2. Dumisha Usafi
2. Dumisha Usafi
KAMA vile tu daktari mpasuaji anavyolinda wagonjwa anaotibu kwa kunawa mikono, kusafisha vifaa anavyotumia, na kuhakikisha kwamba chumba cha upasuaji ni safi, unaweza kuilinda familia yako kwa kudumisha usafi wa mwili wako, wa jikoni, na wa chakula chako.
● Nawa mikono.
Shirika la Afya ya Umma la Kanada linasema kwamba “mikono hueneza asilimia 80 hivi ya magonjwa ambayo huambukizwa kwa ukawaida kama vile mafua na homa.” Kwa hiyo, nawa mikono yako vizuri kwa sabuni na maji kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na unapotayarisha chakula.
● Dumisha usafi jikoni.
Uchunguzi mmoja unaonyesha kwamba ingawa eneo la chooni ndilo safi zaidi ndani ya nyumba, “sponji ama vitambaa vya jikoni ndivyo vitu vyenye bakteria nyingi zinazopatikana katika kinyesi.”
Kwa hiyo, badilisha vitambaa vya jikoni mara kwa mara na utumie maji moto yenye sabuni au yenye dawa za kuua viini kusafisha meza na kaunta za jikoni. Ni kweli kwamba si rahisi kufanya hivyo. Bola anaishi katika nyumba isiyo na maji ya bomba anasema, “Hilo linafanya hali iwe ngumu, lakini sikuzote sisi huhakikisha kwamba kuna sabuni na maji ya kutosha kusafisha eneo la jikoni na nyumba yote.”
● Safisha mboga na matunda.
Huenda vyakula vilichafuliwa na maji machafu, wanyama, kinyesi, au vyakula vingine vibichi kabla ya kuuzwa. Kwa hiyo, hata kama utaondoa maganda ya matunda au mboga, yasafishe kabisa ili kuondoa bakteria hatari. Kufanya hivyo kunachukua muda. Mama mmoja nchini Brazili anayeitwa Daiane anasema hivi, “Ninapotayarisha saladi, huwa siharakishi ili nihakikishe nimeyasafisha majani yote vizuri.”
● Usiweke nyama mbichi pamoja.
Ili kuzuia kuenea kwa bakteria pakia vizuri nyama mbichi ya ng’ombe, kuku, na samaki, na uiweke mbali na vyakula vingine. Tumia ubao tofauti kukatia vyakula hivyo au uoshe ubao huo kwa sabuni na maji moto kabla na baada ya kukatia nyama mbichi au samaki.
Sasa kwa kuwa wewe, vifaa, na vyakula vyako ni safi, utatayarishaje chakula kwa njia ambayo haitakudhuru?
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
WAZOEZE WATOTO WAKO: “Sisi huwafundisha watoto wetu kunawa kabla ya kula na kuosha au kutupa chakula chochote kilichoanguka sakafuni.”—Hoi, Hong Kong