Kuutazama Ulimwengu
Ghuba ya Mexico
Baada kisima cha mafuta kilicho baharini kulipuka mnamo Aprili 2010, mafuta mengi sana yaliendelea kumwagika ndani ya bahari kwa karibu miezi mitatu. Utafiti uliofanywa na kikundi cha watafiti ulionyesha kwamba miezi miwili na nusu baada ya tukio hilo, kemikali fulani hatari zilikuwa zimetoweka. Wataalamu hao walisema kemikali hizo zililiwa na bakteria wanaoweza kumeng’enya methani. Hata hivyo, watafiti wengine hawakubaliani na utafiti huo. Wanaamini kwamba kiwango kikubwa cha mafuta kilizama kwenye sakafu ya bahari.
Urusi
Kulingana na utafiti fulani, asilimia 59 ya Warusi wenye umri wa kati ya miaka 18 na 35 wanaamini kwamba “ili kupata mafanikio maishani, wakati mwingine ni lazima ukiuke sheria na viwango vyako vya maadili,” linasema gazeti Rossiiskaya Gazeta.
Peru
Baadhi ya magunzi ya mahindi ya zamani zaidi kuwahi kupatikana (kama lile linaloonyeshwa hapa juu) yanaonyesha kwamba wenyeji wa eneo la kaskazini mwa Peru walikuwa wakitengeneza bisi na unga wa mahindi miaka 3,000 hivi iliyopita.
Italia
Lucio Soravito De Franceschi, ambaye ni askofu Mkatoliki wa Adria-Rovigo, anaamini kwamba ujumbe wa kidini “unapaswa kuwafikia watu” mahali wanapoishi. “Jukumu letu la uchungaji linapaswa kubadilika kutoka kwenye kugonga kengele za kanisa hadi kugonga kengele za milango,” anasema.
Afrika Kusini
Bei haramu ya pembe za vifaru kwa ajili ya kutengeneza dawa imepanda na kufikia dola 65,000 (za Marekani) kwa kilo moja. Katika mwaka wa 2011, nchini Afrika Kusini pekee, vifaru 448 waliuawa na wawindaji haramu. Magenge yamekuwa yakivamia majumba ya makumbusho na ya mnada barani Ulaya ili kuiba pembe hizo. Hata vifaru kwenye bustani za wanyama barani Ulaya wanaonekana kuwa hatarini.