Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwenda Kufanya Kazi Visiwa vya Pasifiki!

Kwenda Kufanya Kazi Visiwa vya Pasifiki!

Kwenda Kufanya Kazi Visiwa vya Pasifiki!

KUMBI za abiria kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa vya Brisbane na Sydney, Australia, zilijaa msisimko kuliko kawaida. Kikundi cha watu 46 kilikuwa tayari kusafiri hadi Samoa ili kuungana na wengine 39 kutoka New Zealand, Hawaii, na Marekani. Walikuwa na mizigo ya ajabu sana, yaani vifaa, kama vile nyundo, misumeno, na keekee, vifaa ambavyo kwa kawaida mtu hangebeba anaposafiri kwenye kisiwa maridadi cha Pasifiki. Lakini mradi wao pia haukuwa wa kawaida.

Walikuwa wanajitayarisha kusafiri kwa gharama yao wenyewe kwenda kufanya kazi kwa majuma mawili wakiwa wajitoleaji wasiolipwa katika programu ya ujenzi inayosimamiwa na Ofisi ya Uhandisi ya Kimkoa kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Australia. Programu hiyo, inayotegemezwa kwa michango ya hiari, yatia ndani ujenzi wa Majumba ya Ufalme, Majumba ya Kusanyiko, makao ya mishonari, na ofisi za tawi au za tafsiri kwa ajili ya makutaniko ya Mashahidi wa Yehova yanayoongezeka haraka katika visiwa vya Pasifiki. Acheni tuwajue baadhi ya wafanyakazi waliokuwa katika vikundi vya kujenga Majumba ya Ufalme vya nchi zao.

Mwezekaji-nyumba aitwaye Max anatoka katika mji wa Cowra, jimbo la New South Wales, Australia. Ameoa na ana watoto watano. Arnold anatoka Hawaii. Yeye na mkewe wana watoto wawili, naye pia ni painia, au mhudumu wa wakati wote. Max na Arnold ni wazee katika makutaniko ya kwao. Ni wazi kwamba watu hao—sawa na wengine katika programu hiyo—hawakujitolea kwa sababu tu wana wakati mwingi. Badala yake, wao na familia zao wanatambua uhitaji fulani, nao wanataka kufanya wanayoweza ili kusaidia.

Wafanyakazi Kutoka Mataifa Mbalimbali Watimiza Uhitaji Muhimu

Mojawapo ya mahali ambapo ustadi na huduma zao zilihitajika ni Tuvalu, ambalo ni taifa la Pasifiki lenye watu wapatao 10,500 lililo kwenye kikundi cha mbali cha visiwa tisa vya matumbawe karibu na ikweta, kaskazini-magharibi ya Samoa. Kila kimoja cha visiwa hivyo kina ukubwa upatao kilometa za mraba 2.5. Kufikia mwaka wa 1994, Mashahidi 61 katika eneo hilo walihitaji Jumba jipya la Ufalme na ofisi kubwa ya tafsiri haraka.

Katika eneo hilo la Pasifiki ya tropiki, hapana budi kujenga nyumba zinazostahimili dhoruba na vimbunga vikali vinavyotokea mara nyingi. Lakini vifaa bora vya ujenzi ni vichache sana kwenye visiwa hivyo. Suluhisho? Vifaa vyote—mabati na mihimili pamoja na fanicha na pazia, vifaa vya choo na mabomba ya bafu, hata misumari—vilisafirishwa kwa meli kutoka Australia.

Kabla ya vifaa hivyo kuwasili, kikundi kidogo kilitangulia na kutengeneza mahali pa ujenzi na kuweka msingi. Kisha wafanyakazi wa kimataifa wakaja kujenga, kupaka rangi, na kuweka fanicha katika majengo hayo.

