Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watoto Wanene Kupita Kiasi—Suluhisho ni Nini?

Watoto Wanene Kupita Kiasi—Suluhisho ni Nini?

Watoto Wanene Kupita Kiasi—Suluhisho ni Nini?

KATIKA nchi nyingi tatizo la watoto kunenepa kupita kiasi limeenea sana. Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kwamba inakadiriwa kuwa ulimwenguni pote watoto milioni 22 walio na umri wa chini ya miaka mitano ni wanene kupita kiasi.

Uchunguzi wa kitaifa nchini Hispania ulionyesha kwamba mtoto 1 kati ya 3 ni mnene kupita kiasi. Katika muda wa miaka kumi (1985-1995), idadi ya watoto wanene kupita kiasi iliongezeka mara tatu nchini Australia. Katika miaka 30 iliyopita, idadi ya watoto wanene kupita kiasi walio kati ya umri wa miaka 6 na 11 imeongezeka zaidi ya mara tatu nchini Marekani.

Sasa pia watoto katika nchi zinazositawi wananenepa kupita kiasi. Kulingana na Kikundi cha Kimataifa Kinachopambana na Kunenepa Kupita Kiasi, katika maeneo fulani ya Afrika, watoto wengi zaidi wanakabili tatizo la kunenepa kupita kiasi kuliko wale ambao wana utapiamlo. Mnamo 2007, Mexico ilikuwa nchi ya pili ulimwenguni baada ya Marekani, kuwa na watoto wanene kupita kiasi. Inasemekana kwamba huko Mexico City peke yake, asilimia 70 ya watoto na vijana wanaobalehe ni wanene kupita kiasi. Daktari wa watoto Dakt. Francisco González anaonya kwamba huenda “hiki kikawa kizazi cha kwanza kufa kabla ya wazazi wao kwa sababu ya matatizo yanayosababishwa na kunenepa kupita kiasi.”

Ni matatizo gani hayo? Matatu kati ya matatizo hayo ni kisukari, kupanda kwa shinikizo la damu, na ugonjwa wa moyo. Hayo ni matatizo ya afya ambayo awali yalionwa kuwa yanawaathiri hasa watu wazima. Kulingana na Taasisi ya Tiba ya Marekani, asilimia 30 ya wavulana na asilimia 40 ya wasichana waliozaliwa nchini Marekani katika mwaka wa 2000 wanakabili hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya 2 unaosababishwa na kunenepa kupita kiasi.

Uchunguzi unaonyesha kwamba watoto wanakabili hatari kubwa. Kuongezeka kwa idadi ya watoto walionenepa kupita kiasi kunasababisha kuongezeka kwa visa vya kupanda kwa shinikizo la damu. “Iwapo kuongezeka kwa visa vya kupanda kwa shinikizo la damu havitapunguzwa, huenda tukakabili ongezeko kubwa la visa vya ugonjwa mpya wa moyo katika vijana na watu wazima,” anaonya Dakt. Rebecca Din-Dzietham wa Chuo cha Kitiba cha Morehouse huko Atlanta, Georgia.

Mambo Yanayochangia

Ni nini kinachosababisha kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaonenepa kupita kiasi ulimwenguni pote? Ingawa huenda wengine wamerithi tatizo hilo kutoka kwa wazazi wao, kuongezeka sana kwa visa vya kunenepa kupita kiasi katika miaka ya karibuni kunaonyesha kwamba chembe za urithi si kisababishi kikuu. Stephen O’Rahilly, profesa wa biokemia na tiba katika Chuo Kikuu cha Cambridge Uingereza, anasema: “Chembe za urithi haziwezi kueleza kwa nini kuna ongezeko la kunenepa kupita kiasi. Hatuwezi kubadili chembe zetu za urithi katika muda wa miaka 30.”

Ikizungumza kuhusu visababishi hivyo, Kliniki ya Mayo nchini Marekani ilisema: “Ingawa kuna visa fulani vya watoto kunenepa kupita kiasi vinavyotokana na chembe za urithi na homoni, visa vingi vya kunenepa kupita kiasi vinasababishwa na watoto kula sana na kufanya mazoezi machache sana.” Mifano miwili ifuatayo inaonyesha mabadiliko katika njia ambayo watu hula.

