Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Usalama Barabarani la Uarabuni, lililoko nchini Tunisia, lilionyesha kwamba kila mwaka aksidenti zaidi ya 500,000 za barabarani hutukia huko Uarabuni, na kutokeza zaidi ya vifo 36,000.—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, TUNISIA.

“Uchunguzi mmoja unaonyesha kwamba Intaneti ndicho chanzo muhimu zaidi cha habari kuhusu ngono kwa vijana Wachina, kwani elimu ya ngono inayotolewa shuleni na nyumbani haitoshi.”—CHINA DAILY, CHINA.

Kamera za Kompyuta Zinazopeleleza

Polisi nchini Ujerumani walimkamata mtu fulani hivi majuzi ambaye ameshtakiwa kwa kutumia kamera za kompyuta za wasichana wachanga kutazama ndani ya vyumba vyao. Inadaiwa kuwa mlaghai huyo wa kompyuta alifaulu kupata neno la siri la utambulisho la akaunti ya Intaneti ya msichana mmoja, na hivyo akaweza kupata anwani za watu kadhaa. Inasemekana kuwa kupitia akaunti hiyo, alitumia marafiki za msichana huyo programu fulani za kompyuta zilizoingiza virusi katika kompyuta zao ingawa zilizoonekana kuwa programu za kawaida tu—nazo zilimwezesha kuongoza kompyuta za wasichana hao kutoka mahali alipokuwa na kutumia kamera za kompyuta hizo wakati wowote ule. Inasemekana kuwa wachunguzi walipovamia nyumba yake, walipata picha milioni tatu na “alikuwa ameunganisha kompyuta yake kwenye kompyuta za wasichana 80 [kupitia Intaneti] bila wao kujua,” linasema gazeti Aachener Zeitung.

Lugha Mpya kwa Wanasayansi

Wataalamu wa lugha wanaochunguza lugha zinazozungumzwa na watu wachache sana za Kiaka na Kimiji ambazo zinazungumzwa katika jimbo la Arunachal Pradesh lililo kaskazini-mashariki mwa India, linalopakana na Bhutan na China, waligundua lugha nyingine tata ya kitamaduni, ijulikanayo kama Kikoro. Gregory Anderson, mkurugenzi wa Taasisi ya Lugha Zinazotumika Zinazokabili Hatari ya Kutoweka, anasema hivi: “Hii ni lugha ambayo haijawahi kutambuliwa wala kurekodiwa.” Lugha ya Kikoro haikuwa imetambuliwa kwa sababu inazungumzwa na watu 800 hivi katika eneo ambalo usafiri umepigwa marufuku. Katika mwaka wa 2009, lugha 24 ziligunduliwa katika eneo moja nchini China ambalo lilikuwa na lugha moja tu.

Nguruwe-Mwitu Wenye Sumu ya Nyuklia

“Malipo kutoka kwa serikali ili kugharimia hasara ambayo wawindaji wanapata kwa sababu ya kuwinda nguruwe-mwitu wenye sumu ya nyuklia, imeongezeka mara nne [nchini Ujerumani] tangu mwaka wa 2007,” linaripoti gazeti Spiegel Online. Wawindaji wengi huuzia watu nyama ya nguruwe-mwitu, lakini serikali ilitoa sheria zinazozuia uuzaji wa nyama yenye viwango vya juu vya cesium-137, ambayo ni madini yenye sumu ya nyuklia yaliyotokezwa na msiba wa Chernobyl miaka 25 iliyopita. Nguruwe-mwitu huathiriwa sana na uchafuzi huo kwa sababu wanapenda sana kula “uyoga na truffle, ambazo zina uwezo mkubwa wa kufyonza sumu ya nyuklia,” linaeleza gazeti Spiegel. “Sababu kuu ya kuongezeka kwa malipo hayo, si kuongezeka kwa athari za sumu ya nyuklia, bali ni kuongezeka kwa idadi ya nguruwe-mwitu nchini Ujerumani.” Wataalamu wanasema kwamba huenda tatizo hilo likaendelea kwa miaka 50.