Ulimi wa Ndege Mvumaji
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Ulimi wa Ndege Mvumaji
● Watafiti huchunguza vipimo vidogo sana vya damu, DNA, na umajimaji mwingine kwenye kipande cha glasi kilicho na ukubwa wa mkono wa binadamu. Ingawa wao hutumia vifyonzaji au pampu kusogeza matone hayo madogo sana, hawajaweza kufaulu kikamili kwa kutumia mbinu hizo. Je, kuna njia bora zaidi ya kusafirisha kiasi kidogo hivyo cha umajimaji? Dakt. John Bush wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts alisema kwamba “tayari vitu vya asili vinajua jinsi ya kushughulikia tatizo hilo.”
Fikiria hili: Ndege mvumaji hapotezi nguvu kwa kunyonya nekta kutoka kwa ua hadi kwenye mdomo wake. Maji yaliyo mahali tambarare hutenda kinyume cha nguvu za uvutano na kujigawanya katika matone kadhaa. Kwa hiyo, ulimi wa ndege mvumaji unapogusa nekta, umajimaji huo hufanya ulimi wa ndege huyo ujikunje na kuwa kama mrija mwembamba sana, na hivyo nekta inajiingiza yenyewe mdomoni. Kwa ufupi, ndege mvumaji hatumii nguvu zozote kuingiza nekta hadi mdomoni. Ndege wavumaji wanaweza kujaza ndimi zao tena na tena hadi kufikia mara 20 kwa sekunde moja!
Uwezo huo wa “kukunja ulimi na kujivutia” nekta umeonekana pia katika vitwitwi, ambao hunywa maji kwa njia sawa na yule ndege mvumaji. Akizungumza kuhusu uwezo huo, Profesa Mark Denny wa Chuo Kikuu cha Stanford, California, Marekani, alisema hivi: “Inapendeza sana kuona jinsi ambavyo mdomo wa ndege huyo hutumia kanuni za fizikia na hesabu . . . Ikiwa ungemwomba injinia au mwanahisabati abuni njia ya kumwezesha ndege kuingiza maji mdomoni, hangefikiria kubuni njia kama hiyo.”
Una maoni gani? Je, ulimi mdogo sana wa ndege mvumaji—pamoja na uwezo wake wa kunyonya nekta haraka na kwa njia nzuri—ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
© Richard Mittleman/Gon2Foto/Alamy