“Ndugu wa Poland”—Kwa Nini Walinyanyaswa?
“Ndugu wa Poland”—Kwa Nini Walinyanyaswa?
Mwaka wa 1638 bunge la Poland lilikitenda visivyo kikundi cha dini kilichoitwa Ndugu wa Poland. Kanisa na matbaa za kikundi hicho ziliharibiwa. Chuo Kikuu cha Raków kilifungwa na maprofesa waliofundisha humo wakapelekwa uhamishoni.
Miaka 20 baadaye, bunge lilichukua hatua nyingine zaidi. Liliamuru washiriki wote wa kikundi hicho, ambao huenda walikuwa 10,000 au zaidi, waondoke nchini humo. Hali ilipataje kuwa hatari hivyo katika nchi iliyoonwa kuwa mojawapo ya nchi za Ulaya zenye uhuru mwingi? Ndugu wa Poland walikuwa wamefanya nini ili kustahili kutendwa vibaya hivyo?
YOTE hayo yalianza pengo kubwa lilipozuka ndani ya Kanisa la Calvin la Poland. Hoja kuu iliyobishaniwa ilikuwa fundisho la Utatu. Viongozi wa harakati iliyopendezwa na dhana mpya kanisani walikataa fundisho hilo na kusema kuwa halikupatana na Maandiko. Hilo liliwakasirisha viongozi wa kanisa na kusababisha harakati hiyo iliyopendezwa na dhana mpya kujitenga.
Wakalvini waliwaita wapinzani hao Waaria, * lakini waumini wa kikundi hicho kipya walipendelea kujiita Wakristo au Ndugu wa Poland. Pia wao huitwa Wasosini, jina linalotokana na Laelius Socinus, Mwitalia aliyechochewa na Servetus na ambaye mpwa wake wa kiume, Faustus Socinus alisafiri kwenda Poland na akawa maarufu katika harakati hiyo.
Wakati huo kabaila Mpolandi, Jan Sienieński, alinuia kulipa kanisa hilo jipya kile alichokiita “mahali patulivu, patawa” ili lisitawi. Akitumia pendeleo la pekee alilopewa na mfalme wa Poland, Sienieński alianzisha mji wa Raków, ambao baadaye ulipata kuwa makao makuu ya Usosini nchini Poland. Sienieński aliwapa wakazi wa Raków haki kadhaa, kutia ndani haki ya kuabudu kwa uhuru.
Wasanii, madaktari, wafamasi, watu wa mjini, na watu wa dini mbalimbali walivutiwa na mji huo mpya. Isitoshe, makasisi walimiminika humo kutoka Poland, Lithuania, Transylvania, Ufaransa, na hata Uingereza. Hata hivyo, baadhi ya wageni hao waliowasili hawakuwa na imani za Kisosini; kwa hiyo kwa miaka mitatu iliyofuata, tangu 1569 hadi 1572, Raków pakawa mahali pa mijadala ya kitheolojia isiyo na mwisho. Ikawaje basi?
Nyumba Yagawanyika
Harakati yenyewe ya Wasosini ikagawanyika, wale waliokubali maoni ya kupita kiasi upande mmoja na wale ambao maoni yao yalikuwa ya kiasi zaidi upande mwingine. Hata hivyo, licha ya tofauti zao, imani walizokuwa nazo zilikuwa za pekee. Walikataa Utatu; walikataa kubatiza vitoto vichanga; kwa jumla hawakubeba silaha na mara nyingi hawakukubali nyadhifa katika * Pia walipinga kuwepo kwa helo pakiwa mahali pa mateso. Katika yote hayo, walipuuza mapokeo ya kidini yaliyokuwa maarufu.
serikali.Makasisi Wakalvini na Wakatoliki walizusha upinzani mkali dhidi ya kikundi hicho, lakini wahudumu Wasosini wakatumia fursa hiyo ya uhuru wa kidini, ulioungwa mkono na wafalme wa Poland kama vile Augustus Sigismund wa Pili na Stephen Báthory, ili kufundisha dhana zao.
