Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ “Kutazama televisheni siku nzima, kutokula milo pamoja kama familia, na kubuniwa kwa magari ya kusukuma ya watoto wakiwa wametazama mbele tu,” kunawazuia wazazi na watoto kuwasiliana. Tokeo moja ni kwamba watoto wanapoanza kwenda shule, wao “hukasirika kama vichaa” wanaposhindwa kujieleza. —THE INDEPENDENT, UINGEREZA.
▪ Nchini Hispania asilimia 23 ya watoto huzaliwa nje ya kifungo cha ndoa. Nchini Ufaransa idadi hiyo ni asilimia 43; nchini Denmark ni asilimia 45; na nchini Sweden ni asilimia 55.—INSTITUTO DE POLÍTICA FAMILIAR, HISPANIA.
▪ Asilimia 33 ya Waingereza hulala muda unaopungua saa tano usiku, na hilo huwafanya “wasiwe na uwezo mzuri wa kukaza uangalifu, wakose kumbukumbu, [na] wawe na hisia zenye kubadilika-badilika.” Huenda kukosa usingizi kukaongeza “hatari ya kunenepa kupita kiasi, kisukari, kushuka moyo, kutalikiana na kusababisha aksidenti mbaya za magari.” —THE INDEPENDENT, UINGEREZA.
Ujeuri “Ili Kupitisha Wakati Tu”
“Visa vya vijana kuwapiga watu na kuwavunjia heshima huku wakirekodi vitendo hivyo katika video kwa kutumia simu zao za mkononi vinaongezeka,” linasema gazeti la Kihispania El País. Watu fulani hawaponi baada ya kupigwa sana kwa njia hiyo. Kwa nini vijana hufanya uhalifu huo? “Hawafanyi hivyo ili kuiba au kwa sababu ya ubaguzi wa rangi au kwa sababu wao ni washiriki wa genge fulani. Wanafanya hivyo ili kupitisha wakati tu,” linaeleza gazeti XL. “Nyakati nyingine wao huwa wamelewa na wakati mwingine hawajalewa,” anasema Vicente Garrido, mwanasaikolojia ambaye huchunguza uhalifu. “Hata hivyo, jambo linaloonekana katika visa vyote ni kwamba hawana huruma.”
Watu Hawajishughulishi Sana na Magonjwa ya Kitropiki
Magonjwa mengi ya kitropiki hayafanyiwi utafiti wa kitiba. Kwa nini? “Hali yenye kusikitisha ni kwamba . . . makampuni ya dawa hayatafuti [dawa mpya],” anasema Michael Ferguson, mwanabiolojia wa molekuli katika Chuo Kikuu cha Dundee, Scotland. Hakuna faida ya kifedha ambayo itachochea makampuni hayo kufanya hivyo kwani hayawezi kurudisha pesa ambazo yanatumia kutengeneza dawa mpya. Makampuni hayo huona ni afadhali kutengeneza dawa za magonjwa kama vile Alzheimer, kunenepa kupita kiasi, na kukosa nguvu za kujamiiana kwani dawa hizo huleta pesa nyingi. Wakati huohuo, gazeti New Scientist, linasema kwamba inakadiriwa kuwa “kila mwaka watu milioni moja ulimwenguni pote hufa kutokana na malaria, na bado ni vigumu sana kupata matibabu salama na yanayofaa.”
“Wanunuzi” Wachanga
Kulingana na Chuo Kikuu cha La Sapienza, huko Rome, Italia, watoto wenye umri wa miaka mitatu wanaweza kutofautisha nembo za bidhaa sokoni, na wanapofikia umri wa miaka minane wanakuwa “wanunuzi.” Matangazo ya biashara kwenye televisheni huathiri sana maisha yao na kuwageuza kuwa “madikteta” wadogo ambao huwalazimisha wazazi wao wawanunulie bidhaa fulani, linasema gazeti La Repubblica. “Hatari ni kwamba,” linasema gazeti hilo, watoto “huishi katika ulimwengu usio halisi, ambao wanaamini hawawezi kuishi bila kitu chochote kinachotangazwa (na kununuliwa).”
Roboti Yenye “Mimba”
Wahudumu wa afya ambao huwashughulikia wanawake wajawazito wamekuwa wakijizoeza kufanya kazi yao kwa kutumia wajawazito halisi. Lakini sasa, ripoti ya Shirika la Habari la Associated Press linasema, “roboti inayotenda kama mwanamke anayekaribia kujifungua,” inayoitwa Noelle, “imeanza kutumiwa sana.” Roboti hiyo “yenye mimba,” ambayo imeratibiwa ionyeshe mapigo ya moyo na kupanuka kwa mlango wa kizazi, inaweza kuratibiwa kuiga matatizo mbalimbali yanayotokea wakati wa kujifungua na kupunguza au kuongeza muda wa kujifungua. “Mtoto” ambaye Noelle anazaa anaweza kuwa na rangi ya waridi kuonyesha ana afya, au rangi ya bluu kuonyesha hana oksijeni. Kwa nini roboti inatumiwa kwa ajili ya mazoezi? “Ni afadhali kufanya kosa unaposhughulika na roboti inayogharimu dola 20,000 kuliko unaposhughulika na mjamzito halisi,” inasema ripoti hiyo.