Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ “Kwa sasa Urusi ina tani bilioni mbili hivi za takataka zenye sumu katika eneo lake, na hakuna njia inayofaa ya kuziondoa.”—RIA NOVOSTI, URUSI.
▪ Kumekuwa na ongezeko la uharamia baharini katika karne ya 21. Kwa mfano, katika mwaka wa 2007, “kulikuwa na mashambulio na majaribio 263 ya uharamia.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.
Kunywa Kileo Unapokuwa na Mimba
Kila mwaka nchini Ujerumani, watoto 10,000 hivi wanazaliwa na kasoro zinazosababishwa na kileo, linaripoti gazeti Süddeutsche Zeitung. Watoto 4,000 hivi kati yao wamelemaa sana au kabisa. “Hakuna kiasi cha kileo kilicho salama mtu anapokuwa na mimba,” anaonya Sabine Bätzing, Kamishna wa Dawa za Kulevya. “Tunahitaji kusisitizia madaktari, wakunga, na wanawake wenye mimba kwamba hata [mwanamke mwenye mimba] akinywa kidogo mara kwa mara anaweza kumdhuru mtoto kiakili na kimwili au anaweza kuwa na tabia isiyofaa.”
Kutunza Mimea Kunanufaisha Afya
“Wachunguzi wanagundua kwamba kukuza chakula chako, hata kama utafanya hivyo kwa kiwango kidogo sana, ni afadhali kwa afya kuliko watu walivyofikiri,” linasema jarida Psychology Today. Utafiti ulionyesha kwamba “bakteria fulani zinazotokezwa udongoni,” zilipomezwa au kunuswa, zilifanya “mfumo wa kinga wa mwanadamu uchochewe sana kufanya kazi.” Hivyo, gazeti hilo linasema, “inaonekana kwamba kumeza sehemu fulani za udongo ni muhimu kwa afya ya mwanadamu kama tu kula matunda na mboga zinazotoka katika udongo huo.”
Rekodi ya Kuruka kwa Muda Mrefu Zaidi
Wanasayansi katika Shirika la Marekani la Uchunguzi wa Jiolojia (USGS) wameripoti kuhusu “safari ndefu zaidi ya ndege kuwahi kurekodiwa.” Wanasayansi walifuata ndege wanaoitwa bar-tailed godwit kwa kutumia satelaiti walipofunga safari yao ya kila mwaka juu ya Bahari ya Pasifiki. Ndege mmoja wa kike aliruka kwa siku nane bila kusimama, umbali wa kilomita 11,650 kutoka Alaska hadi New Zealand. Wakati alipofika alikuwa “ametumia nusu ya uzito wake wa gramu 700,” linasema gazeti The Week. Wakati wa safari yao ya kurudi, ndege hao wanaoitwa godwit husafiri kutoka New Zealand hadi China kisha wanarudi Alaska. Safari yote ni jumla ya kilomita 29,000. “Ikiwa kila mwaka wanasafiri umbali wa kilomita 29,000 kwa wastani,” linasema shirika la USGS, “basi godwit aliyekomaa anaweza kuwa ameruka kilomita 463,000 hivi maishani mwake.”
Kushika Wezi wa Dungusi
Mimea ya dungusi iliyo katika Mbuga ya Taifa ya Saguaro, huko Arizona, Marekani, inaibiwa. “Kila mtu anataka kuwa na dungusi katika bustani yake,” anasema Jim McGinnis, wa ofisi ya upelelezi wa pekee wa Idara ya Kilimo ya Arizona. Ni jambo la kawaida kuona gari jangwani likibeba dungusi. Wezi hupenda dungusi iliyo na urefu wa mita moja au mbili, kwa kuwa inaweza kuuzwa kwa dola elfu moja au zaidi. Ili kukabiliana na wizi, maofisa wanapanga kuingiza vidude fulani vya kompyuta ndani ya dungusi. Baadaye maofisa hao wanaweza kutumia vifaa vya kuchunguzia ili kujua ikiwa mimea ya dungusi inayouzwa iliibiwa katika mbuga ya taifa.