Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tatizo la Maji—Linashughulikiwa Jinsi Gani?

Tatizo la Maji—Linashughulikiwa Jinsi Gani?

Tatizo la Maji—Linashughulikiwa Jinsi Gani?

Kila sehemu ulimwenguni inakabili tatizo la maji. Tatizo hilo linahatarisha afya ya mabilioni ya wakaaji wa dunia. Ni hatua zipi ambazo zimechukuliwa ili kuhakikisha kwamba maji yanatumika kulingana na kiwango kinachopatikana?

AFRIKA KUSINI: “Maskini wa Durban Wapata Maji Baada ya Miaka Mingi,” kinasema kichwa katika gazeti Science. Makala hiyo inaripoti kwamba maskini wanaoishi huko hawajapata maji ya kutosha kwa muda wa miaka mingi kwa sababu ya sera ya ubaguzi wa rangi iliyofuatwa na serikali zilizopita. Makala hiyo inasema kwamba mnamo 1994 “familia 250,000 katika eneo la Durban hazikuwa na maji safi au mfumo wa kuondoa maji-taka.”

Ili kurekebisha hali hiyo, injinia mmoja alianzisha mpango mnamo 1996 ambao ungesambaza lita 200 hivi za maji kila siku kwa kila familia. Matokeo yalikuwaje? “Kati ya wakaaji milioni 3.5 wa Durban, ni wakaaji 120,000 tu wasio na maji safi,” linaripoti gazeti Science. Sasa mtu hahitaji kwenda mbali ili kuteka maji, na hilo ni tofauti sana na wakati uliopita kwani watu wengi walihitaji kuteka maji umbali wa zaidi ya kilomita moja.

Gazeti Science linaeleza kwamba ili kutatua tatizo la mfumo wa kuondoa maji-taka, badala ya kutumia “vyoo vya zamani vya shimo” sasa wanatumia “vyoo vyenye mfumo wa kutenganisha mkojo na kinyesi katika mashimo mawili na hivyo kuruhusu kinyesi kikauke na kuoza haraka.” Kufikia mwanzoni mwa mwaka wa 2008, vyoo 60,000 hivi vya aina hiyo vilikuwa vimechimbwa, ingawa wakati huo ilikadiriwa kwamba miaka miwili ingepita kabla ya nyumba zote kupata choo kinachofaa.

Brazili: Katika jiji la Salvador, mamia ya watoto walikuwa wakipatwa na magonjwa ya kuharisha kwa sababu ya ukosefu wa vyoo na mfumo wa kuondoa maji-taka. * Ili kurekebisha hali hiyo, wasimamizi wa jiji waliweka mabomba ya kuondoa maji-taka yenye urefu wa kilomita 2,000 kwa ajili ya nyumba zaidi ya 300,000. Matokeo yalikuwa nini? Magonjwa ya kuharisha yalipungua kwa asilimia 22 katika jiji lote na kwa asilimia 43 katika maeneo yaliyoathiriwa sana na magonjwa hayo.

India: Katika sehemu fulani za dunia, kwa kawaida kunakuwa na maji mengi kupita kiasi katika majira fulani; lakini nyakati nyingine maji hayo hayahifadhiwi ili yatumiwe vizuri. Hata hivyo, mnamo 1985, kikundi cha wanawake Wahindi katika wilaya ya Dholera kwenye jimbo la kaskazini-magharibi la Gujarat, walibuni mbinu nzuri ya kuhifadhi maji. Walipanga kikundi ili kujenga kidimbwi cha kuhifadhi maji ambacho kilipokamilika kilitoshana na uwanja wa mpira. Kisha wakatandaza plastiki ngumu ili kuzuia maji yasivuje. Mradi wao ulifanikiwa. Kwa kweli, miezi mingi baada ya majira ya mvua ndefu yaliyofuata bado walikuwa na maji, ingawa walikuwa “wamewakaribisha majirani wao wanywe maji hayo.”

Chile: Nchi hii ya Amerika Kusini ina urefu wa kilomita 4,265 ikipakana na Pwani ya Pasifiki upande wa magharibi na Milima ya Andes upande wa mashariki. Serikali inadhibiti shughuli zote za maji na inaidhinisha ujenzi wa mabwawa na mifereji. Matokeo ni nini? Sasa asilimia 99 ya wakaaji wa jijini na asilimia 94 ya wakaaji wa vijijini nchini humo wanapata maji ya kutosha.

