JE, NI KAZI YA UBUNI?
Mabawa ya Kipepeo
MABAWA ya kipepeo ni mepesi sana hivi kwamba yakipatwa na vumbi au unyevunyevu anaweza kushindwa kuruka. Hata hivyo, mabawa yake hubaki safi na makavu wakati wote. Kwa nini?
Fikiria hili: Watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Ohio, waliomchunguza kipepeo aina ya Giant Blue Morpho (Morpho didius) wamegundua kwamba ingawa bawa lake huonekana kuwa limelainika, kwa kweli lina magamba madogo yaliyolaliana kama vigae vilivyoezeka nyumba. Mpangilio wa magamba hayo hufanya iwe vigumu kwa vumbi au matone ya maji kukwama kwenye bawa. Wahandisi wanajaribu kuiga muundo wa bawa la kipepeo ili kubuni vifaa vitakavyotumiwa viwandani au hospitalini ambavyo havishiki maji au uchafu.
Bawa la kipepeo linaonyesha jinsi wanasayansi wanavyojaribu kuiga muundo wa viumbe hai. Mtafiti Bharat Bhushan anasema hivi: “Viumbe wa asili wamebuniwa kwa njia ya kustaajabisha, kuanzia viumbe wadogo hadi wakubwa, wana miundo ambayo imewashangaza wanadamu kwa miaka mingi.”
Una maoni gani? Je, bawa la kipepeo lilibuniwa? Au lilijitokeza lenyewe?