Kazi Muhimu ya Budny
Tafsiri ya Biblia ya Kikalvini, ambayo ilitumiwa sana wakati huo, haikuwaridhisha wasomaji wengi. Haikutafsiriwa kutoka katika lugha za awali bali kutoka katika Vulgate ya Kilatini na tafsiri nyingine ya Kifaransa ya wakati huo. Mtaalamu mmoja asema kwamba “kwa sababu ya kujaribu kuifanya iwe na muundo wenye kuvutia, ilipoteza uaminifu na usahihi.” Makosa mengi yaliingizwa. Kwa hiyo, msomi ajulikanaye sana aliyeitwa Szymon Budny akaombwa airekebishe tafsiri hiyo. Alikata kauli kwamba ingalikuwa rahisi zaidi kutafsiri upya kuliko kusahihisha tafsiri hiyo nzee. Budny akaanza mradi huo wapata mwaka wa 1567.
Alipokuwa akitafsiri, Budny alichanganua kikamili kila neno na namna mbalimbali za neno hilo kwa njia ambayo hakuna mwingine yeyote nchini Poland alikuwa amefanya. Ilipokuwa vigumu kutafsiri maana ya maandishi ya Kiebrania, alionyesha tafsiri sisisi katika maandishi ya pambizoni. Nyakati nyingine alilazimika kubuni maneno mapya kwa kuunganisha maneno naye alijaribu kutumia lugha sahili ya siku zake, iliyotumika kila siku nchini Poland. Alikusudia kuwaandalia wasomaji tafsiri ya Biblia yenye uaminifu na sahihi.
Tafsiri ya Budny ya Biblia nzima ilichapishwa mwaka wa 1572. Hata hivyo, walioichapisha walifisidi tafsiri yake ya Maandiko ya Kigiriki. Bila kuvunjika moyo, Budny akaanza kutayarisha tafsiri iliyofanyiwa marekebisho, ambayo ilimalizika miaka miwili baadaye. Tafsiri bora ya Budny ya Maandiko ya Kigiriki ilipita ubora wa tafsiri za Kipolandi za awali. Isitoshe, katika sehemu nyingi, alirejeza jina la Mungu, Yehova.
Mwishoni-mwishoni mwa karne ya 16 na miaka thelathini ya kwanza ya karne ya 17, Raków, jiji kuu la harakati hiyo, likawa kituo cha kidini na kisomi. Viongozi na waandishi wa Ndugu wa Poland walichapisha trakti na vichapo vyao huko.
Waliendeleza Elimu
Uchapishaji wa Ndugu wa Poland ulianza kupamba moto wapata mwaka wa 1600, matbaa ilipoanza kutumika huko Raków. Matbaa hiyo ingeweza kutokeza vitabu vidogo-vidogo na pia vitabu vikubwa katika lugha mbalimbali. Kikiwa kituo cha uchapishaji, punde si punde Raków lilianza kulingana na majiji bora barani Ulaya. Yaaminika kwamba vichapo vipatavyo 200 vilichapishwa katika matbaa hiyo katika miaka 40 iliyofuata. Kiwanda cha karatasi kilichokuwa karibu, kilichokuwa cha Ndugu wa Poland, kiliandaa karatasi bora kwa ajili ya vichapo hivyo.
Muda si muda Ndugu wa Poland wakaona uhitaji wa kuelimisha waumini wenzao na watu wengine. Kwa hiyo, Chuo Kikuu cha Raków kikaanzishwa mwaka wa 1602. Wana wa Ndugu wa Poland, hali kadhalika wavulana Wakatoliki na Waprotestanti, walisomea humo. Ingawa chuo hicho kikuu kilikuwa seminari ya kitheolojia, dini silo somo pekee lililofunzwa. Lugha za kigeni, elimu-maadili, ekonomia, historia, sheria, mantiki, sayansi, hesabu, tiba, na sarakasi pia yalikuwa sehemu ya utaratibu wa masomo. Chuo kikuu hicho kilikuwa na maktaba kubwa, ambayo iliendelea kukua, kwa sababu ya matbaa iliyokuwako.
Karne ya 17 ilipoendelea, ilionekana kana kwamba Ndugu wa Poland wangeendelea kusitawi. Hata hivyo, sivyo ilivyokuwa.
