Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Uchunguzi uliofanyiwa watu 2,000 hivi nchini Ujerumani ulionyesha kwamba asilimia 40 hivi ya vijana kati ya umri wa miaka 14 na 19 waliona ni sawa kuvunja uhusiano wa kimapenzi kupitia ujumbe mfupi au barua-pepe. Zaidi ya asilimia 80 ya watu walio na umri wa miaka 50 na zaidi waliona kwamba jambo hilo halifai kabisa.—FRANKFURTER NEUE PRESSE, UJERUMANI.
▪ Inakadiriwa kwamba mnamo 2008, watu walituma ujumbe mfupi trilioni 2.3 kupitia simu.—HITU NEWS, TAHITI.
▪ “Kuvuta sigara kunafupisha uhai wa mtu kwa miaka mingapi? Kwa wastani wa miaka mitano hadi kumi.”—UC BERKELEY WELLNESS LETTER, MAREKANI.
▪ Inakadiriwa kwamba asilimia 60 hivi ya kompyuta zinazotumiwa ofisini nchini Marekani hazizimwi usiku. Kwa sababu hiyo, kila mwaka tani milioni 14.4 hivi za gesi ya kaboni dioksidi hutolewa kutoka kwenye mitambo ya kutokeza umeme.—WORLD WATCH, MAREKANI.
Mabasi Yanawachochea Watu Wasimwamini Mungu
“Huenda hakuna Mungu. Acha kuhangaika na ufurahie maisha.” Maneno hayo yameandikwa kwenye mabasi 200 huko London, Uingereza; kwenye mabasi mengine 600 katika nchi yote; na kwenye mabango mawili makubwa kwenye Barabara ya Oxford huko London, linaripoti gazeti The Guardian. Waliotunga matangazo hayo wanasema kwamba kampeni yao ni ya kukabiliana na matangazo ya kidini yanayosema kwamba watu wasioamini wataishia kwenye moto wa mateso. Neno “huenda” linatumiwa ili kutii sheria za Shirika la Viwango vya Matangazo la Uingereza, kwa kuwa haiwezekani kuthibitisha kwamba hakuna Mungu. Jambo moja ambalo kampeni hiyo inakusudia kutimiza ni kuwatia moyo watu wengi ambao hawaamini kwamba kuna Mungu wajitokeze na kueleza maoni yao.
Hatari za Kupangia Kujifungua Mapema
Nchini Marekani, watoto wengi wanazaliwa mapema kupitia kuharakisha uchungu wa kujifungua au kupitia upasuaji kwa sababu zisizo za kitiba. Hata hivyo, “majuma ya mwisho ya uja-uzito ni muhimu kuliko ilivyofikiriwa hapo awali,” linasema jarida The Wall Street Journal. Uchunguzi uliofanyiwa watoto 15,000 hivi waliotoka tu kuzaliwa ulionyesha kwamba kwa kila juma ambalo mtoto alibaki tumboni kuanzia juma la 32 hadi juma la 39, uwezekano wa mtoto kupatwa na kifafa, homa ya nyongo manjano, matatizo ya kupumua, na kuvuja damu kwenye ubongo ulipungua kwa asilimia 23. Watoto waliozaliwa baada ya majuma 32 hadi 36 walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na matatizo ya kitabia na ya kiakili. Kwa sababu hiyo, Chuo cha Wataalamu wa Ukunga na Magonjwa ya Akina Mama cha Marekani kinapendekeza kwamba watoto wasizaliwe “kabla ya majuma 39 isipokuwa kuwe na sababu nzuri za kitiba za kufanya hivyo,” linasema jarida hilo.
Kupanda Ngazi Kunaboresha Afya
“Kupanda ngazi kwa ukawaida ni njia rahisi ya kuboresha afya,” linasema jarida la kitiba la Uingereza The Lancet. Watafiti waliwaomba wafanyakazi 69 ambao kazi zao hazihitaji nguvu nyingi, wapande ngazi badala ya kutumia lifti. Baada ya majuma 12, kiwango cha oksijeni walichotumia kiliongezeka kwa asilimia 8.6 na hilo lilipunguza “hatari kwa afya yao kwa asilimia 15.” Pia, wafanyakazi hao waliona mabadiliko makubwa katika “shinikizo la damu, mafuta ya mwili, na upana wa kiuno chao.”