Nyumba Zinazoweza Kuhamishwa za Asia ya Kati
Nyumba Zinazoweza Kuhamishwa za Asia ya Kati
JE, UMEWAHI kuona nyumba za duara ambazo huwa na joto wakati wa baridi lakini zinakuwa na baridi wakati wa joto kali? Nyumba kama hizo za watu wanaohamahama wa Asia ya Kati zinaitwa yurt! Kutoka nyika ya Mongolia na Kazakhstan hadi kwenye milima na mabonde ya Kyrgyzstan, nyumba hizo za kitamaduni zilionekana kila mahali wakati fulani uliopita.
Yurt ni aina ya hema lenye umbo la duara lililorembeshwa kwa mikeka ya matete kwenye kuta zake. Upande wa nje, umefunikwa kwa vitambaa vizito sana vilivyotengenezwa kutokana na manyoya ya kondoo. Nyumba hizo ni nyepesi na rahisi kutengeneza, lakini ni thabiti na zinastarehesha iwe ni wakati wa kiangazi au wakati wa baridi kali. Wakirghiz huita yurt nyumba ya kijivu; Wakazakh, nyumba ya kitambaa kizito cha manyoya ya kondoo; na Wamongolia, huiita ger, kumaanisha “makazi.”
Ikitegemea rangi ya manyoya ya kondoo, yurt zinaweza kuwa na rangi ya kijivu-kahawia au nyeupe nyangavu. Mara nyingi, yurt za Wakirghiz na Wakazakh hurembeshwa kwa vitambaa vilivyotiwa rangi nyangavu vyenye michoro ya pembe ya kondoo-dume. Zamani blanketi maridadi na mikeka iliyotengenezwa kwa kitambaa kizito cha manyoya ya kondoo ilifanya familia ionekane kuwa tajiri na yenye kuheshimika.
Sehemu muhimu sana ya yurt ni gurudumu la kati ambapo nguzo zote za paa huunganishwa. Gurudumu hilo zito na lililo thabiti, hutegemeza nyumba yote. Kitambaa kingine kizito kilichotengenezwa kwa manyoya ya kondoo hutumiwa kufunika gurudumu hilo wakati wa baridi kali na kinaweza kuondolewa ili kuingiza hewa wakati wa joto. Wakati wa usiku usio na mawingu, familia inaweza kuondoa kitambaa hicho na kutazama nyota angani kupitia shimo hilo kwenye paa.
Zinafaa Sana kwa Maisha ya Kuhamahama
Katika sehemu fulani za mashambani za Kazakhstan, Kyrgyzstan, na Mongolia, bado watu wanaishi maisha ya kuhamahama. Akieleza jinsi ngamia hutumiwa kuhamisha yurt huko Mongolia, Becky Kemery katika kitabu chake Yurts—Living in the Round, anasema hivi: “Nguzo hupakiwa kwenye ngamia mmoja. Gurudumu la paa hupakiwa mwisho, na hutoshea vizuri juu ya nundu ya ngamia. Halafu vitambaa vizito hupakiwa kwenye ngamia wa pili. Sehemu ambazo hakuna ngamia, wafugaji hutumia yak au farasi kuvuta yurt kwenye mikokoteni, au wanaweza kuzisafirisha wakitumia lori zinazotoka Urusi.”
Yurt za Mongolia huwa na nguzo zilizonyooka na paa tambarare kuliko zile za maeneo mengine. Paa hizo husaidia nyumba hizo kustahimili pepo kali na radi zinapopiga kwenye nchi tambarare.