Kanisa na Serikali Zashambulia
Zbigniew Ogonowski wa Chuo cha Sayansi cha Poland aeleza hivi: “Mwishoni mwa karne ya 17, hali ya Waaria nchini Poland ilianza kuzorota upesi.” Hilo lilitokezwa na utendaji wa makasisi Wakatoliki uliozidi kuwa wa kijasiri. Makasisi walifanya yote wawezayo, kutia ndani kuchongea na
kuchapisha maandishi ya kukashifu, ili kuwaharibia sifa Ndugu wa Poland. Shambulio hilo lilirahisishwa na hali za kisiasa zilizokuwa zimebadilika nchini Poland. Mfalme mpya wa Poland Vasa Sigismund wa Tatu, alikuwa adui wa Ndugu wa Poland. Vivyo hivyo waandamizi wake, hasa Casimir Vasa John wa Pili, waliunga mkono jitihada za Kanisa Katoliki la kuzuia Ndugu wa Poland.Mambo yalifikia upeo ilipodaiwa kwamba wanafunzi kadhaa wa Raków walikufuru msalaba kimakusudi. Kisa hicho kikawa kisingizio cha kuharibu makao makuu ya Ndugu wa Poland. Mwenye Raków alishtakiwa mbele ya mahakama ya bunge kwamba ‘anaeneza uovu’ kwa kuunga mkono Chuo Kikuu cha Raków pamoja na matbaa. Ndugu wa Poland walituhumiwa kwa utendaji wenye kupindua, wa kushiriki katika karamu za ulafi, ulevi, na uasherati, na kuishi maisha ya ukosefu wa adili. Bunge liliamua kwamba Chuo Kikuu cha Raków kifungwe na matbaa na kanisa la Ndugu wa Poland ziharibiwe. Waumini wakaamriwa waondoke jijini humo. Maprofesa wa chuo kikuu walifukuzwa nchini la sivyo wahukumiwe kifo. Ndugu fulani wa Poland wakahamia mahali salama zaidi, kama vile Silesia na Slovakia.
Mwaka wa 1658 bunge liliagiza kwamba Ndugu wa Poland wauze mali yao na kuhamia nchi nyingine kabla ya miaka mitatu kwisha. Baadaye muda huo ukapunguzwa na kuwa miaka miwili. Yeyote aliyedai kuwa na imani zao baada ya hapo angeuawa.
Wasosini fulani wakapiga kambi Uholanzi, ambako waliendelea na utendaji wao wa uchapishaji. Huko Transylvania kutaniko liliendelea kuwapo hadi mwanzoni mwa karne ya 18. Kwenye mikutano, iliyoongozwa hata mara tatu kwa juma, waliimba zaburi, wakasikiliza mahubiri, na kusoma katekisimu iliyokuwa imeandaliwa ili kufafanua mafundisho yao. Ili kudumisha utakato wa kutaniko, waumini wenzi walisahihishwa, wakahimizwa, na ilipohitajika, wakafukuzwa.
Ndugu wa Poland walikuwa wanafunzi wa Neno la Mungu. Waligundua kweli nyingi zenye thamani, nao hawakusita kuwajulisha wengine juu yake. Hatimaye, hata hivyo, walisambaa kotekote barani Ulaya na ikawa vigumu zaidi na zaidi kudumisha muungano wao. Kisha, Ndugu wa Poland wakatoweka.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Arius (250-336 W.K.) alikuwa kasisi wa Aleksandria aliyedai kwamba Yesu alikuwa mdogo kuliko Baba. Baraza la Nisea lilikatalia mbali maoni yake mwaka wa 325 W.K.—Ona Amkeni! la Machi 8, 1990, ukurasa wa 29.
^ fu. 9 Ona Amkeni! la Februari 8, 1990, ukurasa wa 15, “Wasosini—Kwa Nini Walikataa Utatu?”
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nyumba iliyokuwa ya mhudumu Msosini
[Picha katika ukurasa wa 23]
Juu: Rakow Leo; wa kulia kuna nyumba ya watawa iliyoanzishwa mwaka wa 1650 ili kuondolea mbali “Uaria” wowote uliosalia; chini: Makasisi Wakatoliki walisimamisha msalaba mahali hapa ili kuzusha zogo dhidi ya Ndugu wa Poland
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
Title card of Biblia nieświeska by Szymon Budny, 1572