Sanaa ya Kale ya Warusi ya Kupaka Mbao Rangi
Sanaa ya Kale ya Warusi ya Kupaka Mbao Rangi
● Watalii wengi wanaotembelea Urusi hupenda kununua vinyago vilivyochongwa kwa mikono, kama vile wanasesere wanaoitwa matryoshka. Zamani za kale vinyago vingi vilitengenezwa na mafundi stadi hasa kwa kutumia mbao. Sanaa ya kale ya kupaka mbao rangi inajulikana kama khokhloma.
Kwa karne nyingi, Warusi walitumia bakuli za kulia zilizochongwa kwa ustadi na kupakwa rangi, na pia walitumia vijiko, vikombe, na vyombo vingine vilivyotengenezwa kwa mbao. Kwa kawaida, walichora mimea na wanyama kwenye vyombo hivyo. Vijiji vizima vingetumia wakati wao mwingi kutengeneza vyombo fulani vya mbao.
Wanakijiji wangetengeneza vyombo hivyo wakati wa majira marefu ya baridi kali, wakati ambapo hakukuwa na kazi nyingi ya kufanya shambani. Miaka 200 au zaidi iliyopita, miji na vijiji fulani vilifaidika sana kutokana na vyombo hivyo vya mbao. Kwa mfano, wakati mmoja, wakazi wote wa mji wa Semënov waliacha kulima na wakatengeneza vyombo vya mbao karibu milioni mbili vilivyotia ndani mabakuli, masahani, vikombe, na vijiko katika kipindi cha mwaka mmoja tu.
Wakazi wa vijiji vilivyo karibu na mji wa Nizhniy Novgorod walivumbua mbinu mpya ya kufanya vyombo viwe na rangi ya dhahabu inayong’aa. Rangi na vanishi zisizoweza kuharibika kwa moto zilitokezwa, na baada ya vyombo kupakwa vitu hivyo, vilitiwa ndani ya tanuru. Kwa sababu ya moto huo mwingi, vyombo vyenye rangi ya fedha viligeuka na kuwa na rangi laini ya dhahabu. Mbinu hiyo bado inatumiwa leo katika viwanda vya khokhloma huko Nizhniy Novgorod.
Michoro hiyo ya Khokhloma hutia ndani maua na mimea inayopatikana katika misitu na maeneo ya malisho ya Urusi, pamoja na ndege na samaki wa maeneo hayo. Michoro yenye mchanganyiko wa nyasi, majani, pamoja na matunda kama vile beri za aina mbalimbali, hutumiwa sana. Kwa kawaida, michoro hiyo hupakwa rangi nyekundu, nyeusi, ya dhahabu, na kijani. Leo katika sehemu nyingi ulimwenguni, meza nyingi za kulia hurembeshwa kwa vyombo maridadi vya khokhloma vilivyo na michoro kutoka maeneo ya mashambani ya Urusi.