Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hazina Ndogo za Niihau

Hazina Ndogo za Niihau

Hazina Ndogo za Niihau

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HAWAII

KILA masika, mawimbi ya tufani hupiga fuo za Niihau, “Kisiwa Kisichotembelewa Bila Idhini” cha Hawaii. Mawimbi hurusha makoa madogo ya konokono kuelekea ufuoni ambayo hutapakaa katika fuo kadhaa. Niihau—iliyo na ukubwa wa kilomita 180 tu za mraba—ndicho kisiwa kidogo zaidi kati ya visiwa saba vya Hawaii vilivyo na watu. Hivyo basi, inafaa kwamba hazina ndogo zaidi zinapatikana katika kisiwa hicho. Hazina hizo ni makoa mazuri ya Niihau.

Tofauti na kisiwa jirani cha Kauai, kilicho kilomita 27 kaskazini-mashariki, Niihau ni kisiwa tambarare chenye ukame. Lakini kwa nini kinaitwa Kisiwa Kisichotembelewa Bila Idhini? Niihau si mali ya umma, na wageni ambao hawajaalikwa hawaruhusiwi humo. Wakaaji wanaojitegemea wa kisiwa hicho hawana mfumo wa umeme, maji ya bomba, maduka, wala ofisi ya posta. Ili kudumisha utamaduni wao wa zamani, wenyeji 230 hivi wa Hawaii huwasiliana katika Kihawaii. Iwapo hawachungi kondoo au ng’ombe, wanatafuta “dhahabu” yao, yaani, makoa madogo ya konokono. *

Katika majira ya baridi, watu hutembea au kuendesha baiskeli kwenye barabara za vumbi kwenda kwenye fuo safi na ghuba ndogo zenye miamba, nao hukaa huko kwa muda mrefu wakitafuta makoa. Baada ya kukusanya makoa, wao huyaanika chini ya kivuli. Baadaye yatakaguliwa na kutenganishwa kulingana na ubora, kisha yatatumiwa kutengeneza shanga laini. Katika visiwa vilivyo na mimea mingi, shanga nyingi hutengenezwa kwa maua. Huko Niihau, makoa hutumiwa kama “maua.”

“Vito” Kutoka Baharini

Makoa yametumiwa kwa miaka mingi kutengeneza vito huko Hawaii. Mwishoni mwa karne ya 18, wavumbuzi walioabiri—kutia ndani Nahodha James Cook—walipata mapambo yaliyotengenezwa kwa makoa na wakarekodi jambo hilo katika vitabu vyao. Pia walirudi makwao wakiwa na mapambo kadhaa. Huenda baadhi ya mapambo hayo yalitoka Niihau. Kadiri wakati ulivyopita, shanga maridadi za Niihau zilianza kuvaliwa na wanawake mashuhuri wa Hawaii, kutia ndani wacheza-dansi na washiriki wa familia za kifalme. Katika karne ya 20, “vito” hivyo vya pekee vilianza kuuzwa katika masoko ya mbali kwa sababu ya maduka ya sanaa, utalii, na wanajeshi waliopitia Hawaii wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Leo shanga maridadi ambazo wakati mmoja ziliwarembesha watu mashuhuri wa Hawaii zinavaliwa na watu wengi wanaovutiwa nazo katika maeneo ya karibu na ya mbali.

Makoa mengi yanayotumiwa kutengeneza shanga za Niihau yanaitwa momi, laiki, na kahelelani katika Kihawaii. Tofauti za rangi na maumbo humpa mtengenezaji wa shanga—ambaye kwa kawaida ni mwanamke—kazi ngumu lakini yenye kufurahisha ya kuunganisha makoa hayo kwa makini akitumia uzi ili kutokeza shanga maridadi. Aina 20 hivi tofauti-tofauti za makoa yanayong’aa ya momi, yaliyo na umbo la yai hutumiwa. Makoa hayo ni ya rangi mbalimbali kuanzia nyeupe hadi kahawia. Yakiunganishwa katika muundo wa thamani ya juu sana unaoitwa Lei Pikake, makoa hayo yanayong’aa na madogo yenye urefu wa milimita 10 tu, hutokeza shanga zinazofanana sana na nyuzi nyeupe za yasmini.

