Kitu Chenye Thamani Kuliko Kazi
Kitu Chenye Thamani Kuliko Kazi
Limesimuliwa na Murat Ibatullin
Katika mwaka wa 1987, Wizara ya Afya ya Urusi ilinituma Uganda, Afrika. Nilikuwa nimekubali kufanya kazi ya udaktari huko kwa miaka minne. Kwa kweli, sikuwa na nia ya kurudi Urusi, bali nilitaka kupata uzoefu ambao utanisaidia kufanya kazi katika nchi kama Australia, Kanada, au Marekani. Hata hivyo, kufikia mwaka wa 1991, mipango yangu ilibadilika, na nikarudi Urusi. Acha nieleze kwa nini nilifanya hivyo.
NILIZALIWA mwaka wa 1953 katika mji wa Kazan’, mji mkuu wa Jamhuri ya Tatarstan, Urusi ya Kati. Wazazi wangu ni Watatar, na watu wengi wa kabila hilo ni Waislamu. Nilipokuwa mtoto, nakumbuka nikiwaona babu na nyanya yangu wakipiga magoti na kusali kwa Allah. Watoto wao, kutia ndani wazazi wangu, walituambia tusiwasumbue na tuondoke chumba hicho. Wazazi wangu waliabikia jambo hilo kwa sababu walikuwa Wakomunisti na wakati huo waliamini kwamba hakuna Mungu.
Nilipokuwa na umri wa miaka minne, nilipooza wakati wa mlipuko wa mwisho wa polio katika Muungano wa Sovieti. Nakumbuka nikipelekwa mara kwa mara hospitalini na kulazwa mara kadhaa. Nakumbuka babu yangu akiniombea ili nipate nafuu. Nilitaka kuwa kama watoto wengine, kwa hiyo, licha ya kuwa na mguu mlemavu, nilicheza kandanda, mpira wa magongo, na michezo mingine.
Kadiri nilivyoendelea kukua, ndivyo nilivyotamani kuwa daktari. Sikuwa mtu wa kidini, na wakati uleule sikuamini kwamba hakuna Mungu. Ni kwamba tu sikuwahi kufikiria kumhusu Mungu. Kufikia wakati huo, nilichambua sera za Ukomunisti na mara kwa mara nilibishana na baba na mjomba wangu. Mjomba wangu alikuwa mwalimu wa falsafa katika chuo kimoja kikuu, naye baba yangu alifanya kazi na Shirika la Usalama wa Kitaifa la Sovieti, lililoitwa KGB. Nilipomaliza masomo katika chuo cha kitiba, nilijiwekea mradi wa kuwa daktari mpasuaji wa neva na kuhamia nchi nyingine.
Kutafuta Maisha Bora
Katika mwaka wa 1984, niliandika tasnifu kuhusu uchunguzi wa uvimbe kwenye ubongo. Kisha, mwaka wa 1987, nilitumwa Uganda katika hospitali mmoja huko Mulago. Nilihamia nchi hiyo maridadi nikiwa pamoja na mke wangu Dilbar, na watoto wetu, Rustem aliyekuwa na umri wa miaka saba na Alisa aliyekuwa na umri wa miaka minne wakati huo. Kazi ilikuwa ngumu katika hospitali hiyo na ilitia ndani kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliokuwa na virusi vya UKIMWI. Mara nyingi nilitembelea hospitali nyingine nchini humo kwa kuwa wakati huo kulikuwa na wapasuaji wawili tu wa mfumo wa neva nchini Uganda.
Siku moja, mimi na Dilbar tuliona Biblia ya Kirusi kwa mara ya kwanza katika duka la vitabu huko Uganda. Tulinunua nakala kadhaa ili tuwatumie marafiki wetu katika Muungano wa Sovieti, kwa kuwa katika nchi hiyo ilikuwa vigumu sana kununua Biblia wakati huo. Tulisoma sura kadhaa za Biblia, lakini tukaacha kwa sababu hatukuelewa chochote.
Ingawa hivyo, kwa miaka mitatu tulihudhuria makanisa mbalimbali huko Uganda na kujaribu kuelewa yale ambayo wenyeji huamini na ni nini hufanya maisha yao yawe na kusudi. Pia niliamua kuisoma Kurani katika lugha yake ya awali. Mimi na Rustem tulianza kujifunza Kiarabu. Baada ya miezi michache, tungeweza kuzungumza Kiarabu kwa ufasaha.
Katika kipindi hichohicho, tulikutana na Heinz na Marianne Wertholz, wamishonari ambao ni walimu wa Biblia kutoka Ujerumani na Austria. Tulipokutana mara ya kwanza, hatukuzungumzia dini hata kidogo. Tulikuwa tu kama wazungu wanaokutania Afrika kwa mara ya kwanza. Tuliwauliza wanafanya nini Uganda na wakatuambia kwamba wao ni wamishonari wa Mashahidi wa Yehova na walikuwa nchini humo ili kuwasaidia watu kujifunza Biblia.