Zile za Kyrgyzstan na Kazakhstan huwa zimeinuka zaidi na zina umbo la mviringo. Kwa kawaida, mlango wa yurt huangalia upande ambao jua huchomoza, ili kuruhusu mwangaza upenye ndani. Ndani kuna masanduku ya mbao ambayo huhifadhi vitambaa vizito pamoja na blanketi zenye rangi nyangavu zilizokunjwa. Kulingana na desturi, mgeni mheshimiwa au mwanamume wa familia hiyo mwenye umri mkubwa zaidi ndiye anayepaswa kuketi mbele ya sanduku hilo.Wanawake wanapaswa kuketi upande wa kulia wa nyumba hizo. Vyombo vyote vya kupikia, kuoshea, kushonea, na kutengeneza vitambaa huwekwa upande huo. Wanaume hukaa upande ule mwingine. Matandiko ya farasi, mijeledi ya kuongoza farasi, na vifaa vingine vya kuwinda na kuchunga wanyama hupatikana upande huo.
Bado Yurt Zinatumika Licha ya Mabadiliko ya Kisiasa
Baada ya Mapinduzi ya Kikomunisti yaliyotokea mwaka wa 1917, maisha ya kuhamahama yalibadilika sana. Warusi walijenga shule, hospitali, na barabara katika maeneo ya Asia ya Kati, na hivyo wenyeji hao wangeweza kukaa mahali pamoja.
Baada ya muda, wenyeji wengi waliyaacha maisha yao ya kuhamahama na wakaanza kuishi mijini na vijijini. Hata hivyo, bado yurt hutumiwa na wachungaji wakati wa miezi ya kiangazi wanapowachunga kondoo, ng’ombe, na farasi katika mashamba makubwa ya mifugo.
Maksat, mwanamume Mkirghiz aliye na umri wa zaidi ya miaka 35 anasema hivi: “Nilipokuwa kijana, nilimsaidia baba yangu kuchunga wanyama. Katika mwezi wa Julai (Mwezi wa 7) baada ya barafu kuyeyuka, tulipeleka wanyama wetu hadi sehemu za juu za milimani ili kuwalisha.
“Tulipofika huko tulisimamisha yurt yetu kando ya kijito ili tupate maji kwa ajili ya kupika na kuosha. Tuliishi hapo hadi mwanzoni mwa Oktoba (Mwezi wa 10) wakati hali ya hewa ilipobadilika na kuwa baridi.” Kwa hiyo, yurt bado inatumika hadi sasa.
Yurt ya Kisasa
Ni kawaida kuona yurt kando ya barabara katika maeneo ya Kyrgyzstan. Zinatumika kama maduka au mikahawa, ambapo wageni wanaweza kufurahia chakula cha wenyeji. Pia, wageni wanaweza kuona jinsi maisha ya Wakirghiz yalivyokuwa kwa kulala ndani ya yurt katika milima ya Kyrgyzstan au kando ya Ziwa Issyk Kul lililo safi sana.
Yurt pia hutumika katika sherehe fulani za kitamaduni za mazishi katika Asia ya Kati. Maksat anaeleza hivi, “Nchini Kyrgyzstan mtu aliyekufa huwekwa ndani ya yurt, ambapo familia na marafiki huja na kuomboleza kifo cha mpendwa wao.”
Katika miaka ya hivi majuzi nchi za Magharibi pia zimeanza kutumia yurt. Watu fulani wamepigia debe utumizi wa yurt kwa kuwa si ghali, zinajengwa kwa vifaa vinavyopatikana kwa urahisi, na pia haziharibu mazingira. Hata hivyo, yurt nyingi za kisasa zimejengwa kwa njia tofauti na zile za zamani. Zinajengwa kwa vifaa vya hali ya juu ili zidumu kwa muda mrefu zaidi.
Ingawa hatuwezi kujua chanzo cha yurt kwa usahihi, hatuwezi kupinga kwamba ni nyumba yenye thamani. Bado yurt ni sehemu yenye thamani ya maisha ya kuhamahama ya watu wa Asia ya Kati na ni uthibitisho ulio wazi wa ubunifu wa watu wanaoweza kubadilikana na wenye bidii.
[Picha katika ukurasa wa 17]
“Yurt” zilizojengwa kando ya Ziwa Issyk Kul nchini Kyrgyzstan