Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vyakula vya Thailand

Vyakula vya Thailand

Vyakula vya Thailand

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MALASIA

UNAPOTEMBEA katika barabara yenye watu wengi huko Bangkok, Thailand, huenda kwa ghafla ukasikia harufu tamu kutoka kandokando ya barabara hiyo. Huko wapishi hupika vyakula vitamu vya Thailand kandokando ya barabara. Pua yako inapojawa na harufu tamu na macho yako yanapovutiwa na rangi maridadi, huenda ukashawishiwa kuonja vyakula hivyo vitamu.

Vyakula vya Thailand vinavutia kwa sababu vimetayarishwa kwa kuchanganya miti-shamba, mizizi, majani, na mbegu zilizochaguliwa kwa makini. Hilo hutokeza harufu nzuri na mchanganyiko wenye ladha mbalimbali—tamu, chachu, chumvi-chumvi, chungu, na kali—ambazo hufanya iwe vigumu sana kupita bila kuonja vyakula hivyo. Thailand ilipataje kuwa na mapishi hayo yasiyo ya kawaida? Jibu linapatikana katika historia yake ya kale.

Mchanganyiko wa Ladha Kutoka Mataifa Mbalimbali

Thailand iko katika eneo linalopitiwa na watu wengi wanaosafiri kutoka upande mmoja wa Asia kwenda mwingine. Kwa karne nyingi Wachina, Walaotia, Wakambodia, Waindonesia, watu wa Ulaya, na watu wengine walipitia Thailand, na wengi wao waliamua kuishi huko. Watu hao walileta vyakula kutoka nchi za kwao, nazo ladha na harufu nzuri za vyakula hivyo mbalimbali zimebaki nchini humo.

Hapo zamani, wasafiri Wahindi waliwaonyesha watu wa Thailand jinsi ya kutumia bizari katika mapishi. Katika karne ya 16, Wareno walileta pilipili na huenda pia walileta nyanya. Leo, vikolezo vingi sana vinatumiwa kutayarisha vyakula vya Thailand, lakini vyakula vyao vingi vinatia ndani pilipili zenye rangi ya manjano, kijani, na nyekundu, na rojo ya bizari yenye rangi hizo. Mchanganyiko huo wa bizari na pilipili hufanya vyakula vya Thailand viwe na ladha tamu kama vyakula vya kutoka Mashariki.

Mapishi Mengi, Ladha Nyingi Zaidi

Mlo wa kawaida wa Thailand unatia ndani vyakula vingi tofauti-tofauti kama vile supu, saladi, vyakula vya kukaangwa vyenye bizari na mchuzi. Wali mweupe haukosekani mezani. Kisha kuna kitindamlo, kinachoweza kutia ndani peremende zilizotengenezwa kwa sukari na mayai. Nyama ya nazi na tui (maziwa ya nazi) pia yanatumiwa kutayarisha vyakula vitamu vya Thailand.

Siri ya chakula kizuri mahali popote pale ni kutumia vitu ambavyo havijahifadhiwa kwa muda mrefu, na huko Thailand vitu hivyo vinapatikana kwa urahisi. Masoko katika majiji na miji, huuza matunda na mboga zilizotoka tu kuchumwa, na pia vikolezo kama vile lemon grass, giligilani, kitunguu saumu, tangawizi, galangal, iliki, ukwaju, na bizari. Pia utapata samaki waliotoka tu kuvuliwa. Katika masoko kama hayo utapata pia pilipili na malimau mengi, ambavyo ni viungo muhimu sana katika kutayarisha vyakula vya Thailand.

Iwe unatembelea Thailand ama unataka tu kuonja chakula cha Thailand ukiwa kwenu, jaribu tom yam goong, supu ya ngisi iliyotiwa chachu na pilipili, ambayo inapendwa sana nchini Thailand. Unaweza pia kujaribu saladi iliyokolezwa ya papai, tambi kwa kuku au bata-choma, nyama ya nguruwe iliyosagwa, au samaki aliyetiwa marinadi. Ma ho, yaani, “farasi walio mwendoni,” ni mchanganyiko wa nyama ya nguruwe, kamba, na njugu zilizorundikwa juu ya mananasi yaliyotoka tu kuchumwa na kisha mchanganyiko huo hupambwa kwa pilipili na majani ya mgiligilani. Kisha malizia mlo wako na kitindamlo cha wali unaonata na tui na maembe.

Ni njia gani bora ya kula chakula cha Thailand? Kulingana na tamaduni za sehemu fulani za nchi hiyo, unapaswa kutumia vidole kuufinyanga wali unaonata uliotayarishwa kwa njia ya pekee na kutokeza vidonge vidogo, kisha tumbukiza vidonge hivyo kwenye mchuzi halafu uvirushe kinywani mwako. Unapokula tambi, huenda ukapendelea kutumia vijiti vya kulia. Lakini ikiwa vitakutatanisha, unaweza kutumia uma na kijiko.

Je, sasa unatamani kula vyakula vya Thailand? Mapochopocho ya nchi hiyo maridadi ya Asia huenda yakakufanya uonje vyakula vitamu vya nchi za Mashariki vyenye ladha mbalimbali ambazo hujawahi kuonja.

[Picha katika ukurasa wa 23]

1 Supu ya tom yam goong

2 Saladi ya tambi na nyama iliyosagwa ya nguruwe na ngisi

3 Saladi iliyokolezwa ya papai

4 Ma ho

5 Wali unaonata ulio na tui na maembe