JE, NI KAZI YA UBUNI?
Manyoya ya Pengwini Anayeitwa Emperor
PENGWINI anayeitwa emperor anaweza kuogelea upesi sana majini na kuruka juu ya barafu kwa kasi ya ajabu. Anafanyaje hivyo?
Fikiria hili: Pengwini huyo hubana hewa katika manyoya yake. Kufanya hivyo hakuzuii asipigwe na baridi tu bali pia kunamwezesha kusonga kwa kasi mara mbili au tatu zaidi ya vile ambavyo angesonga. Jinsi gani? Wataalamu wanaochunguza viumbe wa baharini wamesema kwamba huenda anafanya hivyo kwa kuachilia viputo vidogo-vidogo sana vya hewa kutoka kwenye manyoya yake. Viputo hivyo vinapoachiliwa, vinasaidia kupunguza msuguano uliopo kati ya maji na manyoya ya pengwini na hivyo kumwezesha kuongeza mwendo.
Kwa kupendeza, mainjinia wamekuwa wakijifunza njia za kufanya meli zisonge kasi zaidi kwa kutumia viputo vya hewa ili kupunguza msuguano uliopo kati ya maji na meli. Hata hivyo, watafiti wanakiri kwamba si rahisi kufanya uchunguzi huo kwa kuwa “ni vigumu sana kuiga manyoya tata ya pengwini ili kubuni vifaa vinavyofanana na manyoya hayo.”
Una maoni gani? Je, manyoya ya pengwini anayeitwa emperor yalijitokeza yenyewe? Au yalibuniwa?