NCHI NA WATU | KAMBODIA
Kutembelea Kambodia
VIJIJI VINAVYOELEA, masoko yenye bidhaa nyingi, mitaa iliyojaa pikipiki zinazobeba kila kitu kuanzia kuku hadi friji—haya ni baadhi tu ya mambo unayoona na kusikia unapokuwa Kambodia.
Wakambodia wanajulikana sana kwa kuwa wachangamfu, wenye urafiki, na ushirikiano. Kwa kawaida wao huitana kaka, dada, shangazi, mjomba, bibi (nyanya), au babu—hata wanapokutana na mtu kwa mara ya kwanza!
Wali ni chakula kikuu cha Wakambodia. Mlo wa kawaida unakuwa angalau na aina tatu au nne za vyakula, mara nyingi supu haikosekani. Watu wengi wanapenda sana samaki. Kwa kawaida kila mlo huwa na mchanganyiko wa chakula kitamu, chenye uchachu, na chenye chumvi.
Miaka 2000 hivi iliyopita, wafanyabiashara kutoka India na watu waliokuwa wakisafiri kwenda China walipita kwenye pwani ya Kambodia na wakabadilishana bidhaa kama vile hariri na vito ili wapate vikolezo, miti yenye manukato, pembe za ndovu, na dhahabu. Baada ya muda Wakambodia waliiga tabia za India na China, na hivyo Uhindu na Ubudha ukasitawi nchini Kambodia. Leo, asilimia 90 ya watu wa Kambodia ni Wabudha.
Mashahidi wa Yehova wanahubiri ujumbe wa tumaini ulio katika Biblia nchini Kambodia. Wamewasaidia watu wengi kwa kutumia kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? Kitabu hicho kinapatikana katika lugha 250 hivi, kutia ndani Kikambodia.
Kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa?, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova, kinapatikana katika Kikambodia (kimeonyeshwa hapa).