Ugonjwa wa Mifupa Unaoshambulia Kimyakimya
Ugonjwa wa Mifupa Unaoshambulia Kimyakimya
Anna, mwenye umri wa miaka 19, aliyekuwa akipata nafuu kutokana na ugonjwa wa kujinyima chakula alianguka ghafula kwa sababu ya maumivu makali sana ya mgongo. Alivunjika mifupa miwili ya mgongo na hivyo kimo chake kikapungua kwa sentimita tano. Yote hayo yalisababishwa na ugonjwa wa mifupa (“osteoporosis”).
INASEMEKANA kwamba ugonjwa huo wa mifupa huathiri watu kimyakimya kwa kuwa mara nyingi hakuna dalili zinazoonyesha kuwa mifupa ina kasoro hadi inapodhoofika sana na mtu anaanguka ghafula na kuvunjika. Mara nyingi, mifupa inayovunjika ni ile ya nyonga, mbavu, mgongo, au mkono. Watu wengi huhusianisha ugonjwa huo wa mifupa na wanawake wazee walio dhaifu. Hata hivyo, kama vile kisa cha Anna kinavyoonyesha, ugonjwa huo wa mifupa unaweza kuwapata vijana pia.
Tisho Kubwa kwa Afya
Shirika la kimataifa linaloshughulikia ugonjwa huo wa mifupa linaripoti kwamba “katika Muungano wa Ulaya, mtu mmoja huvunjika mifupa kutokana na ugonjwa huo baada ya kila sekunde 30.” Nchini Marekani, watu milioni 10 wana ugonjwa huo wa mifupa, na wengine milioni 34 wanakabili hatari ya kupatwa na ugonjwa huo kwa sababu mifupa yao haina uzito wa kutosha. Zaidi ya hilo, Taasisi za Kitaifa za Afya za Marekani zinaripoti kwamba “mwanamke mmoja kati ya wawili, na mwanamume mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 50 na zaidi, watavunjika mifupa maishani mwao kutokana na ugonjwa wa mifupa.” Na hali itazidi kuwa mbaya hata zaidi.
Jarida la Shirika la Afya Ulimwenguni linaloitwa Bulletin of the World Health Organization linasema kwamba katika miaka 50 ijayo idadi ya
watu wanaovunjika mifupa ulimwenguni kote kutokana na ugonjwa huo, itaongezeka kufikia mara mbili ya ilivyo leo. Huenda maoni hayo yanategemea idadi ya wazee inayotarajiwa kuongezeka. Lakini bado madhara ya ugonjwa huo yanatisha. Unawalemaza watu wengi sana na hata kuua. Asilimia 25 hivi ya wagonjwa wenye umri wa miaka 50 au zaidi ambao wamevunjika nyonga, hufa kutokana na matatizo ya afya katika muda wa mwaka mmoja baada ya kuvunjika.Je, Umo Hatarini?
Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba watu wengi hurithi ugonjwa huo. Ikiwa wazazi wamewahi kuvunjika nyonga, kuna uwezekano mara mbili kwamba watoto wao pia watapatwa na tatizo hilohilo. Pia wale ambao walipata utapiamlo walipokuwa katika tumbo la uzazi na hivyo kuwa na mifupa isiyokuwa na uzito wa kutosha walipokuwa watoto, wanaweza kupatwa na ugonjwa huo. Umri pia unaweza kumfanya mtu apate ugonjwa huo. Kadiri mtu anavyozeeka ndivyo mifupa yake inavyozidi kuwa dhaifu. Matatizo fulani ya afya kama vile, ugonjwa wa Cushing, kisukari, na pia kutokezwa kwa homoni nyingi kupita kiasi kwenye dundumio, yanaweza kuchangia kutokea kwa ugonjwa huo wa mifupa.
Kukoma hedhi kwa wanawake husababisha upungufu wa estrojeni inayodumisha uzito wa mifupa. Hiyo ndiyo sababu wanawake wengi zaidi hupatwa na ugonjwa huo wa mifupa kuliko wanaume. Mwanamke anapofanyiwa upasuaji na kutolewa kifuko cha mayai anapatwa na upungufu wa estrojeni na hivyo kumfanya akome hedhi mapema.
Mtu anaweza kupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa huo wa mifupa kwa kubadili mazoea ya kula na mtindo wa maisha yake. Chakula kisichokuwa na kalisi na vitamini D ya kutosha kinaweza kufanya mifupa idhoofike. Pia kutumia chumvi nyingi kunaweza kuongeza hatari ya kupatwa na ugonjwa huo, kwa sababu chumvi hufanya mwili upoteze kalisi. Kutumia kileo kupita kiasi pia huchangia kudhoofika kwa mifupa kwani mara nyingi mtu huwa na mazoea mabaya ya kula.
