Vikaragosi Vinapotumiwa Kuigiza
Vikaragosi Vinapotumiwa Kuigiza
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRIA
‘NAAM, muziki ulikuwa mtamu, lakini mbinu ya kuchezesha vikaragosi ilistaajabisha hata zaidi. Vikaragosi hivyo vilitoa ishara zisizotarajiwa ambazo sijawahi kuona katika maonyesho mengine ya vikaragosi!’
Je, msemaji huyo anaelezea maonyesho ya vikaragosi ya watoto? La. Amini usiamini, hayo ni maneno ya mtu mzima aliyesisimka baada ya kutembelea opera (maonyesho). Maonyesho hayo yenye kuvutia yalifanyiwa wapi? Yalifanyiwa katika Jumba la Maonyesho ya Vikaragosi la Salzburg, Austria, jiji la mtungaji maarufu wa nyimbo anayeitwa Mozart.
Je, umewahi kusikia kuhusu vikaragosi vya mbao vyenye kimo cha kati ya nusu mita na mita moja vikiigiza kwenye maonyesho? Vikaragosi katika Jumba la Maonyesho ya Vikaragosi la Salzburg hufanya hivyo. Vinapoanza kucheza jukwaani, vikaragosi hivyo huwafurahisha watazamaji, na kuwaingiza katika ulimwengu mwingine, ulimwengu wa kuwaziwa wenye muziki wa kupendeza.
Mchanganyiko wa Mambo Halisi na ya Kuwaziwa
Muziki unapoanza na pazia linapofunguliwa kwa ajili ya onyesho la kwanza, watazamaji wanashangazwa na yale wanayoona.
Je, kweli hivyo ni vikaragosi vya mbao vinavyotembea jukwaani na kutoa ishara kana kwamba vinaimba? Na namna gani nyuzi nyembamba zinazoonekana waziwazi juu ya vichwa vyao? Huenda wageni wengine wakakatishwa tamaa na kusema, ‘Si nyuzi zote zinaonekana waziwazi!’ Isitoshe, hakuna mtu mahali ambapo wapiga muziki huketi. Wazo la kucheza muziki uliorekodiwa halipendezi hata kidogo. Mgeni anaweza kufikiri hivi kwa hasira, ‘Huu ni upuuzi!’ Lakini ngoja kidogo! Polepole, maoni ya watazamaji yanabadilika.Mara tu watazamaji wanapobadili maoni yao mabaya, vikaragosi hivyo vinaanza kuwavutia. Mchanganyiko wa ajabu wa mambo halisi na ya kuwaziwa unatukia. Kamba za hariri zinazoongoza vikaragosi hivyo hazikumbukwi tena. Watazamaji wanasisimuliwa na onyesho lenyewe na pia wazo lisilo la kawaida la vikaragosi kuigiza katika jumba dogo la opera. Muda si muda wazo hilo halionekani tena kuwa la upuuzi na watazamaji wanasahau kwamba wanatazama vikaragosi visivyo na uhai. Ndiyo, vikaragosi vina uwezo wa ajabu wa kuwatumbuiza hata watazamaji wenye maoni mabaya na kuwaingiza katika ulimwengu wa vikaragosi.
Jukwaani na Nyuma ya Jukwaa
Mambo yanayotendeka nyuma ya jukwaa yanapendeza kama tu yale yanayotendeka jukwaani. Waigizaji halisi ni wale wanaochezesha vikaragosi nyuma ya jukwaa, wakiwa kwenye daraja lililo juu ya jukwaa. Wale wanaochezesha vikaragosi wanapopinda mikono yao kana kwamba wanatumia lugha ya ishara, vikaragosi huimba, hulia, hupigana, na kuinama kwa heshima kama tu waimbaji halisi wanavyofanya baada ya onyesho.
Gazeti The New York Times lilisema hivi kuhusu kinachowafurahisha watu sana: “Nyuma ya jukwaa, wanadamu wanaweza kuigiza sehemu za watu wa umri wowote au jinsia yoyote; wanapaswa tu kuwa na sifa
moja: ustadi.” Na ustadi wanaotumia kuchezesha vikaragosi na kuvifanya vionekane hai unastaajabisha sana.Vikaragosi Vinapendeza Kuliko Sanamu
Jumba la Maonyesho la Vikaragosi la Salzburg limefanikiwa kwa zaidi ya miaka 90—tangu 1913, kampuni hiyo ilipofanya maonyesho ya wimbo mmoja wa Mozart kwa mara ya kwanza. Anton Aicher, aliyekuwa mchonga-vinyago, ndiye aliyeanzisha maonyesho hayo. Alipomaliza masomo huko Munich, alitengeneza vikaragosi vinavyotoa ishara kama mtu halisi. Aligundua kuwa kuchezesha vikaragosi kunafurahisha kuliko kuchonga sanamu.
Muda si muda washiriki wa familia ya Aicher walipendezwa na burudani hiyo. Familia yake ilisaidia kushona nguo za vikaragosi na kuimba na kurekodi sauti zinazotumiwa katika igizo. Walifanikiwa sana hivi kwamba baada ya muda walihitaji kuongeza maonyesho yao. Tangu 1927, walialikwa wakatumbuize katika nchi nyingine. Siku hizi, maonyesho hayo hufanywa kwa kawaida katika nchi nyingine, kama Japani na Marekani. Watu wa tamaduni zote hufurahia maonyesho ya vikaragosi.
Je, Unaweza Kufurahia Maonyesho Hayo?
Opera imefafanuliwa kuwa “mchezo wa kuigiza unaofanywa kupitia muziki unaoambatana na ala za muziki huku waimbaji wakiwa wamevaa mavazi maalumu.” (The Concise Oxford Dictionary of Music) Maneno ya nyimbo hutungwa kwa kutegemea hadithi, historia, masimulizi ya Biblia na dhana. Yanaweza kuzungumzia msiba, mahaba, au vichekesho. Maonyesho yanayofanywa katika jumba hilo la maonyesho huwa ya Kijerumani au Kiitaliano. Kwa hiyo, ni jambo la hekima kusoma kwanza muhtasari uliotafsiriwa ili ujue ikiwa utafurahia mchezo huo.
Mkristo ataamuaje ikiwa maonyesho fulani yanafaa? Je, atategemea umashuhuri wa waimbaji? Au je, ataamua kwa kutegemea sauti tamu ya muziki? Au atategemea hadithi inayoigizwa?
Kwa kweli kama vile burudani nyingine, njia bora ya Mkristo kujua ikiwa atasikiliza au kutazama maonyesho fulani ni kulinganisha muhtasari wake na yale ambayo mtume Paulo alisema: “Mwishowe, akina ndugu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, mambo yoyote yaliyo ya hangaiko zito, mambo yoyote yaliyo ya uadilifu, mambo yoyote yaliyo safi kiadili, mambo yoyote yaliyo ya kupendeka, mambo yoyote yanayosemwa vema, wema wa adili wowote ulioko na jambo lolote la kustahili sifa lililoko, endeleeni kuyafikiria mambo hayo.”—Wafilipi 4:8.
[Picha katika ukurasa wa 8]
AUSTRIA
VIENNA
Salzburg
[Picha katika ukurasa wa 8]
Vikaragosi ambavyo viko tayari kuigiza katika maonyesho mbalimbali
[Picha katika ukurasa wa 9]
Jumba la Maonyesho ya Vikaragosi la Salzburg
[Picha katika ukurasa wa 10]
Anton Aicher, mwanzilishi
[Hisani]
By courtesy of the Salzburg Marionette Theatre
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
All photos on pages 8 and 9: By courtesy of the Salzburg Marionette Theatre