Kilio cha Mtoto wa Sokwe
Kilio cha Mtoto wa Sokwe
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KAMERUN
Pitchou ni sokwe-jike aliyezaliwa katika msitu mmoja huko Afrika ya kati. Pitchou alipokuwa na umri wa mwaka mmoja hivi, wawindaji walimuua mama yake na sokwe wengine wote katika kikundi chao, kwa ajili ya nyama yao. Pitchou alikuwa mdogo sana hangeweza kuuawa kwa ajili ya nyama hivyo alihifadhiwa ili auzwe kama mnyama-kipenzi. Wakati huohuo, Pitchou alianza kuugua na kulia sana.
PITCHOU ni mmoja tu kati ya maelfu ya wanyama mayatima walio katika jamii ya nyani. Kuna mambo kadhaa ambayo yametokeza hali hii yenye kusikitisha. Jambo moja ni biashara ya magendo ya nyama ya wanyama-pori. Ili kutosheleza mahitaji ya mikahawa na watu mmoja-mmoja ya nyama hizo, wawindaji stadi huwinda usiku na mchana msituni. Wakati huohuo, wawindaji haramu wanawauzia wafanyabiashara wanaouza isivyo halali wanyama na nyama hiyo kwenye soko lililo nchini mwao na la kimataifa pia.
Jambo lingine linahusisha ukataji wa miti mingi kwa muda mfupi. Misitu inapoharibiwa, wanyama hupoteza makao, mahali pa kujificha, kula, na kuzalia. Isitoshe, ukataji wa miti na uwindaji unategemezana. Kwa njia gani? Kwanza barabara za kusafirisha miti inayokatwa huwapa wawindaji nafasi za kuingia katika msitu ambako wanyama waliochanganyikiwa na wasio na makao huwindwa kwa urahisi. Mambo mengine yanatia ndani kuongezeka kwa idadi ya watu, kukua kwa majiji, kuongezeka kwa uhitaji wa vyakula vyenye protini, na mbinu za hali ya juu za kuwinda, vilevile vita, na silaha zinazopatikana kwa wingi kutokana na vita. Kwa sababu hiyo, wanyama wa jamii ya nyani na wanyama wengine wanakabili hatari ya kutoweka, na hilo hutokeza misitu isiyo na wanyama. Lakini kuna matatizo mengine pia. Matatizo gani? Kwa mfano, wanaposambaza mbegu, wanyama huchangia kurutubisha udongo na kufanya kuwe na unamna-namna wa mimea msituni. Kwa hiyo, wanyama wanapotoweka huenda mimea ikatoweka pia.
Hata hivyo, bado wanyama-pori wanauawa. Katika sehemu za Afrika Magharibi kwa kipindi fulani cha miaka kumi tu, wanyama wa jamii ya nyani walipungua kwa asilimia 90. “Ikiwa uwindaji haramu utaendelea, hivi karibuni hakutakuwa na sokwe wowote porini,” wanasema wataalamu wa wanyama-pori nchini Kamerun. *
Kuwaokoa Mayatima
Ili kukabiliana na hali hiyo yenye kusikitisha, vikundi vya kuhifadhi wanyama-pori kama vile Kituo cha Wanyama-Pori cha Limbe kilicho chini ya Mlima Kamerun huko Afrika Magharibi, hutunza wanyama walio katika hatari ya kutoweka. Wanapotembelea kituo cha Limbe, wageni wanaweza kuona sokwe, sokwe-mtu, nyani wakubwa, na jamii nyingine 13 za nyani, na pia wanyama wengine. Katika miaka ya karibuni, kituo hicho kimewatunza wanyama karibu 200 hivi mayatima na wasio na makao kwa kuwapa mahali salama pa kuishi, chakula, na matibabu. Lengo lingine la kituo hicho ni kuwafundisha wageni wengi kutoka Kamerun, nchi jirani na sehemu nyingine za dunia jinsi wanavyoweza kuhifadhi
mazingira. Katika mwaka wa karibuni wageni zaidi ya 28,300 walitembelea kituo hicho.Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa kwa Pitchou. Watazamaji walisikitishwa na vilio vya sokwe huyo mdogo na wakamnunua kutoka kwa wawindaji na kumpeleka kwenye kituo hicho. Alipowasili huko, Pitchou alifanyiwa uchunguzi wenye kina katika hospitali ya wanyama ya kituo hicho. Mbali na mshtuko, Pitchou alikuwa pia na kohozi, upungufu wa maji mwilini, hakuwa amelishwa vizuri, alikuwa akiharisha, na alikuwa na vipele. Kwa sababu ya matatizo yake ya ngozi, alipewa jina Pitchou, linalomaanisha “madoadoa” katika lugha ya huko. Jambo la kupendeza ni kwamba Pitchou alipona bila kuhitaji upasuaji ambao kama ungehitajika ungefanywa katika kituo hicho.