Mara nyingi mabibi arusi huko Hawaii hupambwa kwa nyuzi nyingi za makoa ya laiki yanayong’aa ambayo yanafanana na punje za mchele. Makoa hayo ni ya rangi mbalimbali kuanzia nyeupe kabisa, rangi ya pembe ya ndovu hadi manjano, huku mengine yakiwa na milia ya kahawia. Makoa ya kahelelani, ambayo huenda yalipata jina kutokana na chifu fulani wa zamani wa Hawaii, yana urefu wa milimita 5. Makoa hayo laini yaliyo na umbo kama la kilemba ndiyo magumu zaidi kuunganisha, na shanga zinazotengenezwa kutokana nayo zinauzwa kwa bei ghali zaidi. Makoa hayo ni ya rangi mbalimbali kama vile zambarau au rangi zisizopatikana kwa urahisi kama vile pinki. Makoa hayo yanauzwa kwa bei inayozidi mara tatu bei ya makoa yenye rangi nyinginezo.

Kutengeneza Ushanga kwa Makoa ya Niihau

Mtengenezaji wa shanga akiamua muundo anaotaka, yeye hutoa mchanga wote kutoka katika makoa na kuyatoboa mashimo akitumia chombo chenye makali sana. Ingawa anafanya kazi kwa uangalifu na ustadi, koa 1 kati ya kila makoa 3 huvunjika. Hivyo, lazima awe na makoa mengi ya ziada ili afaulu kutengeneza ushanga mmoja, na hilo huenda likachukua miaka kadhaa! Ili kuunganisha ushanga, mtengenezaji anaweza kutumia uzi wa nailoni uliopakwa nta, au simiti inayokauka upesi. Tangu zamani, pande mbili za mwisho za ushanga hufungiliwa koa dogo lililo na umbo bapa, kisha koa moja au mawili yanaongezwa mahali miisho hiyo miwili inapounganishiwa.

Kuna njia nyingi sana za kuunganisha shanga kama tu kulivyo na aina nyingi za makoa. Muundo mmoja ni ule wa shanga za uzi mmoja zilizotengenezwa kwa makoa ya momi ambazo zinaweza kuwa na urefu wa sentimita 150 hadi 190. Pia kuna shanga za kamba zilizo na mamia ya makoa madogo ya kahelelani, na aina nyingine ni ile ya shada zilizofumwa kwa maumbo tata—mengine yakiwa na makoa na mbegu. Kuunda shanga ni kazi ngumu sana inayochukua muda mrefu, na inayoumiza macho. Lakini wasanii stadi na wenye subira wa Niihau hutengeneza shanga tata zenye umaridadi usio na kifani. Kila ushanga ni tofauti, na ni rahisi kuelewa kwa nini shanga hizi huuzwa kwa bei ghali kama tu mawe ya thamani. Baadhi ya shanga hizo huuzwa kwa maelfu ya dola.

Kwa kulinganishwa na visiwa vingine vya Hawaii, Niihau hakina mimea mingi wala watu wengi, nacho kimejitenga sana. Lakini jitihada za watengenezaji stadi wa shanga wa eneo hilo zimewawezesha watu kutoka mbali sana na Niihau wafurahie umaridadi wa hazina za “Kisiwa Kisichotembelewa Bila Idhini.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Makoa ya aina hiyo yanapatikana pia katika vile visiwa vingine vya Hawaii na kwingineko katika Pasifiki, lakini wingi na ubora wa makoa yanayopatikana katika sehemu mbalimbali unatofautiana.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Makoa yaliyokaushwa hukaguliwa, kutenganishwa kulingana na ubora, na hutumiwa kutengeneza shanga laini

[Hisani]

© Robert Holmes

[Picha katika ukurasa wa 25]

Makoa ya “momi”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

© drr.net