“Je, Wewe Husherehekea Sikukuu ya Akina Nyanya?”
“Je, Wewe Husherehekea Sikukuu ya Akina Nyanya?”
ILIKUWA asubuhi katika majira ya baridi kali. Natalia, msichana mwenye umri wa miaka 16 nchini Poland, alikuwa akisubiri treni, wakati waandishi wawili wa habari wa gazeti fulani walipomkaribia na kumwuliza, “Je, wewe husherehekea Sikukuu ya Akina Nyanya?”
Sikukuu ya Akina Nyanya, Sikukuu ya Akina Babu, Sikukuu ya Akina Mama, Sikukuu ya Wanawake, na Sikukuu ya Walimu ni siku maalum nchini Poland. Kwa kawaida, watoto wadogo husherehekea Sikukuu ya Akina Nyanya, na Sikukuu ya Akina Babu, kwa kutengeneza kadi za salamu, wakati watoto wakubwa wanawapa babu na nyanya zao zawadi au maua.
Mwanzoni, Natalia alikosa jibu alipoulizwa swali hilo. Lakini mara baada ya kutoa sala kimyakimya, aliwaambia hivi wale waandishi wa habari, “Mimi ni Shahidi wa Yehova, na huwa sisherehekei Sikukuu ya Akina Nyanya.” Inaonekana jibu hilo liliwashangaza waandishi wa habari. Natalia akatabasamu kisha akasema: “Ninaishi na nyanya yangu, kwa hiyo ninaweza kumpa maua, kuzungumza naye, na kumwonyesha jinsi ninavyothamini fadhili zake kila siku. Sasa kwa nini nimshukuru mara moja tu kwa mwaka?”
Majibu hayo yaliwavutia sana waandishi hao wa habari, kama vile ambavyo yangeweza kukuvutia wewe pia. Kesho yake asubuhi gazeti la habari lilikuwa na maelezo ya Natalia na picha yake.
Je, jambo hili limekufanya ujiulize kama wewe pia umejiandaa kuongea kuhusu imani na msimamo wako, ikiwa bila kutarajia utaulizwa mambo hayo? Waabudu wa kweli wa Mungu wanafanya kila wanaloweza ili kumletea sifa kwa kuwa tayari kutoa sababu kwa yale wanayoamini na wanafanya hivyo kwa hiari kila inapohitajika.—1 Petro 3:15.