Tungefanya Nini Bila Punda?
Tungefanya Nini Bila Punda?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ETHIOPIA
PUNDA wamekuwa muhimu sana kwa usafiri kwenye mitaa ya Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ambayo ni nchi ya 16 kwa idadi ya watu duniani. Madereva wa magari wamewazoea na wanatambua kwamba punda wanajua wanakoenda na watafika huko kwa njia yoyote ile. Punda hawaogopi kunapokuwa na msongamano wa magari, wanabeba mizigo yao mizito kwa ustadi, pia hawaangalii nyuma. Kwa hiyo, kama hungependa kuguswa na makaa, kinyesi cha ng’ombe au mzigo wowote waliobeba, afadhali uwapishe!
Inakadiriwa kwamba idadi ya punda nchini Ethiopia ni kama milioni tano, hiyo ni sawa na punda mmoja kwa kila watu 12. Mamilioni ya Waethiopia huishi juu ya vilima, ambavyo vimetenganishwa na mabonde marefu. Sehemu za uwanda wa juu zimetenganishwa na vijito vingi vidogo. Pesa nyingi sana zingehitajika kujenga madaraja au hata barabara za udongo katika maeneo kama hayo. Kwa hiyo punda, ambaye ni mnyama mvumilivu, huandaa njia bora sana ya usafiri.
Punda anaweza kustahimili halihewa yoyote ya Ethiopia, iwe katika sehemu ya chini iliyo kavu na yenye joto au kwenye milima. Pia anaweza kupita kwenye miteremko mikali, njia nyembamba za miguu, bonde la mto lililojaa mawe, njia zenye matope, na sehemu nyingine zilizo ngumu kupita. Anaweza kupita mahali ambapo farasi au ngamia hawawezi. Kwa mamilioni ya watu, punda ndiyo usafiri pekee, hasa katika miji ambayo nyumba nyingi haziwezi kufikiwa kwa magari.
Punda wanaweza kupita njia zenye kona kali na kupitia katika vijia vyembamba sana. Hawahitaji magurudumu ya bei ghali na mara nyingi hawana shida kupitia sehemu zinazoteleza. Wao hubeba mizigo iliyo na umbo na ukubwa wowote na wanaweza kuifikisha mahali popote. Madereva wa magari waliokasirika wanapoketi wakipiga honi kwa sababu ya msongamano wa magari, punda hupata njia kwa urahisi. Hakuna polisi anayeweza kufikiria kumtoza
punda faini kwa kupitia upande usiofaa wa barabara. Mahali pa kuegesha si tatizo. Punda anaweza kuuzwa kwa dola 50 lakini huwezi kulinganisha bei yake na gharama za kusafiri kwa gari.Punda Katika Mji Mkuu
Asubuhi kuna maelfu ya punda wanaosafiri kwenda Addis Ababa, jiji lililo na zaidi ya watu 3,000,000, na mara nyingi hao punda wametoka umbali wa zaidi ya kilometa 25. Jumatano na Jumamosi huwa siku zenye shughuli nyingi sana kwa sababu ni siku za soko. Safari hii inachukua karibu saa tatu na inabidi watu watoke nyumbani alfajiri. Mara nyingine wenye punda hutembea kando yao, lakini mara nyingi wao huhitaji kukimbia ili kuwafikia punda hao.
Mara nyingi punda hubeba mifuko ya nafaka, mboga, kuni, saruji, na makaa, pia mitungi ya chuma iliyo na mafuta ya kupikia na masanduku yenye chupa za vinywaji. Punda wengine wanaweza kubeba mizigo yenye uzito wa kilo 90 au hata zaidi. Mizigo mirefu kama vile miti ya mianzi au mikalitusi, hufungwa kwenye migongo yao na kuburutwa barabarani. Mizigo ambayo hufanya watu wawatazame sana wanyama hao ni ile ya matita makubwa ya majani makavu au nyasi kavu ambazo huwa karibu kuwafunika wanyama hao.
Asubuhi wanapoenda sokoni wakiwa wamebeba mizigo mizito punda hao huenda kasi sana. Lakini mizigo hiyo ikiondolewa na kuuzwa, wao hurudi nyumbani polepole, mara nyingine hata wakisimama kula majani yaliyo kandokando ya njia. Siku ambazo hawapeleki vitu sokoni bado wao hutumika kufanya kazi za nyumbani kama kuteka maji na kuleta kuni. Pia watu huazima au kukodisha punda hao. Punda fulani hutumiwa kwa ajili ya biashara ya usafirishaji. Katika sehemu fulani punda huvuta mkokoteni au hata mara nyingine punda wawili huvuta gari dogo la kukokotwa.
Wanapaswa Kuheshimiwa
Punda hawana mahitaji mengi. Wao hujitafutia chakula na wanaweza kula karibu kila kitu. Wanapotendewa vizuri wao hushikamana na mabwana wao. Punda husemekana pia kuwa werevu zaidi ya farasi. Pia wana kumbukumbu nzuri sana. Bila kuandamana na mtu yeyote wanaweza kuteka maji yaliyo umbali wa kilometa nane iwapo tu kutakuwa na mtu wa kujaza na kumimina kwenye pande zote mbili. Punda pia huwekewa kengele ili watu kwenye nyumba zilizo njiani wawasikie na hivyo kupokea mizigo waliyobeba.
Hata punda wawe ni wafanyakazi wenye bidii kadiri gani, kuna kiasi cha mizigo ambacho hawakubali kubeba, na pia kuna wakati wanahitaji kupumzika. Katika hali hizi, au wakati mzigo umewekwa kwa njia inayoumiza, wao hulala chini. Nyakati kama hizo ndizo watu hushindwa kuwaelewa na hivyo kuwatukana au kuwapiga. Labda unaweza kukumbuka jambo kama hilo lilitukia katika nyakati za Biblia.—Hesabu 22:20-31.
Punda wanahitaji kutunzwa. Inahuzunisha wakati ambapo mzigo haufungwi vizuri na unaposonga unafanya punda kuingia kwenye shimo na kuvunjika miguu. Vidonda, vimelea, kuoza mguu, nimonia na shida nyingine zinaweza kuwafanya wanyama hao wenye bidii wawe dhaifu. Kwa sababu hiyo, kituo cha kuchunguza na kutibu punda kimeanzishwa huko Debre Zeyit, mji ambao uko karibu na Addis Ababa. Kituo hicho kina kompyuta, vyumba vya matibabu, magari ya kuwabeba punda wagonjwa na pia sehemu ya kufanyia upasuaji. Kwa hiyo, mnamo 2002, punda wapatao 40,000 walipata matibabu.
Mzee wa ukoo Abrahamu alivuka milima akitumia punda wake kuelekea Mlima Moria. (Mwanzo 22:3) Katika historia yote ya taifa la Israeli, punda alitumiwa sana katika maisha ya kila siku. Hata Yesu alitumia punda kuingia kwa ushindi huko Yerusalemu.—Mathayo 21:1-9.
Punda ametumika kwa muda mrefu nchini Ethiopia. Hata hivyo, hajapoteza umuhimu wake katika maisha ya watu. Ingawa muundo wa magari umebadilika kadiri ambavyo wakati umepita, bado punda ana muundo uleule. Hakika punda anastahili kuheshimiwa!
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
‘The Donkey Sanctuary’, Sidmouth, Devon, UK