Je, Ungependa Kusafiri kwa Riksho?
Je, Ungependa Kusafiri kwa Riksho?
UNAPOWASILI Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh, mara moja mgeni huona jambo tofauti. Katikati ya umati wa watu utaona riksho nyingi sana! Idadi kubwa ya riksho hizo husafiri kwenye barabara na vijia zikiwa zimebeba watu na mizigo.
Huko Dhaka, riksho ndiyo njia ya usafiri inayopendwa sana. Ingawa idadi ya riksho zilizoandikishwa ni 80,000 hivi, watu wengi wanahisi kwamba kuna riksho nyingi zaidi barabarani kila siku. Kwa kweli, Dhaka inatajwa kuwa mji mkuu wa riksho ulimwenguni!
Riksho za Zamani
Ingawa wakati wa utawala wa Mfalme Louis wa 14 wa Ufaransa (1638-1715) kulikuwa na viti vya kuvutwa, riksho ya kwanza iliyokokotwa na mwanadamu ilibuniwa na Jonathan Gable, mmishonari Mmarekani huko Japani miaka ya 1870. Inasemekana kwamba alibuni gari hilo kwa ajili ya mke wake dhaifu na lilikuwa gari la kwanza kuitwa katika Kijapani jinrikisha, linalomaanisha gari linalokokotwa na mwanadamu. Mwishowe jina hilo limekuja kuwa “riksho” katika Kiswahili. Baada ya muda, miundo mbalimbali ya riksho ilianza kutumiwa kotekote Asia kama njia ya usafiri isiyogharimu sana. Wakati Charles Taze Russell (kulia), ambaye aliongoza kwa bidii kazi ya Wanafunzi wa Biblia (kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo), alipotembelea Japani mwaka wa 1912, alitumia riksho kusafiri kotekote nchini humo pamoja na msafara wake.
Huko Dhaka, riksho za magurudumu matatu zilianza kutengenezwa mwishoni mwa miaka 1930. Tofauti na riksho ambazo zilikokotwa na mwanadamu kwa kutumia miti miwili iliyofungwa kwenye gari hilo, riksho hizo mpya zilifanana na baiskeli kubwa yenye magurudumu matatu. Mwendeshaji wa riksho aliendesha akiwa kwenye gurudumu la mbele. Hilo lilimwezesha kubeba abiria au mizigo kwa mwendo mrefu zaidi huku akiendesha kwa urahisi katikati ya barabara zenye msongamano wa magari.
Mapambo Yenye Kupendeza
Riksho za Dhaka zimejaa mapambo. Zoea hilo la kupamba riksho lilianzaje? Riksho zilipotokea kwa mara ya kwanza huko Dhaka, ilibidi zishindane na magari yaliyokokotwa na farasi yaliyoitwa tomtom ambayo yalibeba abiria na mizigo. Huenda wamiliki wa riksho walianza kupamba magari yao ili kuvutia wateja watumie njia hii mpya ya usafiri. Mwishowe michoro na matangazo ya biashara yaligeuzwa kuwa sanaa ya pekee.
Sanaa iliyo kwenye riksho ni yenye kuvutia sana. Kwa kweli, Syed Manzoorul Islam, mchambuzi wa sanaa huko Bangladesh alifafanua riksho za Dhaka kuwa “majumba yanayosonga ya maonyesho ya sanaa.” Sehemu yote ya nje ya riksho imepambwa kwa michoro na picha zenye rangi maridadi. Shada, zari, na shanga zenye kung’aa zinaning’inia kutoka kwenye paa lake.
Kila msanii ana mtindo wake na mambo anayopenda kuchora. Michoro fulani inaonekana kama mabango yenye mandhari kutoka sinema za zamani na za siku hizi za Kihindi na Kibangladeshi. Sanaa hizo zinaonyesha kumbukumbu za maisha ya vijijini na mandhari za mashambani na, nyakati nyingine, masuala ya kijamii na ya kisiasa. Wasanii wengi hupenda kuchora picha za wanyama, ndege, uwindaji, na mandhari za mashambani.
Katika miaka ya 1950 kulikuwa na wachoraji wachache wa riksho. Leo, kuna wasanii kati ya 200 na 300 wanaofanya kazi hiyo. Riksho hizo zinatengenezwa kwenye karakana za pekee kwa kutumia vifaa kutoka kwa vitu mbalimbali. Kwa mfano, akitumia kipande cha mabati kutoka kwenye mkebe wa mafuta ya kupikia au kitu kingine kilichotupwa, msanii anaweza kutumia rangi ngumu inayong’aa kuchora mandhari yenye kuvutia. Sanaa ya riksho ni utamaduni wa Bangladesh. Inatambuliwa na kuvutia kwa njia ya pekee.
Mwendeshaji wa Riksho
Kama unavyoweza kuwazia, mwendeshaji wa riksho ana maisha magumu. Wazia ukiendesha riksho siku nzima ukiwa umebeba watu wengi au mizigo. Wateja wanaweza kutia ndani wake, watoto wa shule, wafanyabiashara, au wanunuzi wakiwa na bidhaa zao. Mara nyingi, watu wawili, watatu, au zaidi wanatumia riksho moja. Riksho inaweza kutumiwa pia kumbebea mfanyabiashara magunia ya mchele, viazi, vitunguu, au vikolezo akaviuze sokoni. Nyakati nyingine huenda mteja akawa ameketi juu ya mizigo yake mingi. Kwa mpita-njia, huenda ikaonekana mwendeshaji wa riksho hawezi kuiendesha ikiwa na mizigo mizito hivyo. Lakini hata kuwe na joto kali au mvua nyingi namna gani, mwendeshaji wa riksho hufanya kazi kwa bidii bila kulalamika.
Waendeshaji wengi wamehamia jijini kutoka maeneo ya vijijini yenye umaskini ambako wameshindwa kujipatia riziki kwa kulima. Kwa kuwa hawapati kazi zenye mshahara mnono, wengi huacha familia zao vijijini na kuwa waendeshaji wa riksho. Wakitumia nguvu zao, wao hupata dola chache (za Marekani) kila siku.
Njia ya Pekee ya Usafiri
Riksho zinaendelea kutumiwa sana huko Dhaka kwa sababu eneo hilo ni tambarare na kuna vijia na vichochoro vingi ambavyo haviwezi kutumiwa na vyombo vingine vya usafiri. Watu wengi huona njia hiyo ya usafiri isiyochafua mazingira kuwa yenye manufaa na yenye kufurahisha.
Katika majiji mengi ya Asia, riksho ziko karibu kutoweka. Tamaa ya kupata vyombo vinavyoweza kuwasafirisha watu wengi na maisha ya kisasa imefanya riksho zisitumiwe sana. Hata hivyo, ingawa watu wengi wanaziona kuwa zimepitwa na wakati, kuna jitihada ya kudumisha riksho kwa kuboresha muundo wake.
Unaposafiri huko Dhaka, unaweza kuchagua kutumia usafiri wa umma wa aina yoyote kama vile basi, teksi, pikipiki, riksho zenye injini, au riksho maridadi zinazoendeshwa kwa pedali. Lakini hutawahi kusahau raha ya kusafiri kwa riksho kwenye barabara za Dhaka zilizosongamana!
[Picha katika ukurasa wa 23]