Kuutazama Ulimwengu
Ulimwengu
Shirika la Afya Ulimwenguni limefikia mkataa kwamba kuvuta moshi unaotoka kwenye magari yanayotumia dizeli “kunaongeza hatari ya kupata kansa ya mapafu” na pia uwezekano wa kupata kansa ya kibofu cha mkojo.
Antaktika
Mabaki ya chavua na mbegu za vimelea yaliyochimbuliwa kutoka kwenye mchanga-tope wa bahari yanaonyesha kwamba mitende na miti mingine inayokua tu katika maeneo yenye joto, ilikuwepo katika eneo la Antaktika miaka mingi iliyopita. Wengi wanaamini kwamba mamilioni ya miaka iliyopita majira ya baridi kali huko Antaktika yalikuwa ya kiasi na “hayakutokeza barafu,” na halijoto katika ncha za dunia haikuwa tofauti sana na ya maeneo ya ikweta.
Ireland
Ripoti iliyotolewa katika mwaka wa 2012 na Shirika la Makasisi Wakatoliki la Ireland inaonyesha kwamba asilimia 87 ya Wakatoliki waliofanyiwa uchunguzi nchini humo wanaamini kwamba makasisi wanapaswa kuruhusiwa kuoa; asilimia 77 wanaamini kwamba wanawake wanapaswa kuruhusiwa kuwa makasisi.
Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini-Mashariki mwa Asia
Uchunguzi wa dawa za malaria ulionyesha kwamba katika maeneo fulani dawa hizo huwa za hali ya chini au bandia, na matokeo ni kwamba hazitibu vizuri au zinashindwa kutibu malaria. Katika nchi zilizo Kusini-Mashariki mwa Asia, asilimia 36 ya dawa zilizopimwa ziligunduliwa kuwa bandia, na ndivyo ilivyokuwa kwa asilimia 20 ya dawa zilizopimwa katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.
El Salvador
Katikati ya mwezi wa Aprili mwaka wa 2012, serikali ya El Salvador ilitangaza siku ya kwanza ambayo haikuwa na mauaji katika muda wa miaka mitatu hivi. Katika mwaka wa 2011, watu 69 kati ya 100,000 waliuawa kutokana na jeuri inayohusianishwa na dawa za kulevya, na hiyo ni mojawapo ya idadi kubwa zaidi ulimwenguni.