiye “aliyevumbua nadharia nyingi kuhusu nguvu za uvutano kabla ya Newton.” Utafiti wa Newton kuhusu nuru pia ulitegemea kitabu cha Hooke.

Kwa kusikitisha, mabishano kuhusu elimu-nuru na nguvu za uvutano yaliharibu uhusiano wa wanaume hao. Hata Newton aliondoa marejeo ya Hooke katika kitabu Mathematical Principles. Kulingana na ripoti moja, Newton pia alijaribu kufuta habari zilizoeleza mambo ambayo Hooke alifanya kuchangia maendeleo ya kisayansi. Isitoshe, vifaa vya Hooke, ambavyo vingi alivitengeneza kwa mkono, makala zake nyingi, na picha halisi ya Hooke ilitoweka baada ya Newton kuwekwa kuwa msimamizi wa Royal Society. Kwa sababu ya mambo hayo, Hooke alisahauliwa kwa zaidi ya karne mbili.

Jambo la kustaajabisha ni kwamba katika barua aliyomwandikia Hooke ya Februari 5, 1675, Newton aliandika maneno haya maarufu: “Ikiwa nimefaulu kuona mbali ni kwa sababu nimesimama juu ya mabega ya Majitu kama wewe.” Akiwa msanifu-ujenzi, mwastronomia, mwanasayansi wa kufanya majaribio, mvumbuzi, na soroveya, Robert Hooke alikuwa jitu katika siku zake.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Da Vinci alikuwa mchoraji, mchongaji-sanamu, mhandisi, na mvumbuzi Mwitaliano aliyeishi mwishoni mwa karne ya 15 na mwanzoni mwa karne ya 16.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Michoro ya Hooke ya chembe za theluji na sakitu

[Picha katika ukurasa wa 26]

Muundo wa hadubini ya Hooke

[Picha katika ukurasa wa 27]

Hooke alikuwa mtu wa kwanza kufafanua matundu kama ya sega katika kizibo

[Picha katika ukurasa wa 27]

Kitabu “Micrographia” cha Hooke kilionyesha vitu alivyoona kwa kutumia hadubini

[Picha katika ukurasa wa 27]

Ukubwa uliokadiriwa wa kiroboto

Inasemekana kwamba wanawake walizimia walipoona mchoro wa Hooke wa kiroboto

[Picha katika ukurasa wa 28]

Nyumba ya Montague ilikuwa mojawapo ya michoro mingi ya ujenzi ya Hooke

[Picha katika ukurasa wa 28]

Mchoro wa Hooke unaoonyesha sheria yake kuhusu jinsi springi hujivuta

[Picha katika ukurasa wa 28]

Nguzo ya Ukumbusho ya London ndiyo nguzo ndefu zaidi ulimwenguni iliyojengwa kwa mawe tu

[Picha katika ukurasa wa 28]

Kituo cha Royal Observatory

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Spring, microscope, and snowflakes: Images courtesy of the Posner Memorial Collection, Carnegie Mellon University Libraries

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]

Images courtesy of the Posner Memorial Collection, Carnegie Mellon University Libraries

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 28]

Spring diagram: Image courtesy of the Posner Memorial Collection, Carnegie Mellon University Libraries; London’s Memorial Tower: Matt Bridger/DHD Multimedia Gallery; Royal Observatory: © National Maritme Museum, London