TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA
Galileo
Kati ya karne ya 14 na 16, wanasayansi na wanafalsafa wa Ulaya walianza kuelewa ulimwengu katika njia ambayo ilipingana na mafundisho ya Kanisa Katoliki. Mtu mmoja aliyechunguza upya mbingu ni Galileo Galilei.
KABLA ya kuwapo kwa Galileo, watu wengi waliamini kwamba jua, sayari, na nyota zilizunguka dunia. Imani hiyo ilikuwa miongoni mwa mafundisho rasmi ya Kanisa Katoliki.
Akitumia darubini yake, Galileo alipata ushahidi unaopingana na mafundisho ya kisayansi yaliyokubaliwa na wengi. Kwa mfano, alipotazama madoa meusi yaliyoonekana katika uso wa jua yakihama, alitambua kwamba jua linazunguka katika mhimili. Utafiti kama huo umemsaidia mwanadamu kuongeza ujuzi wake kuhusu ulimwengu kwa kiasi kikubwa, ijapokuwa uchunguzi huo ulikuwa chanzo cha ugomvi kati ya Galileo na Kanisa Katoliki.
SAYANSI NA DINI
Miaka mingi mapema, mtaalamu wa nyota kutoka Poland, Nicolaus Copernicus, alianzisha nadharia ya kwamba dunia inazunguka jua. Galileo alichunguza utafiti wa Copernicus kuhusu mwendo wa vitu vilivyo angani na kukusanya ushahidi akitegemea nadharia hiyo. Mwanzoni, Galileo alisita kusema kuhusu utafiti wake kwa sababu ya kuhofu kwamba atadhihakiwa na kupuuzwa.
Akiwa ameshindwa kuzuia msisimuko wake kutokana na yale aliyoona kupitia darubini yake, Galileo alianza kusema kuhusu utafiti wake. Baadhi ya wanasayansi waliona utafiti wake kuwa chanzo cha ubishi, na baada ya muda mfupi, makasisi walianza kutumia majukwaa ya kanisa kumpinga Galileo.Katika mwaka wa 1616, Kadinali Bellarmine, “mwanatheolojia maarufu wakati huo,” alimweleza Galileo kuhusu amri mpya iliyowekwa na Kanisa Katoliki dhidi ya mawazo ya Copernicus. Alimsisitiza sana Galileo kukubaliana na amri hiyo, na kwa miaka mingi baadaye, Galileo hakupinga waziwazi kwamba dunia inazunguka jua.
Katika mwaka 1623, Papa Urban wa Nane, aliyekuwa rafiki wa Galileo, alianza kutawala. Hivyo, katika mwaka wa 1624, Galileo alimwomba papa aondoe amri iliyowekwa mwaka 1616. Badala ya kufanya hivyo, Urban alimsihi Galileo kufafanua nadharia zinazopingana za Copernicus na Aristotle katika njia ambayo haitapendelea yeyote kati ya hizo.
Hivyo, Galileo akaandika kitabu chenye kichwa Dialogue on the Great World Systems. Ingawa papa alimwagiza Galileo kutopendelea upande wowote, kitabu hicho kilipendelea mawazo ya Copernicus. Baada ya muda mfupi tu, maadui wa Galileo walianza kudai kwamba kitabu chake kinamdhihaki papa. Akiwa ameshitakiwa kuwa mzushi wa kidini na kutishiwa kuteswa, Galileo alilazimishwa kukataa mafundisho ya Corpenicus. Katika mwaka wa 1633, Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi, lilimhukumu kifungo cha kudumu cha nyumbani, na kupiga marufuku vitabu vyake. Galileo alikufa akiwa nyumbani kwake katika mji wa Arcetri, karibu na Florence, Januari 8, 1642.
Papa John Paul wa Pili, alikubali kwamba Kanisa Katoliki lilimhukumu kimakosa Galileo
Kwa mamia ya miaka, baadhi ya utafiti wa Galileo uliendelea kuwa katika orodha ya vitabu ambavyo Wakatoliki hawakuruhusiwa kusoma. Hata hivyo, katika mwaka wa 1979, kanisa hilo lilichunguza tena hatua iliyochukuliwa na Baraza la Kikatoliki la Kuhukumu Wazushi miaka 300 iliyopita. Mwishowe, katika mwaka wa 1992, Papa John Paul wa Pili, alikubali kwamba Kanisa Katoliki lilimhukumu kimakosa Galileo.