Kisha nikakumbuka kwamba pindi moja wakati wa somo la falsafa katika chuo kikuu nilichohudhuria huko Urusi, tuliambiwa kwamba Mashahidi ni madhehebu na kwamba wao huwatoa watoto wao kuwa dhabihu na kunywa damu yao. Niliwaeleza Heinz na Marianne jambo hilo, kwa kuwa sikuamini kwamba wanaweza kufanya hivyo. Mimi na Dilbar tulikubali kitabu Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani, na tukasoma sehemu kubwa kwa muda wa saa chache. Nilimwuliza Dilbar jinsi alivyohisi kukihusu, naye akaniambia kwamba alifurahia sana mambo aliyokuwa akisoma na alikuwa amesisimuka sana! Nilimwambia kwamba nilihisi vivyo hivyo.
Baada ya kukisoma, tulikuwa na hamu ya kuzungumza tena na Heinz na Marianne. Tulipokutana nao, tulizungumzia habari nyingi. Yale tuliyojifunza kuhusu Biblia yalitugusa sana moyo. Tulichochewa kuwaambia marafiki na wafanyakazi wenzetu yale tuliyokuwa tukijifunza. Watu hao walitia ndani balozi wa Urusi, mabalozi wadogo wa Urusi na nchi nyingine, na mwakilishi wa Vatikani. Mwakilishi huyo wa Vatikani alitushangaza alipotuambia kwamba Agano la Kale ni “hadithi tu.”
Tunarudi Nyumbani
Mwezi moja kabla ya kurudi Urusi katika mwaka wa 1991, mimi na Dilbar tuliamua kuwa Mashahidi wa Yehova. Tulidhani kwamba tutakaporudi Kazan’, tutaanza kuhudhuria mikutano mara moja. Lakini kwa kusikitisha, kwa miezi mitatu hatukujua mahali ambapo Jumba la Ufalme lilikuwa wala hatukumwona Shahidi yeyote! Kwa hiyo, tuliamua kuhubiri nyumba kwa nyumba, kama Mashahidi wa Yehova wanavyofanya ulimwenguni pote, hata ingawa ilitubidi tufanye hivyo peke yetu. Tulianza kujifunza Biblia
na watu kadhaa, kutia ndani mwanamke mmoja ambaye baadaye alikuja kuwa Shahidi.Baada ya hayo, tulitembelewa na Shahidi mmoja mzee ambaye alikuwa amepewa anwani yetu na Mashahidi huko Uganda. Tulianza kukutana pamoja na kikundi cha watu 15 waliofanya mikutano katika nyumba ndogo. Heinz na Marianne waliendelea kuwasiliana nasi na hata walikuja kututembelea huko Kazan’. Baadaye tuliwatembelea huko Bulgaria, ambako walikuwa wamepewa mgawo na bado wanatumika huko wakiwa wamishonari.
Matokeo Mazuri Katika Nchi ya Nyumbani
Kila nilipopata nafasi, niliwaambia kweli za Biblia wafanyakazi wenzangu katika hospitali moja huko Urusi nilipokuwa nikifanya kazi. Wengi wao wameitikia na wakawa Mashahidi wa Yehova, kutia ndani madaktari wenzangu. Katika mwaka wa 1992, mwaka moja baada ya kurudi Urusi, kikundi cha Mashahidi huko Kazan’ kiliongezeka na kuwa na watu 45; na mwaka uliofuata, kikawa zaidi ya 100. Leo, katika mji wa Kazan’, kuna makutaniko saba ya Mashahidi—matano ya Kirusi, moja la Kitatar, na moja la lugha ya ishara. Pia kuna vikundi vya Kiarmenia na Kiingereza.
Katika mwaka wa 1993, nilihudhuria kongamano la kitiba huko New York City, ambako nilipata nafasi ya kutembelea makao makuu ya ulimwengu ya Mashahidi wa Yehova huko Brooklyn. Nilikutana na Lloyd Barry, ambaye alikuwa akisaidia kuratibu kazi ya kuhubiri ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote. Licha ya kuwa na shughuli nyingi, alizungumza nami kwa muda fulani.
Tulizungumzia uhitaji wa kuwa na vichapo vya Biblia katika Kitatar. Miaka kadhaa baadaye, kulikuwa na kikundi cha watafsiri wa Kitatar huko Urusi, na vichapo katika Kitatar vikaanza kuchapishwa. Tulifurahi kama nini tulipoanza kupokea kwa ukawaida Mnara wa Mlinzi, gazeti ambalo limetayarishwa kwa ajili ya kujifunza Biblia! Muda mfupi baada ya hapo, kutaniko la kwanza la Kitatar lilianzishwa.
Kutumia Mbinu za Kuhifadhi Damu
Ninatii sheria zote za Mungu za maadili, ambazo zinatia ndani sheria inayopatikana kwenye Matendo 15:20 ambayo inawaamuru watumishi wa Mungu “wajiepushe . . . na damu.” Mstari wa 29 unaongezea kwamba watumishi wa Mungu wanapaswa “kuendelea kujiepusha na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu na damu na vitu vilivyonyongwa na uasherati.”
