TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA
Amri Zilizogawa Mabara
BAADA ya Christopher Columbus kurudi kutoka safari yake ya kwanza kuizunguka Amerika katika 1493, wafalme wa Hispania na Ureno walishindwa kukubaliana kuhusu ni nani atakayesimamia biashara na utawala wa kikoloni wa maeneo hayo mapya yaliyogunduliwa. Hispania ilimwomba papa, Aleksanda wa Sita, atatue mgogoro huo.
WAFALME NA MAPAPA WAGAWA MABARA
Hispania, Ureno, na Papa tayari walikuwa wamefikiria kumiliki maeneo mapya yaliyogunduliwa. Katika mwaka wa 1455, Papa Nicholas wa Tano aliipa Ureno haki zote za kuvumbua na kumiliki kila kitu walichopata katika nchi na visiwa vilivyokuwa katika Pwani ya Bahari ya Atlantiki katika Afrika. Kwenye Mkataba wa Alcáçovas wa mwaka wa 1479, Afonso wa Tano wa Ureno na mwana wake, Prince John, walisalimu mamlaka yao juu ya Visiwa vya Canary kwa Ferdinand na Isabella wa Hispania. Ikiwa sehemu ya makubaliano, Hispania ilitambua mamlaka ya Ureno ya kufanya biashara katika Afrika na umiliki wa Azores, Visiwa vya Cape Verde na Madeira. Miaka miwili baadaye, Papa Sixtus wa Nne alithibitisha mkataba huo na kutaja kihususa kwamba ugunduzi wowote mpya katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Visiwa vya Canary, ungemilikiwa na Ureno.
Hata hivyo, John, aliyekuwa John wa Pili wa Ureno, alidai kwamba maeneo yaliyogunduliwa na Columbus yalimilikiwa na Ureno. Watawala wa Hispania hawakukubaliana na uamuzi huo, hivyo wakakata rufaa kwa papa mpya, Aleksanda wa Sita, ili awape haki ya kutawala na kuanzisha Ukristo katika maeneo yaliyogunduliwa na Columbus.
Papa Aleksanda wa Sita aligawa mabara kupitia maandishi tu
Ili kusuluhisha hilo, Aleksanda aliweka amri tatu rasmi. Ya kwanza, “kwa mamlaka ya Mungu Mweza-Yote,” aliipa Hispania pendeleo la pekee la umiliki usioisha wa
maeneo mapya yaliyogunduliwa. Amri ya pili iligawanya upande wa kaskazini hadi kusini uliokuwa na urefu wa kilomita 560, magharibi mwa Visiwa vya Cape Verde. Aleksanda alisema kwamba maeneo yoyote yaliyokuwa tayari yamegunduliwa au ambayo yangegunduliwa upande wa magharibi wa mstari huo, yangemilikiwa na Hispania. Papa aligawa mabara kupitia maandishi tu! Amri yake ya tatu iliongezea Hispania umiliki katika upande wa mashariki wa dunia hadi India. Hilo lilimkasirisha sana Mfalme John, ambaye watumishi wake walikuwa wametoka tu kuzunguka kusini mwa Afrika, na hivyo kupanua mamlaka ya Ureno kufikia Bahari ya Hindi.RAMANI YAGAWANYWA TENA
Akiwa amechoshwa na Aleksanda, * John alifanya makubaliano ya moja kwa moja na Ferdinand na Isabella. Mwandishi William Bernstein anasema hivi: “Watawala wa Hispania walikazia fikira zaidi kumiliki maeneo mapya katika Amerika na pia waliwaogopa sana Wareno waliokuwa wakatili, hivyo walikuwa tayari kufikia makubaliano nao.” Hivyo, mnamo 1494 mkataba ulioitwa Tordesillas ulitiwa sahihi katika mji huo wa Hispania.
Mkataba wa Tordesillas ulidumisha mstari wa upande wa kaskazini hadi kusini uliowekwa na Aleksanda, lakini ukauongeza mpaka kufikia urefu wa kilomita 1,480 zaidi magharibi. Ilidaiwa kwamba bara la Afrika na Asia “yalimilikiwa” na Ureno; na Amerika ilimilikiwa na Hispania. Kuhamishwa huko kwa mstari mpaka upande wa magharibi, kulipanua eneo la utawala wa Ureno mpaka kwenye eneo lililogunduliwa baadaye na kuitwa Brazili.
Amri zilizoipa mamlaka Hispania na Ureno kumiliki na kutetea maeneo mapya waliyopata, zilitumiwa kama msingi wa umwagaji mkubwa wa damu. Amri hizo zilipuuza haki za watu walioishi katika maeneo yaliyogunduliwa kwa kuwakandamiza na kuwatendea isivyo haki. Zimekuwa pia chanzo cha mgogoro wa karne nyingi miongoni mwa mataifa kuhusu umiliki na uhuru wa kutumia bahari.
^ fu. 9 Kwa habari zaidi kuhusu papa huyo aliyejulikana kwa kuwa fisadi, tazama makala “Aleksanda wa Sita—Papa Asiyesahauliwa na Roma,” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi, Juni 15, 2003, ukurasa 26-29.