Kama ilivyotajwa hapo mwanzoni, Anna alipatwa na ugonjwa huu wa mifupa kwa sababu ya
tatizo la kula. Tatizo hilo lilifanya awe na upungufu wa madini muhimu, apunguze uzito, na akose hedhi. Kwa sababu hiyo, mwili wake ukaacha kutokeza estrojeni na hivyo mifupa yake ikadhoofika.Jambo lingine linalochangia kutokea kwa ugonjwa huo ni kutofanya mazoezi ya kutosha. Uvutaji wa sigara pia unachangia sana kwa sababu unapunguza madini yaliyo kwenye mifupa. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, mtu 1 kati ya 8 hivi alivunjika nyonga kwa sababu ya kuvuta sigara. Lakini uchunguzi unaonyesha kwamba mtu anapoacha kuvuta sigara, mifupa yake inaacha kuzorota na uwezekano wa kuvunjika unapungua.
Kuzuia Ugonjwa wa Mifupa
Mtu anapaswa kuanza kuzuia ugonjwa wa mifupa tangu utotoni na anapobalehe. Wakati huo ndipo mifupa ya mwili wa mwanadamu hukaribia kufikia uzito kamili. Kalisi huhifadhiwa hasa ndani ya mifupa nayo ndiyo madini muhimu zaidi ili kufanyiza mifupa yenye nguvu. Kalisi hupatikana hasa katika maziwa na vitu vinavyotokana na maziwa kama vile maziwa-mgando na jibini; dagaa na pia samoni (wanapoliwa na mifupa yao); lozi; unga wa shayiri; mbegu za ufuta; tofu; na pia mboga za majani ya kijani kibichi.
Ili kalisi iweze kufyonzwa mwilini, vitamini D ni muhimu. Vitamini hiyo hufanyizwa ngozi inapopigwa na jua. Manuel Mirassou Ortega, daktari ambaye ni mwanachama wa Mexican Bone and Mineral Metabolism Association, alisema hivi: “Mtu anapopigwa na jua kwa muda wa dakika kumi kila siku anapunguza uwezekano wa ugonjwa wa mifupa kuongezeka, kwa kuwa visehemu 600 vya vitamini D huongezeka.” Vitamini hii pia inaweza kupatikana kwenye vyakula kama vile sehemu ya katikati ya yai, samaki wa baharini, na pia ini.
Ni muhimu sana pia kufanya mazoezi ili kuzuia ugonjwa huo wa mifupa. Mazoezi humsaidia mtoto na kijana anayebalehe kujenga mifupa yenye nguvu, na pia mtu anapozeeka yanasaidia mifupa yake idumishe uzito unaofaa. Mazoezi yanayopendekezwa zaidi ni yale yanayofanywa bila kukaza sana mifupa na viungo, kwa mfano kutembea, kupanda ngazi, na hata kucheza dansi. *
Unaweza kuzuia ugonjwa huu unaoanza kimyakimya. Kama vile tayari tumeona, unaweza kufanya hivyo kwa kula chakula kinachofaa na kuishi kwa njia itakayosaidia kudumisha uzito unaofaa wa mifupa na kuiimarisha. Ni kweli kwamba inaweza kuwa vigumu kwa watu wengi ambao wanaishi bila kufanya mazoezi kubadilika. Lakini wale wanaoishi maisha yenye utendaji wanapata faida kubwa kama nini! Jambo la maana ni kwamba wanaweza kuepuka kuwa kati ya mamilioni ulimwenguni pote walio na ugonjwa wa mifupa.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 16 Kufanya mazoezi kupita kiasi hivi kwamba wanawake wanakosa hedhi kunaweza kudhoofisha mifupa kwa kukosa estrojeni. Inapendekezwa kwamba wanawake walio na umri unaozidi miaka 65 wapimwe uzito wa mifupa yao ili ionekane mifupa imedhoofika kwa kiasi gani. Ikiwa imedhoofika sana, kuna dawa zinazoweza kuzuia na kutibu ugonjwa huu wa mifupa. Hata hivyo, mtu anapaswa kufikiria hatari na faida kabla ya kuanza matibabu hayo.
[Blabu katika ukurasa wa 21]
Mtu anaweza kuzuia ugonjwa huo kwa kula chakula kinachofaa na kuishi kwa njia itakayosaidia kuimarisha mifupa na kudumisha uzito unaofaa
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]
Ugonjwa huo hufanya mifupa kuwa myepesi na dhaifu, na inaweza kuvunjika kwa urahisi. Mtu anaweza kupimwa aonekane kama ana ugonjwa huo kwa kutumia mbinu inayopima uzito wa madini ya mfupa.
[Picha]
Mfupa wenye afya
Mfupa wenye ugonjwa
[Hisani]
© BSIP/Photo Researchers, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Mazoezi yanayofaa yanaweza kumsaidia mtu ahifadhi uzito wa mifupa
[Picha katika ukurasa wa 20]
Lozi na vitu vinavyotokana na maziwa vina kalisi nyingi