Kinywaji cha Mexico Kilichosambaa Ulimwenguni
Kinywaji cha Mexico Kilichosambaa Ulimwenguni
● Mashujaa Wahispania walipofika Mexico katika miaka ya mapema ya karne ya 16, walikunywa kinywaji cha eneo hilo kinachoitwa pulque, kilichotengenezwa kutokana na maji yaliyochacha ya mmea wa aina fulani ya mkonge-pori. Kinywaji cha pulque kina kiasi kidogo cha kileo, kama pombe. Pia, kina protini za mboga, wanga, vitamini, na madini, na kinatumiwa katika maeneo mengi kuongeza madini mwilini.
Kwa kuwa walizoea kunywa kileo pamoja na chakula chao, Wahispania walianza kutokeza kileo kikali zaidi kwa kutumia maji hayo ya mkonge-pori, ambacho walikiita mescal. Kileo hicho ndicho leo kinaitwa tequila. Siku hizi kuna viwanda vingi vinavyotokeza tequila nchini Mexico, na vinatokeza zaidi ya lita milioni 189 kwa mwaka, na asilimia 40 ya kinywaji hicho huuzwa nje ya nchi hiyo.
Mashamba ya mkonge-pori aina ya blue agave, yanapatikana katika nyanda kame za juu za magharibi ya kati ya Mexico, hasa katika jimbo la Jalisco karibu na mji wa Tequila. Kinywaji hicho kilipewa jina la mji huo. * Mkonge-pori hukomaa baada ya miaka 12 hivi, na muda huo wote unafyonza madini mengi sana. Mmea huo unapovunwa, majani yake yenye miiba hukatwa na kuacha sehemu ya ndani yenye umbo la nanasi inayoitwa piña. Kwa wastani, sehemu hiyo ina uzito wa kilogramu 50 na ina maji hayo yenye madini mengi. Kilogramu 7 hivi ya piña inaweza kutokeza lita 1 ya tequila.
Watu wengi nchini Mexico hufurahia kunywa tequila, wakiinywa pamoja na chumvi na kipande cha limau. Watu wa nchi nyingine wanafahamu zaidi margarita, mchanganyiko wa tequila, maji ya limau, na mvinyo wenye ladha ya machungwa, inayoandaliwa pamoja na barafu katika glasi iliyopakwa chumvi kidogo mdomoni. * Kwa kuwa nchi 90 hivi hununua tequila, inaweza kusemwa kwamba kileo hicho cha Mexico kimesambaa katika nchi nyingi ulimwenguni.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Kati ya aina 136 hivi za mkonge-pori nchini Mexico, aina kadhaa hutumiwa kutokeza pulque na vileo vingine. Lakini ni aina ya blue agave pekee ambayo hutumiwa kutokeza tequila.
^ fu. 5 Biblia haishutumu kutumia kileo kwa kiasi. (Zaburi 104:15; 1 Timotheo 5:23) Hata hivyo, Biblia inashutumu kunywa kileo kupita kiasi na ulevi.—1 Wakorintho 6:9, 10; Tito 2:3.