Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Toledo—Mchanganyiko wa Utamaduni wa Enzi za Kati

Toledo—Mchanganyiko wa Utamaduni wa Enzi za Kati

Toledo—Mchanganyiko wa Utamaduni wa Enzi za Kati

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

KATIKATI ya Rasi ya Iberia kuna mlima wa matale ambao umezungukwa na Mto Tagus kwenye pande zake tatu. Kwa karne nyingi mto huo umetokeza majabali yanayozingira mlima huo. Jiji la Toledo lilijengwa kwenye majabali hayo nalo limekuja kuonwa kuwa linatambulisha Hispania na utamaduni wake.

Leo, barabara nyembamba zinazojipinda za sehemu ya kale ya Toledo humfanya mgeni akumbuke Enzi za Kati. Malango, kasri, na madaraja ya jiji hilo ni ya mtindo wa Enzi za Kati na yanaonyesha wakati ambapo Toledo lilikuwa mojawapo ya majiji muhimu zaidi Ulaya.

Hata hivyo, Toledo si kama majiji mengine ya Ulaya. Hata kituo cha gari-moshi kina muundo wa nchi za Mashariki. Unapotazama minara ya ukumbusho na sanaa za Toledo, utaona ufundi wa vizazi mbalimbali ambavyo vimekuwepo katika jiji hilo. Wakati jiji hilo lilipokuwa na mafanikio makubwa miaka 700 hivi iliyopita, watu wa jamii mbalimbali walihamia huko.

Utamaduni Mbalimbali

Kabla ya Waroma kufika Hispania, tayari Waselti na Waiberia walikuwa wamejenga mji katika eneo hilo linalofaa. Waroma waliliita jiji hilo Toletum (kutokana na neno tollitum linalomaanisha “kuinuliwa juu”) na kulifanya mojawapo ya majiji makuu ya mkoa. Mwanahistoria Mroma Livy alifafanua Toledo kuwa “jiji dogo, ambalo liliimarika kwa sababu ya mahali lilipokuwa.” Wavisigothi waliposhinda Hispania baada ya Milki ya Roma kuanguka, walifanya Toledo kuwa jiji lao kuu. Ni katika jiji hilo ambapo Mfalme Reccared alishutumu mafundisho ya Arius katika karne ya sita, na hilo liliwezesha Hispania kuwa kituo cha Ukatoliki wa asili na makao ya askofu mkuu wa kwanza yalikuwa Toledo.

Hali ya kidini ilibadilika wakati Toledo ilipoanza kuwa sehemu ya milki ya khalifa. Barabara nyembamba za jiji hilo la kale zilitengenezwa katika kipindi hicho kuanzia karne ya 8 mpaka ya 11. Kwa sababu Waislamu walikubali dini nyingine ziwepo, utamaduni wa Wakristo, Wayahudi, na Wamoor ulisitawi huko Toledo. Mwishowe mwaka wa 1085, Mfalme Alfonso wa 6 (mfalme Mkatoliki) alishinda jiji hilo. Ingawa utawala ulibadilika, watu wa jamii mbalimbali waliendelea kuishi pamoja kwa karne kadhaa.

Minara mingi ya ukumbusho yenye kupendeza huko Toledo ni ya kipindi cha enzi za kati. Watawala Wakatoliki walifanya Toledo kuwa jiji lao kuu, Wayahudi walitengeneza vyombo vya sanaa na kufanya biashara, nao mafundi Waislamu walitumia ustadi wao kuchora ramani za ujenzi. Wasomi wa dini hizo tatu walifanya kazi pamoja katika Chuo cha Watafsiri. Katika karne ya 12 na 13, walitafsiri maandishi mengi ya kale katika Kilatini na Kihispania. Kwa sababu ya jitihada za watafsiri hao, watu wa Magharibi walifaidika kutokana na ujuzi mwingi wa kisayansi wa Waarabu.

Hata hivyo, uhuru wa kidini ulikoma katika karne ya 14 wakati ambapo maelfu ya Wayahudi waliuawa kikatili. Kufikia wakati ambapo Columbus alivumbua Amerika, Baraza la Kihispania la Kuwahukumu Wazushi lilikuwa limeanzisha mahakama huko Toledo na iliwabidi Wayahudi na Waislamu kuchagua ikiwa watabadili imani yao au wahamishwe.

Minara ya Ukumbusho

Leo sehemu ya katikati ya jiji la Toledo ina minara ya ukumbusho zaidi ya mia moja. Kwa sababu hiyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni lilitangaza Toledo kuwa Jiji Linalostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni. Majengo mawili yenye kupendeza yaliyojengwa katika enzi za kati ni madaraja yaliyo juu ya Mto Tagus. Daraja moja linawezesha watu wanaotoka mashariki wafike jijini na lile la pili linawawezesha watu wa magharibi wafike jijini. Na ni wageni wachache tu ambao hukosa kuona lango kubwa la Puerta Nueva de Bisagra lililo nje ya jiji la kale lililozingirwa kwa kuta.