Kwa hiyo, Mashahidi wa Yehova wanapoenda hospitalini, wao huwaomba madaktari waheshimu maoni yao kuhusu matibabu yasiyohusisha damu. Kwa muda fulani, nilikuwa mshiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ya Mashahidi huko Kazan’. * Katika mwaka wa 1997, wakati Pavel, mwenye umri wa mwaka moja kutoka jiji la Novosibirsk alipohitaji upasuaji mara moja, mama yake aliwasiliana nasi ili kupata msaada. Wakati huo, nchini Urusi, kulikuwa na madaktari wachache tu wenye uzoefu ambao wangekubali kufanya upasuaji bila kutumia damu. Tulikubali kumsaidia kupata daktari ambaye angetumia matibabu ya badala.
Tulipata hospitali ya upasuaji wa moyo huko Kazan’ iliyokuwa na madaktari ambao walikubali kumfanyia Pavel upasuaji. Machi 31, 1997 (31/3/1997), walifaulu kumfanyia upasuaji wa kurekebisha tatizo baya la moyo linaloitwa tetralogy of Fallot bila kutumia damu. Mnamo Aprili 3 (3/4/1997), gazeti Vechernyaya Kazan, liliripoti hivi: “Kijana huyo mdogo yuko sawa na hahitaji tena kutumia dawa za moyo . . . Mama ya Pavlik [jina Pavel limenyambuliwa kuonyesha alikuwa mdogo] alitulia kwa mara ya kwanza katika muda wa miezi 11.” Baada ya muda
mfupi, Pavel alipata nafuu baada ya upasuaji na akaanza kutembea akiwa bado hospitalini.Pavel sasa ana afya nzuri na anaishi maisha ya kawaida. Anapenda kuogelea, kuteleza kwenye theluji, na kucheza kandanda. Yuko katika darasa la nane, na yeye pamoja na mama yake wanashirikiana na kutaniko moja la Mashahidi wa Yehova katika jiji la Novosibirsk. Baada ya kisa hicho, madaktari katika hospitali hiyo walifaulu kuwafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa kadhaa ambao ni Mashahidi wa Yehova bila kutumia damu. Huko Tatarstan, kumekuwa na maendeleo mengi katika mbinu za matibabu, na imekuwa kawaida kufanyiwa upasuaji bila kutumia damu.
Kazi Yangu Leo
Mimi, mke wangu, na Mashahidi wengine tunafanya kazi katika hospitali inayotoa matibabu ya hali ya juu kwa wagonjwa walio na matatizo ya moyo na mfumo wa neva. Sisi hufanya upasuaji wa aina mbalimbali hasa tukitumia mbinu za kuhifadhi damu. Ninafanya kazi ya kuchunguza mfumo wa neva kwa kutumia eksirei na ninaendeleza masomo yangu ya kutibu mfumo wa neva bila kumfanyia mgonjwa upasuaji kwa njia ya kawaida au kumtia damu. Nikiwa profesa katika Idara ya Magonjwa ya Mfumo wa Neva na Upasuaji wa Mfumo wa Neva katika Chuo Kikuu cha Kitiba cha Kazan’, mimi huwatolea hotuba wanafunzi wa tiba na madaktari na kuwasaidia kuona manufaa ya kutumia matibabu yasiyohusisha damu. *
Mke wangu hufanya kazi pamoja nami akiwa mtaalamu wa kupiga picha kwa kutumia mawimbi ya sauti. Sisi hufurahia sana kazi yetu kwa sababu tunaweza kuwasaidia watu. Lakini tunapata uradhi mwingi zaidi kwa kuona jinsi ambavyo kweli za Biblia huwasaidia watu kuwa na uhusiano na Mungu. Tunapata furaha moyoni tunapowaambia watu kuhusu ahadi ya Mungu kwamba hivi karibuni hapa duniani “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 23 Halmashauri za Uhusiano na Hospitali ni vikundi vya Mashahidi wa Yehova vinavyosaidia hospitali na wagonjwa kushirikiana suala la damu linapotokea.
^ fu. 27 Matibabu yasiyohusisha damu hutumiwa kama matibabu ya badala. Kwa kuwa kuna hatari nyingi zinazohusianishwa na kutiwa damu mishipani, matibabu na upasuaji usiohusisha kutiwa damu mishipani unazidi kupendwa na watu wengi ulimwenguni pote. Kutiwa damu mishipani kuna hatari ya kuambukizwa UKIMWI na maambukizo mengine na pia mwili kuathiriwa na damu hiyo.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Nikiwa daktari Afrika
[Picha katika ukurasa wa 13]
Mimi na mke wangu tulipoanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, 1990
[Picha katika ukurasa wa 14]
Nilipomtembelea Lloyd Barry wakati wa ziara yangu huko Brooklyn, New York, 1993
[Picha katika ukurasa wa 15]
Pavel na mama yake leo
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nikihubiri na mke wangu, Dilbar