Suluhisho Halisi

Inaonekana kwamba kila nchi ina mbinu yake ya kukabiliana na tatizo la maji. Katika nchi fulani ambapo upepo wenye nguvu unavuma kwa kawaida, vinu vya upepo huinua maji hadi mahali yanapoweza kutekwa kwa urahisi na pia hutumiwa kutokeza umeme. Katika nchi tajiri zaidi, inaonekana kwamba kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari ni njia moja ya kusuluhisha tatizo hilo. Katika maeneo mengi, mabwawa makubwa huhifadhi maji ya mito na mvua, mbinu ambayo imefanikiwa kwa kiasi fulani ingawa maeneo ya kuhifadhia yaliyo katika sehemu kame hupoteza asilimia 10 hivi ya maji kupitia uvukizaji.

Mashahidi wa Yehova ambao ndio wachapishaji wa gazeti hili, wanaamini kwamba suluhisho halisi kwa tatizo la maji linaweza kupatikana tu kutoka kwa Mungu na si mwanadamu. Biblia inasema hivi: “Dunia na vyote vinavyoijaza ni vya Yehova [Mungu], nchi yenye kuzaa na wale wanaokaa ndani yake. Kwa maana yeye ameiweka imara juu ya bahari, naye huiweka imara juu ya mito.”—Zaburi 24:1, 2.

Mungu aliwapa wanadamu jukumu la kutunza sayari hii. (Mwanzo 1:28) Hata hivyo, wanadamu wameharibu mali za asili na matokeo mabaya yanathibitisha kwamba “mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.”—Yeremia 10:23.

Yehova atachukua hatua gani ili kurekebisha mazingira ya dunia? Biblia inatuhakikishia kwamba anakusudia ‘kufanya vitu vyote kuwa vipya.’ (Ufunuo 21:5) Hebu fikiria ulimwengu usio na umaskini, ukame, na upungufu wa maji. Fikiria ulimwengu usio na mafuriko yanayosababishwa na majira ya mvua ndefu, ambayo siku hizi huua maelfu ya watu kila mwaka. Wakati wa utawala wa Ufalme wake, Mungu atatimiza ahadi zake nyingi! Yehova mwenyewe amesema hivi: “Ndivyo litakavyokuwa neno langu linalotoka katika kinywa changu. Halitarudi kwangu bila matokeo, bali hakika litatenda yale ambayo yamenipendeza, na hakika litafanikiwa katika yale ambayo nimelituma.”—Isaya 55:11.

Je, ungependa kujifunza mengi kuhusu kusudi la Mungu la kurekebisha hali duniani kama linavyoelezwa katika Neno lake Biblia? Makala inayofuata itaeleza jinsi unavyoweza kufanya hivyo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kila mwaka ulimwenguni pote, watoto milioni 1.6 hivi wanakufa kwa sababu ya magonjwa ya kuharisha. Idadi hiyo ni kubwa kuliko ya wale wanaokufa kutokana na magonjwa ya UKIMWI, kifua kikuu, na malaria yakiunganishwa pamoja.

[Blabu katika ukurasa wa 5]

“Mahali hakuna maji, hakuna uhai. . . . Uhai wetu unategemea maji.”—Michael Parfit, mwandishi wa National Geographic

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Ili kutokeza tani moja ya nafaka, unahitaji tani 1,000 za maji

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Asilimia 70 ya matumizi ya maji ulimwenguni ni kunyunyizia mashamba.”—Plan B 2.0, cha Lester R. Brown

[Grafu/Picha katika ukurasa wa 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kuna kiasi gani cha maji baridi?

Maji yote

97.5% Maji ya chumvi

2.5% Maji baridi

Maji baridi

99% Maji haya baridi yako kwenye miamba ya barafu au chini ya ardhi

1% yanaweza kupatikana kwa urahisi na wanadamu karibu bilioni saba na mabilioni ya viumbe wengine

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kuweka mabomba kwa ajili ya maji safi huko Durban, Afrika Kusini

[Hisani]

Courtesy eThekwini Water and Sanitation Programme

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wanawake wakifanya kazi kwenye mradi wa kuhifadhi maji ya mvua huko Rajasthan, India, mnamo 2007

[Hisani]

© Robert Wallis/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wakaaji wakishiriki ujenzi wa mfumo mpya wa kusambaza maji kwa ajili ya kijiji chao karibu na Copán, huko Honduras

[Hisani]

© Sean Sprague/SpraguePhoto.com