Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unajua Nini Kuhusu Uchawi?

Unajua Nini Kuhusu Uchawi?

Unajua Nini Kuhusu Uchawi?

UCHAWI! Neno hilo lakukumbusha nini?

Kwa wengi, uchawi hasa ni ushirikina na mazingaombwe, yasiyopaswa kuzingatiwa kwa makini. Kwa maoni yao, uchawi ni jambo la kuwaziwa tu—wachawi wazee ambao wamevalia majoho yenye kufunika kichwa wanaoongeza mabawa ya popo kwenye jungu la maji yenye kuchemka, wanaogeuza watu kuwa vyura, na kuruka angani usiku kwa kutumia mpini wa ufagio huku wakicheka kwa nia ya kudhuru wengine.

Kwa wengine, uchawi ni jambo zito. Wachunguzi fulani husema kwamba zaidi ya nusu ya idadi ya watu ulimwenguni wanaamini kwamba wachawi ni halisi na wanaweza kuathiri maisha ya wengine. Mamilioni huamini kwamba uchawi ni mbaya, hatari, na wapaswa kuogopwa sana. Kwa mfano, kitabu kimoja juu ya dini ya Kiafrika chasema: “Imani katika kusudi na hatari za mizungu mibaya, ulozi na uchawi imekolea katika maisha ya Waafrika . . . Wachawi na walozi ndio watu wenye kuchukiwa zaidi katika jumuiya zao. Hata kufikia wakati huu kuna sehemu na pindi ambapo wao hupigwa na watu hadi kifo.”

Hata hivyo, katika nchi za Magharibi, uchawi umeanza kuheshimiwa. Vitabu, televisheni, na sinema zimesaidia sana kupunguza hofu ya uchawi. Mchanganuzi wa vitumbuizo, David Davis, asema: “Kwa ghafula, wachawi wamekuwa wachanga na wenye kuvutia zaidi, naam, warembo zaidi. Watengeneza-sinema wa Hollywood wanatambua maelekeo upesi sana. . . . Kwa kuwafanya wachawi waonekane warembo zaidi na wenye kupendeka, watengeneza-sinema hao wanaweza kuvutia watazamaji wengi, kutia ndani wanawake na watoto.” Wanajua jinsi ya kubadili kila mwelekeo kuwa mradi wenye kunufaisha kifedha.

Wengine husema kwamba uchawi umekuwa mojawapo ya harakati za kiroho zinazokua kwa kasi zaidi huko Marekani. Kotekote katika nchi ambazo zimesitawi, idadi inayoongezeka ya watu wenye kuchochewa na wanaharakati wa kutetea haki na usawa wa wanawake, na ambao wamepoteza imani katika dini mashuhuri, hutafuta kutimiza mahitaji yao ya kiroho kwa kujihusisha na aina mbalimbali za uchawi. Kwa kweli, kuna aina nyingi sana za uchawi hivi kwamba watu hutofautiana hata kuhusu maana ya neno “mchawi.” Hata hivyo, mara nyingi wale wanaodai kuwa wachawi hujitambulisha kuwa wa dini ya Wicca—ambayo inafafanuliwa katika kamusi moja kuwa “dini ya kipagani inayoabudu nguvu za asili iliyoanzia magharibi mwa Ulaya kabla ya Ukristo na ambayo inapata uhuisho wa karne ya 20.” * Hivyo, wengi hujiita wapagani au wapagani mamboleo.

Katika historia yote, wachawi wamechukiwa, wakanyanyaswa, wakateswa, na hata kuuawa. Si ajabu kwamba wachawi wa siku hizi wanataka sana kueleweka vema zaidi. Katika uchunguzi mmoja, idadi kubwa ya wachawi waliulizwa ujumbe ambao wangetaka kuambia watu. Jibu lao ambalo limefupishwa na Margot Adler lilikuwa: “Sisi si waovu. Hatuabudu Ibilisi. Hatudhuru wala kushawishi watu. Sisi si hatari. Sisi ni watu wa kawaida kama nyinyi. Tuna familia, kazi, matumaini, na miradi pia. Sisi si madhehebu. Sisi si watu wa kuogofya. . . . Hampaswi kutuogopa. . . . Sisi tunafanana nanyi zaidi kuliko vile mnavyofikiri.”

Watu wanazidi kuukubali ujumbe huo. Lakini je, hilo lamaanisha kwamba hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu zoea la uchawi? Hebu tuchunguze swali hilo katika makala ifuatayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Neno la Kiingereza ambalo limetafsiriwa uchawi linatokana na maneno ya Kiingereza cha Zamani “wicce” na “wicca,” ambayo hurejezea wachawi wanaume na wanawake pia.