Utendaji huo wote katika visiwa vya Tuvalu uliamsha hasira kali ya kasisi mwenyeji ambaye alitangaza kwenye redio kwamba Mashahidi wanajenga “Mnara wa Babeli”! Lakini ukweli wa mambo ulikuwaje? “Watu waliokuwa wakijenga Mnara wa Babeli unaotajwa katika Biblia walipotambua kuwa hawaelewani kwa sababu Mungu ameichafua lugha yao, waliuacha mradi wao pasipo kuukamilisha mnara,” asema Graeme, mfanyakazi wa kujitolea. (Mwanzo 11:1-9) “Hali ni kinyume kabisa watu wanapomfanyia Yehova Mungu kazi. Licha ya tofauti za lugha na desturi, wakati wote miradi hiyo hukamilika.” Na mradi huu pia ulikamilika—kwa majuma mawili tu. Naam, watu 163, akiwemo mke wa waziri mkuu, walihudhuria sherehe ya kuweka wakfu.

Doug, msimamizi wa mradi huo, asema hivi akikumbuka mambo hayo: “Ilifurahisha kufanya kazi na wajitoleaji kutoka nchi nyinginezo. Tuna njia tofauti-tofauti za kufanya mambo, istilahi tofauti-tofauti, hata vipimo tofauti-tofauti, ingawa hivyo mambo hayo hayakusababisha matatizo yoyote.” Ndugu huyo, ambaye ameshiriki miradi kadhaa ya aina hiyo, aongeza kusema: “Hilo huimarisha maoni yangu kwamba kwa msaada wa Yehova watu wake waweza kujenga mahali popote duniani, haidhuru mahali hapo pamejitenga au ni pagumu jinsi gani. Ni kweli kuwa tuna watu wengi wenye ustadi, lakini roho ya Yehova ndiyo huwezesha hayo.”

Roho ya Mungu pia huzichochea familia za Mashahidi kwenye visiwa hivyo ziandae chakula na makazi, vitu ambavyo ni gharama kubwa kwa wengine. Wale wanaoonyeshwa ukarimu huo huuthamini sana. Ken, kutoka Melbourne, Australia, alifanya kazi kwenye mradi kama huo huko Polynesia ya Ufaransa. Asema hivi: “Tulikuja kutumika, lakini tukatendewa kama wafalme.” Inapowezekana, Mashahidi wenyeji pia husaidia katika ujenzi. Kwenye Visiwa vya Solomon, wanawake walichanganya kokoto—kwa mikono. Wanaume na wanawake mia moja walikwea milima mirefu yenye mvua nyingi, wakaleta zaidi ya tani 40 za mbao. Vijana walisaidia pia. Mfanyakazi mmoja wa kutoka New Zealand akumbuka hivi: “Namkumbuka ndugu mchanga wa kisiwani aliyebeba mifuko miwili hadi mitatu ya saruji kwa wakati mmoja. Pia alipakua changarawe kwa sepetu mchana kutwa kukiwa na joto na mvua.”

Inanufaisha sana Mashahidi wenyeji wanapoishiriki kazi hiyo. Ofisi ya tawi ya Samoa ya Watch Tower Society yaripoti: “Ndugu wa visiwani wamejifunza ustadi wa kazi wanaoweza kutumia kujenga Majumba ya Ufalme na kufanya marekebisho baada ya kimbunga. Ustadi huo unaweza pia kuwasaidia kujiruzuku katika jumuiya ambamo ni vigumu kwa wengi kujiruzuku.”

Programu ya Ujenzi Yatoa Ushahidi Mzuri

Colin alikuwa Honiara naye akaona Jumba la Kusanyiko la Visiwa vya Solomon likijengwa. Kwa kuvutiwa, aliiandikia ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ya huko ujumbe huu: “Watu wote wameungana na hapana anayenung’unika, wao ni kama familia moja.” Muda mfupi baadaye, aliporudi kijijini kwake huko Aruligo, umbali wa kilometa 40, yeye na familia yake walijenga Jumba lao wenyewe la Ufalme. Kisha wakatuma ujumbe mwingine kwa ofisi: “Jumba letu la Ufalme, pamoja na jukwaa, limekamilika, basi twaweza kufanya mikutano fulani hapa?” Mikutano hiyo ilipangwa mara moja, na zaidi ya watu 60 huhudhuria kwa ukawaida.

