Jinsi Mfadhaiko Unavyotuathiri
Jinsi Mfadhaiko Unavyotuathiri
Ni nini hutukia unapokimbia ili usiachwe na basi au treni? Bila shaka, unahisi jinsi shinikizo la damu mwilini hupanda na kufanya moyo wako upige kwa kasi zaidi. Hata ukiachwa na basi hilo, moyo wako utaacha kupiga kwa kasi na utapumua kwa njia ya kawaida.
HATA hivyo, mambo yanaweza kuwa tofauti unaposhughulika na hali yenye kufadhaisha inayoendelea kwa muda mrefu. Inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kabla ya wasiwasi, kukazika kwa misuli, kupanda kwa shinikizo la damu, na mfumo wako wa umeng’enyaji kurudia hali ya kawaida. Watu wanazidi kutambua kwamba si rahisi kuacha kuwa na wasiwasi. Kwa mfano, wengi huhisi kana kwamba wao ni wafungwa katika kazi ambayo haiwaletei faida yoyote. Mfadhaiko unaathiri mwili na afya yako kwa njia gani?
Jinsi Mwili Wako Unavyotenda Unapofadhaika
Dakt. Arien van der Merwe, mtaalamu anayeshughulikia mfadhaiko, anaeleza jinsi ambavyo mwili wako hutenda unapofadhaika. Mara moja mwili unaanza kutenda na “kemikali nyingi za mfumo wa neva na homoni huenea mwilini na kutayarisha viungo na mifumo yote iwe tayari kukabiliana na mfadhaiko unaokuja.”
Uko tayari kuchukua hatua upesi. Hisi zako zote zinatendeshwa, iwe ni ile ya kuona, kusikia, au kugusa. Ubongo wako hutenda kwa kasi na tezi zako za adrenali hutoa homoni zenye nguvu, na kutendesha misuli yako kutia ndani moyo, mapafu, na viungo vingine ili viweze kukabiliana na hali yoyote yenye kufadhaisha.
Kwa hiyo, hali ya dharura inapotokea uhai wako unaweza kuokolewa kwa sababu ya jinsi mwili wako unavyotenda unapofadhaika, kama vile kukufanya uruke kando na kuhepa gari linalokaribia. Hata hivyo, hali huwa tofauti kabisa mfadhaiko unapoendelea.
Mfadhaiko Unapokuwa Wenye Kudhuru
Namna gani ikiwa kila wakati mwili wako unatendeshwa kwa kasi hivyo? Misuli yako itaendelea kukazika, moyo wako utaendelea kupiga kwa kasi, shinikizo la damu litaendelea kuwa juu, na damu itaendelea kuwa na viwango vya juu vya kolesteroli, mafuta, sukari, homoni, na kemikali nyingine. Kemikali kama hizo—ambazo zimekusudiwa kutokea kwa wakati mfupi tu kunapokuwa na mkazo—zinaweza kuharibu viungo muhimu vya mwili iwapo
zitaendelea kutokezwa kwa wingi. Kukiwa na madhara gani?Unaweza kuanza kupatwa na maumivu ya mgongo, kichwa, mshtuko wa ghafula wa misuli ya shingo, na kukazika kwa misuli. Madaktari wanasema kwamba mara nyingi dalili kama hizo zinahusiana na mfadhaiko wa kuendelea. Mfadhaiko kama huo unaweza kumfanya mtu asiwe na matokeo kazini, na hata unaweza kumfanya asiwe mchangamfu na asiwe na uhusiano mzuri na wengine. Unaweza pia kumfanya awe na ugonjwa wa kuhara, kukazika
kwa misuli ya umio. Huenda mfadhaiko unaoendelea ukatokeza madhara makubwa hata zaidi. Magonjwa kama vile kiharusi, mshtuko wa moyo, figo kuacha kufanya kazi, matatizo ya kupumua, na kisukari yanaweza kusababishwa au kuzidishwa na mfadhaiko unaoendelea.Van der Merwe anaandika hivi: “Kwa sababu ya kutokezwa kwa homoni inayoitwa cortisol mtu anapokuwa na mfadhaiko wa muda mrefu, mafuta hujikusanya tumboni na mgongoni.” Matatizo ya ngozi kama vile ukurutu na kubambuka kwa ngozi yanasababishwa au kuzidishwa na mfadhaiko. Mfadhaiko mkali umehusianishwa pia na kushuka moyo, mtu kuwa mkali sana, na uchovu wa kupindukia. Kumbukumbu na pia uwezo wa kukaza fikira unaweza kuathiriwa sana na mfadhaiko unaoendelea. Mfumo wa kinga wa mtu aliye na mfadhaiko wa muda mrefu unaweza kuathiriwa sana hivi kwamba anaweza kupatwa kwa urahisi na mafua na hata kansa na magonjwa yanayotokea kwa sababu ya mfumo wake wa kinga kushambulia chembe fulani za mwili.
Kwa kuwa mfadhaiko ni tisho kubwa kwa afya yetu ya kiakili, kimwili, kihisia, na kiroho, tunahitaji kujua jinsi tunavyoweza kuudhibiti. Hata hivyo, hatutaki kuondoa kabisa uwezo wa mwili wetu wa kukabiliana na mfadhaiko. Kwa nini?
Tunaweza kulinganisha mfadhaiko na farasi aliye na msisimuko. Farasi huyo anapotubeba, tunaweza kufurahia safari na kusisimka. Hata hivyo, farasi huyo akienda mbio bila kudhibitiwa, anaweza kuhatarisha uhai wetu. Vivyo hivyo, kuwa na mkazo fulani mwilini mwetu kunaweza kufanya maisha yafurahishe na kusisimua, na kutuchochea tuwe wabunifu, tufanye kazi kwa bidii, tuwe wachangamfu, na wenye afya.
Hata hivyo, tunaweza kudhibiti mfadhaiko kwa njia gani ili tufurahie maisha? Habari inayofuata inazungumzia njia zinazofaa za kudhibiti mfadhaiko na jinsi ambavyo tunatenda tunapofadhaika.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
‘TUMEUMBWA KWA NJIA YA AJABU’ NA MUUMBA MWENYE UPENDO NA HEKIMA
Jinsi miili yetu inavyokabiliana na mfadhaiko si jambo tulilorithi kutoka kwa watu wa kale kama watu wengine wanavyodhania. Badala yake, mifumo tata ya mwili wetu imeundwa kwa ustadi na Muumba mwenye hekima. Kwa mfano, uwezo wa damu kuganda ambao huuwezesha mwili kujikinga dhidi ya maambukizo na kuponesha vidonda, na pia uwezo wa mwili kukabiliana na mfadhaiko ni uthibitisho wa kwamba miili yetu iliumbwa na Mbuni mwenye hekima na upendo.
Mifumo hiyo ya mwili inathibitisha kwamba ‘tumeumbwa kwa njia ya ajabu yenye kuogopesha.’ (Zaburi 139:13-16) Maandalizi ya kiroho na ya kimwili ambayo Mungu anatoa kwa upendo, na pia jinsi alivyowaumba wanadamu kwa njia ya ajabu ili wafurahie maisha, inatuhakikishia kwamba hakutakuwa na maumivu, maombolezo, au kifo katika Paradiso duniani.—Ufunuo 21:3-5.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MADHARA YA MFADHAIKO WA MUDA MREFU
Maumivu ya kichwa
Kusaga meno
Maumivu ya shingo
Ugonjwa wa moyo
Vidonda vya tumbo
Maumivu ya mgongo
Mshtuko wa ghafula wa misuli