Mahali Mto Unaporudi Nyuma
Mahali Mto Unaporudi Nyuma
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KAMBODIA
JE, UMEWAHI kuona mto ukirudi nyuma? Vipi msitu unaofunikwa na maji kwa nusu mwaka? Je, ulijua kwamba watu wanaishi katika nyumba zinazoelea ambazo lazima zihamishwe kwa sababu maji hupotea? Je, unasema kwamba “haiwezekani”? Ikiwa unasema hivyo, huenda ukabadili maoni yako baada ya kutembelea Kambodia katika majira ya mvua.
Kila siku, kuanzia katikati ya Mei (Mwezi wa 5) hadi Oktoba (Mwezi wa 10), mawingu hutanda asubuhi na mvua hunyesha alasiri. Maji hutiririka kwenye maeneo ambayo yalikuwa yamekauka na yenye vumbi nayo mito hufurika.
Kwa Nini Unarudi Nyuma?
Tafadhali tazama ramani iliyoambatanishwa. Ona mahali ambapo Mto Mekong unakutana na Mto Tonle Sap. Maji hayo huungana na kugawanyika kuwa sehemu inayojulikana kama Mto Mekong na Mto Bassac. Mito hiyo huendelea kutiririka kuelekea kusini katikati ya nchi ya Vietnam na kufanyiza Delta kubwa ya Mekong.
Mara tu msimu wa mvua unapoanza, sehemu ya chini ya delta hufurika. Maji yaliyofurika hujaza vijito vilivyokauka. Majira ya mvua yanapoendelea, maji ya Mto Tonle Sap hugeuza mkondo na kuanza kutiririka kuelekea kaskazini badala ya kufuata mkondo wake wa kawaida kuelekea kusini. Mto huo uliofurika, hurudi nyuma hadi kwenye Ziwa Tonle Sap.
Ziwa hilo liko kwenye eneo tambarare kilomita 100 hivi kutoka Phnom Penh, mji mkuu wa Kambodia. Katika majira ya kiangazi, eneo la ziwa hilo huwa na ukubwa wa kilomita 3,000 hivi za mraba. Hata hivyo, katika majira ya mvua, maji huongezeka mara nne au tano zaidi na hivyo kulifanya ziwa hilo kuwa sehemu kubwa zaidi yenye maji baridi Kusini-Mashariki ya Asia.
Maeneo ambayo yalikuwa mashamba ya mpunga, barabara, miti, na vijiji hufurika. Wavuvi ambao mashua zao zilikuwa zikielea juu ya maji yenye kina cha mita 1, sasa huelea juu ya miti yenye urefu wa mita 10 hivi! Mahali kwingine, mafuriko makubwa hivyo huonwa kuwa msiba. Lakini kwa wakaaji wa Kambodia hiyo ni baraka. Kwa nini?
Mafuriko Yanapokuwa Baraka
Mto Tonle Sap unaorudi nyuma huacha mchanga wenye rutuba kwenye eneo la Tonle Sap. Kwa kuongezea, idadi kubwa ya samaki huingia katika ziwa hilo kutoka kwenye Mto Mekong na kuzaana kwa wingi katika eneo hilo lenye rutuba. Kwa kweli, Ziwa Tonle Sap ni mojawapo ya vyanzo vikuu ulimwenguni vya samaki wa maji baridi. Baada ya majira ya mvua, maji hupungua haraka sana kutoka kwenye ziwa hilo hivi kwamba wavuvi hupata samaki waliokwama kwenye miti!
Mafuriko hayo ya kila mwaka hutokeza mfumo unaobadilika wa ikolojia. Miti na mimea mingine iliyo katika eneo linalofurika, huwa na mfumo tofauti wa ukuzi ikilinganishwa na mimea iliyo kwenye maeneo yasiyofurika. Kwa kawaida, miti ya kitropiki hukua polepole, huangusha majani katika majira ya kiangazi na kutokeza majani mapya katika majira ya mvua. Lakini miti ya eneo la Tonle Sap haiangushi majani hadi inapofunikwa na mafuriko. Na badala kukua haraka katika majira ya mvua, inakua polepole. Baada ya maji kupungua na majira ya kiangazi kuanza, matawi hutokeza maua na majani hukua haraka. Maji ya ziwa yanapoisha, ardhi hufunikwa na majani yanayooza ambayo yanarutubisha miti na mimea mingine katika majira ya kiangazi.
Nyumba Zilizoinuliwa na Nyumba Zinazoelea
Namna gani kuhusu watu? Watu fulani wanaoishi karibu na ziwa wanajenga nyumba zao ndogo zikiwa zimeinuliwa. Katika majira ya kiangazi, nyumba hizo zinakuwa mita 6 hivi juu
ya ardhi. Lakini wakati wa mafuriko, mashua za wavuvi na mabakuli makubwa ya chuma ambayo nyakati nyingine yanatumiwa kuwasafirisha watoto, yanatia nanga karibu na mlango.Wakaaji wengine wa maeneo ya ziwa hilo, hujenga nyumba zinazoelea. Familia inapokua, nyumba nyingine inayoelea huunganishwa na nyumba iliyopo. Inakadiriwa kwamba kuna vijiji 170 vinavyoelea kwenye ziwa hilo.
Wakati wa mchana, watu wazima na watoto hutega samaki wakitumia mitego na nyavu. Kadiri kiwango cha maji kinavyoongezeka au kupungua, nyumba au vijiji vinaweza kusonga kilomita kadhaa ili zibaki karibu na ufuo au maeneo yaliyo na samaki wengi.
Mashua ndefu hutumika kama maduka au masoko yanayoelea, yakitosheleza mahitaji ya kila siku ya wakaaji, au hata kutumika kama “mabasi” ya umma. Watoto wanaoenda shuleni wanasoma katika shule inayoelea. Kila kitu, iwe ni mimea au watu huishi kulingana na kiwango cha maji katika nchi ambayo mto hurudi nyuma.
[Ramani katika ukurasa wa 23]
Majira ya kiangazi
Majira ya mvua
KAMBODIA
Ziwa Tonle Sap
Mto Tonle Sap
Mto Mekong
PHNOM PENH
Mto Bassac
Delta ya Mekong
VIETNAM
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mvulana akiendesha mashua kwenye Mto Tonle Sap
[Picha katika ukurasa wa 23]
Picha za kijiji kilekile katika majira ya kiangazi na katika majira ya mvua
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Map: Based on NASA/Visible Earth imagery; village photos: FAO/Gordon Sharpless