Manyoya ya Bundi
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Manyoya ya Bundi
▪Mainjinia wa vyombo vya angani wanammezea mate bundi arukaye usiku. Kwa nini? Kwa sababu mabawa yake hayapigi kelele anaporuka. Habari fulani katika Tovuti ya National Geographic inasema, “Hakuna ndege mwingine anayeruka kimyakimya hivyo.” Ni nini kinachomfanya bundi aruke hivyo?
Fikiria hili: Ndege wengi wanaporuka wao hutokeza kelele wakati upepo unapopita juu ya manyoya yao. Lakini manyoya ya bundi hayafanyi hivyo. Manyoya yake ya nyuma yana miisho ya pekee ambayo hutawanya mawimbi ya sauti yanayotokezwa upepo unapopita juu ya bawa anapopiga mabawa yake chini. Manyoya mengine kwenye mwili wa bundi husaidia kufyonza kelele nyingine yoyote inayotokea.
Mainjinia wa vyombo vya angani wangependa sana kujifunza mengi kuhusu uwezo huo wa kuruka bila kelele ili hatimaye watengeneze ndege zenye uwezo huo. Kuwa na ndege za aina hiyo kutasaidia viwanja vya ndege vilivyo na sheria kali kuhusu kelele nyingi, viruhusu ndege kuruka na kutua usiku sana na mapema asubuhi. Mipango fulani ya kuboresha ndege kwa njia hiyo tayari inafanywa. Geoffrey Lilley, profesa aliyestaafu wa vyombo vya angani wa Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza anasema, “tumeanza sasa kujaribu kuboresha ndege kwa njia hiyo.” Anaongeza kwamba huenda ikachukua miongo kadhaa kabla ya ndege inayoruka kimyakimya kutengenezwa.
Una maoni gani? Je, manyoya ya bundi yenye uwezo wa kupunguza kelele yalijitokeza yenyewe tu? Au je, yalibuniwa?
[Picha katika ukurasa wa 23]
Linganisha unyoya wa bundi upande wa kushoto na wa mwewe kulia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Long-eared owl: © Joe McDonald/Visuals Unlimited; barn owl sequence: © Andy Harmer/Photo Researchers, Inc.; feather comparison: Courtesy of Eike Wulfmeyer/Wikimedia/GFDL