Farasi wa Shetland Mtulivu Lakini Mwenye Nguvu
Farasi wa Shetland Mtulivu Lakini Mwenye Nguvu
● Ikiwa umewahi kutembelea maonyesho ya kilimo huko Ulaya huenda umeona au kupanda farasi wa Shetland. Jina lao linaonyesha wazi kwamba awali farasi hao walitoka katika Visiwa vya Shetland vilivyoko kaskazini-mashariki ya Scotland. Kwa kweli, wachimbuaji wa vitu vya kale wamechimbua mifupa ya farasi wadogo wanaokadiriwa kuwa waliishi maelfu ya miaka iliyopita.
Farasi wa Shetland wanaweza kutambuliwa kwa urahisi kwa miguu yao mifupi, manyoya marefu ya shingo na mkia, na manyoya mengi katika sehemu nyingine za mwili, ambayo humlinda dhidi ya hali mbaya ya hewa katika Visiwa vya Shetland. Kwa kawaida farasi hao huwa na kimo cha sentimita 70 hadi 107, nao huwa na rangi nyeusi au ya kahawia. Kimo cha sentimita 107 ndicho kimo cha juu zaidi kurekodiwa, ingawa inasemekana kuwa wale wa Amerika wana urefu usiozidi sentimita 117.
Ingawa si warefu sana, farasi hao wa Shetland wana nguvu sana. Kwa kulinganisha na ukubwa wao, farasi hao ndio wenye nguvu zaidi kati ya farasi wote. Kwa sababu hiyo, farasi hao walitumiwa kuvuta mimea iliyooza kutoka majini, kulima, na kufanya kazi katika migodi ya makaa ya mawe, ambako ni wanyama wadogo tu wangeweza kupita katika vijia vya chini ya ardhi. Kwa kweli, wengi wao waliishi maisha yao yote katika migodi hiyo bila kuona nuru kamwe.
Wanapozoezwa vizuri, farasi hao wa Shetland ni watulivu sana na hivyo wanaweza kutumiwa na watoto. Kwa sababu ya utulivu wao, walitumiwa katika programu za kuwasaidia walemavu kufanya mazoezi.
Kwa sababu ya sifa zao nzuri na uwezo wao wa kubadilikana na mazingira tofauti-tofauti, farasi wa Shetland wamesafirishwa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Vilevile vikundi vya wapenda-farasi na orodha za ukoo wa wanyama zimeanzishwa kwa ajili ya farasi hao. Lakini jina la farasi huyo bado linamhusianisha na kisiwa cha awali alikotoka, ambako farasi hao wa Shetland wana afya nzuri na hawajazalishwa na wengine.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kwa kulinganisha na ukubwa wao, farasi hao ndio wenye nguvu zaidi kati ya farasi wote
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
© S Sailer/A Sailer/age fotostock