Mtu akiwa mbali ataona minara miwili mirefu ya ukumbusho. Upande wa mashariki kuna ngome kubwa ya mraba inayoitwa Alcázar. Kwa karne nyingi imetumika kama makao ya gavana Waroma, makao ya wafalme Wavisigothi, ngome ya Waarabu, na makao ya wafalme Wahispania. Sasa Jumba la Ukumbusho la Jeshi na maktaba kubwa inapatikana huko. Lakini kwa kuwa Toledo hasa ni jiji la kidini, kuna kanisa kubwa la Kigothi katikati ya jiji hilo.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 17.

Kanisa hilo na makanisa mengine huko Toledo yana michoro iliyochorwa na msanii maarufu aliyeishi Toledo. Anaitwa El Greco, jina linalomaanisha “Mgiriki.” Jina lake kamili ni Doménikos Theotokópoulos. Katika eneo alilokuwa akiishi lililo katika eneo la kale la Wayahudi, sasa kuna jumba la maonyesho ya sanaa lenye picha zake kadhaa.

Huenda jiji la Toledo linapendeza zaidi mtu anapolitazama kutoka kwenye vilima vilivyo kusini mwa jiji hilo. Au labda uzuri wa Toledo unaonekana unapopita kwenye barabara zake nyembamba. Huenda mgeni akapotea kidogo, lakini atafurahia vijia vya kale vyenye kupendeza, majengo ya zamani, mabaraza ya ghorofani, na maduka yenye vitu vya kupendeza.

Muda si muda inambidi mtalii aondoke kwenye jiji la kale la Toledo. Mahali pazuri pa kutokea ni kwenye ukingo wa kusini wa Mto Tagus. Siku inapokaribia kwisha, jua linaanza kutua likiangaza jiji hilo ambalo minara yake ya ukumbusho huonyesha jinsi lilivyokuwa na ufanisi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

JAMII TATU ZA TOLEDO

Katika Enzi za Kati, Toledo liligawanywa katika maeneo matatu ambako Wakatoliki, Wayahudi, na Waislamu waliishi kulingana na sheria na desturi zao. Baadhi ya majengo yao ya kale ya ibada sasa yamekuwa maeneo yanayotembelewa na watalii.r

➤ Msikiti wa karne ya kumi ambao sasa unaitwa Cristo de la Luz, umejengwa kwa matofali kama ilivyo kawaida ya mafundi Waislamu. Msikiti huo uko katika eneo la Medina ambako Waislamu matajiri waliishi.

➤ Ingawa baadaye yaligeuzwa kuwa makanisa ya Kikatoliki, masinagogi mawili ya enzi za kati yanaonyesha kwamba kulikuwa na jamii kubwa ya Wayahudi huko Toledo. Wakati fulani mmoja kati ya wakaaji watatu wa jiji hilo, alikuwa Myahudi. Sinagogi la kale zaidi ni lile la Santa María la Blanca na kama msikiti ulioonyeshwa kwenye picha hapo juu, sehemu yake ya ndani ina nguzo nyingi zenye mapambo. Sinagogi kubwa zaidi la El Tránsito (kulia), sasa hivi ni jumba la makumbusho lenye vitu vya kale vya Wayahudi wa Ulaya.

➤ Ujenzi wa kanisa kubwa zaidi la Kigothi huko Hispania ulianza katika karne ya 13 na ukachukua miaka zaidi ya 200.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

MAPANGA YA KIPEKEE, NA KEKI TAMU

Kwa miaka zaidi ya elfu mbili, wafua vyuma wa jiji hilo wametengeneza mapanga, na jiji la Toledo linajulikana kwa chuma bora. Majeshi ya Hannibal na askari wa Roma walitumia mapanga hayo yaliyotengenezwa kando ya Mto Tagus. Karne kadhaa baadaye, mafundi Waislamu walirembesha mapanga na silaha zao za Toledo kwa michoro ya Damasko. Kushoto kuna mchoro wa upanga wa Toledo. (Ona makala “Kupamba Chuma kwa Dhahabu,” katika gazeti la Januari 22, 2005 (22/1/2005) la Amkeni!) Siku hizi maduka mengi yanayouza bidhaa kwa ajili ya watalii yana mapanga mengi ya aina tofauti-tofauti, na mavazi ya vita. Unaweza kuona mapanga hayo katika filamu au yakiwa yamenunuliwa na watalii, lakini hayatumiwi vitani.

Utamaduni mwingine wa Toledo ni kuoka keki za lozi ambao ulianza Waarabu waliposhinda jiji hilo. Tayari kulikuwa na mashamba makubwa ya milozi nchini Hispania Waislamu walipofika, lakini hakukuwa na sukari ambayo ni kiungo muhimu cha keki hizo. Katika muda wa miaka 50 baada ya ushindi wa Waislamu, watu walianza kupanda miwa kusini mwa Hispania. Kufikia karne ya 11 keki za lozi zilipendwa sana huko Toledo, na tangu wakati huo watu wanazipenda sana. Sasa keki hizo huuzwa katika maduka mengi huko Toledo nazo hutengenezwa katika maumbo madogo. Mtu hawezi kutembelea Toledo na akose kuonja keki hizo zinazodondosha mate.

[Hisani]

Agustín Sancho

[Picha katika ukurasa wa 16]

 

URENO

HISPANIA

Madrid

Toledo

[Picha katika ukurasa wa 18]

Daraja la San Martin