Kwanza, kwa kuwa wazazi wanaofanya kazi hawana muda wa kutosha wala nguvu za kutayarisha chakula, imekuwa kawaida kwa watoto kula vyakula vyepesi. Mikahawa inayouza vyakula vyepesi imeenea kila mahali ulimwenguni. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba karibu asilimia 33 ya watoto wote nchini Marekani walio na umri wa kati ya miaka 4 na 19 hula vyakula vyepesi kila siku. Kwa kawaida vyakula hivyo vina sukari na mafuta mengi na hupakuliwa kwa kiasi kikubwa.

Sababu ya pili, soda zinapendwa kuliko maziwa na maji. Kwa mfano, watu nchini Mexico wanatumia pesa nyingi sana kila mwaka kununua soda, kuliko vyakula kumi muhimu. Kulingana na kitabu Overcoming Childhood Obesity, kunywa soda moja tu ya mililita 600 kwa siku kunaweza kumfanya mtu aongeze kilo 11 hivi kwa mwaka!

Ukieleza kuhusu ukosefu wa kufanya mazoezi, uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Glasgow huko Scotland ulionyesha kwamba watoto wenye umri wa miaka mitatu hufanya “mazoezi mepesi na mazito” kwa dakika 20 tu kila siku. Akizungumza kuhusu uchunguzi huo, Dakt. James Hill, profesa wa matibabu ya watoto katika Chuo Kikuu cha Colorado, anasema: “Si watoto wa Uingereza peke yao ambao hawafanyi mazoezi, tatizo hilo linaonekana pia katika nchi nyingi ulimwenguni pote.”

Suluhisho Ni Nini?

Wataalamu wa masuala ya lishe hawapendekezi kwamba watoto wawekewe vizuizi vya kula kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri ukuzi na afya yao. Badala ya hivyo, Kliniki ya Mayo inasema: “Njia bora zaidi ya kuwazuia watoto wasinenepe kupita kiasi ni kuboresha lishe na muda ambao familia nzima inatumia kufanya mazoezi.”—Ona sanduku katika makala hii.

Mkiwa familia, azimieni kula vyakula vyenye afya na kufanya mazoezi. Mkifanya hivyo, watoto wenu watafuata mazoea hayo hata watakapokuwa watu wazima.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28]

WAZAZI WANAWEZA KUFANYA NINI?

1 Nunua na kuwapa familia yako matunda na mboga badala ya vyakula vyepesi.

2 Usiwape soda, vinywaji vingine vyenye sukari, na vitumbua kwa kiasi kikubwa. Badala yake, wape maji au maziwa yasiyo na mafuta mengi na vitumbua vyenye lishe.

3 Tumia mbinu za kupika chakula zisizohusisha kutia mafuta mengi, kama vile, kuoka na kuchemsha, badala ya kukaanga.

4 Usiwapakulie chakula kingi.

5 Usiwape watoto chakula kama thawabu au hongo.

6 Usiwaruhusu watoto wakose kiamsha-kinywa. Wakifanya hivyo watakula kupita kiasi baadaye.

7 Ketini mezani mnapokula. Kula unapotazama televisheni au kutumia kompyuta kunamfanya mtu asijue kiasi cha chakula anachokula au asijue kwamba ameshiba.

8 Watie moyo wafanye mazoezi ya kimwili kama vile, kuendesha baiskeli, kucheza mpira, au kuruka kamba.

9 Dhibiti wakati unaotumiwa kutazama televisheni, kutumia kompyuta, na kucheza michezo ya video.

10 Panga familia itembelee hifadhi za wanyama, ikaogelee, au ikacheze.

11 Wape watoto wako kazi zinazowahitaji watumie nguvu

12 Weka mfano mzuri kwa kula vyakula vyenye afya na kufanya mazoezi.

[Hisani]

Vyanzo: Taasisi za Kitaifa za Afya na Kliniki ya Mayo