Kama ilivyo kawaida kwa wanyama wanaoletwa kwenye kituo hicho, kwa siku 90 Pitchou hakuruhusiwa kuchangamana na wanyama wengine. Kisha alijiunga na sokwe wengine 11 katika eneo walilotengewa lililo na mazingira yanayofanana na
msitu. Wafanyakazi wa kituo hicho walifurahi sana kuona sokwe wenye umri mkubwa wakimkaribisha Pitchou. Hilo ni jambo la kawaida kwa sokwe, na hivyo Pitchou akawa mmoja wa kikundi hicho.Urafiki wa karibu kati ya wafanyakazi wa kituo hicho na wanyama hutokeza uhusiano wa karibu. Kuona utendaji unaoendelea huko huwasaidia wageni kuelewa jukumu ambalo wanadamu walipewa na Mungu alipowaamuru wenzi wa kwanza waitiishe dunia pamoja na wanyama waliomo.—Mwanzo 1:28.
Mayatima Hao Watapatwa na Nini?
Lengo kuu la kituo hicho ni kuwarudisha wanyama wake porini. Hata hivyo, hilo si jambo rahisi. Si rahisi kwa wanyama ambao wamezoea kutunzwa na wanadamu kujitunza. Pia kuna hatari ya kuwindwa kwa ajili ya chakula. Nchi kadhaa za Afrika zimekubali kuunganisha maeneo fulani ya mpakani ili kuwalinda wanyama na kuboresha usimamizi wa mbuga za kitaifa. Inatumainiwa kwamba mipango hiyo itawezesha mayatima kurudishwa porini na kuchangia kuhifadhiwa kwa wanyama wote kutia ndani wale wa jamii ya nyani katika eneo hilo.
Wakati huohuo, inaonekana kwamba mambo yanayozuia jitihada hizo, kama vile pupa, umaskini, kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watu, na ukataji wa miti, yataendelea kuathiri vibaya wanyama wa jamii ya nyani na wengine pia. Ikiwa hakutakuwa na ulinzi thabiti haraka, “huenda idadi ya jamii za wanyama-pori ikapungua haraka,” anasema Felix Lankester, msimamizi wa Kituo cha Wanyama-Pori cha Limbe. “Matokeo . . . yanaweza kuwa kutoweka kabisa kwa wanyama-pori tunaojaribu kuhifadhi.”
Hilo linasikitisha sana. Lakini inasikitisha hata zaidi kuona wanadamu wakiteseka kwa sababu ya magonjwa na kukosa chakula chenye lishe na pia kuona watoto, walio na tumbo kubwa na macho yanayotokwa na machozi kila wakati, wakifa kwa sababu ya kukosa chakula. Kwa wazi, kisa cha Pitchou kinaonyesha hali yenye kusikitisha ya ulimwengu kwa ujumla, hasa ukosefu wa usawa na haki.
Kwa kupendeza, Muumba anajali mambo yanayotendeka duniani. Hivi karibuni ataondoa visababishi vya ukatili, kuteseka, na kutoweka kwa wanyama na atahakikisha kwamba kuna upatano wenye kudumu kati ya viumbe wote.—Isaya 11:6-9.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Wataalamu wa afya wanaonya kwamba watu wanaoshika na kula nyama ya wanyama-pori wanaweza kuambukizwa magonjwa hatari kama vile kimeta na Ebola, na pia virusi vinavyofanana na UKIMWI.
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
Pitchou kabla na baada ya kupata afya nzuri
[Picha katika ukurasa wa 23]
“Guenon” mwenye masikio mekundu
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nyani mkubwa akimtunza mtoto wake
[Picha katika ukurasa wa 24]
Eneo la kuingia kwenye kituo cha Limbe
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kumtunza Bolo, sokwe yatima
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
All photos pages 22 and 23: Limbe Wildlife Centre, Cameroon
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Both photos: Limbe Wildlife Centre, Cameroon