Mshauri mmoja wa Muungamano wa Ulaya aliona mradi huo huko Tuvalu. “Labda kila mtu anawaambia jambo hili,” akamwambia mfanyakazi fulani, “kwa maoni yangu, huu ni mwujiza!” Mwanamke aliyekuwa akifanya kazi kwenye maungio ya simu alimwuliza mfanyakazi mwingine wa kujitolea aliyezuru: “Mbona nyinyi nyote mna furaha sana? Hapa pana joto kali!” Hawakuwa wameona kamwe Ukristo ukitenda kazi kwa njia hiyo yenye kutumika na ya kujitolea.

Kujitolea Pasipo Kujuta

“Yeye apandaye kwa wingi atavuna pia kwa wingi,” Biblia yasema kwenye 2 Wakorintho 9:6. Wafanyakazi, familia zao, na makutaniko yao wanaendelea kupanda kwa wingi kwa kuwasaidia Mashahidi wenzao katika Pasifiki. “Kutaniko langu lilichangia zaidi ya theluthi moja ya nauli yangu,” asema Ross, mzee kutoka Kincumber, karibu na Sydney, “na shemeji yangu, aliyeandamana nasi pia, aliongezea dola 500.” Mfanyakazi mwingine aligharimia safari yake kwa kuuza gari lake. Mwingine naye akauza shamba lake. Kevin alihitaji dola 900 zaidi, basi akaamua kuuza hua zake 16 wenye umri wa miaka miwili. Kupitia rafiki yake, alifaulu kupata mnunuzi aliyempa dola 900 kamili kwa hua hao!

“Je, ilifaa kulipa nauli ya ndege na kupoteza mshahara wote huo jumla ya dola 6,000?” Danny na Cheryl wakaulizwa. “Ndiyo! Hata kama gharama hiyo ingekuwa maradufu, bado ingefaa,” wakajibu. Alan, kutoka Nelson, New Zealand, aliongezea: “Fedha nilizotumia kwenda Tuvalu zingaliweza kunifikisha Ulaya na bado nibaki na nyingine za ziada. Lakini je, kweli ningalipata baraka hizo, au ningalipata marafiki wengi kutoka sehemu mbalimbali, au kufanyia mtu mwingine jambo fulani badala ya kujifanyia mimi mwenyewe tu? La! hata hivyo, haidhuru kile nilichowapa ndugu zetu wa visiwani, wao walinipa mengi zaidi.”

Jambo jingine muhimu linalofanikisha programu hiyo ni utegemezo wa familia. Ingawa baadhi ya wake wanaweza kuandamana na waume zao na hata kusaidia kazini, wengine wana wajibu wa kutunza watoto wanaokwenda shuleni au biashara ya familia. “Utayari wa mke wangu wa kuwatunza watoto na nyumba nilipokuwa sipo,” akasema Clay, “ulikuwa ni ujitoleaji mkubwa sana hata kuliko wangu.” Kwa kweli, waume wote ambao hawakuweza kuandamana na wake zao wanakubaliana kwa dhati na maneno hayo!

Tangu kukamilika kwa mradi huko Tuvalu, wafanyakazi wa kujitolea wamejenga Majumba ya Ufalme, Majumba ya Kusanyiko, makao ya mishonari, na ofisi za tafsiri huko Fiji, Tonga, Papua New Guinea, New Caledonia, na kwingineko. Miradi mingi, kutia ndani mingine katika eneo la Kusini-Mashariki ya Asia, ingali inapangwa. Je, wafanyakazi wa kutosha watapatikana?

Yaonekana hilo halitakuwa tatizo. “Kila mtu hapa ambaye ameshiriki katika miradi ya kimataifa ya ujenzi ameomba akumbukwe wakati mradi mwingine unapopangwa,” yaandika ofisi ya tawi ya Hawaii. “Punde tu warudipo nyumbani, wao huanza kuweka akiba ya fedha kwa ajili ya miradi hiyo.” Mbona programu hiyo isifanikiwe kwa kuwa mbali na baraka nyingi za Yehova kuna ujitoaji kama huo usio na ubinafsi?

[Picha katika ukurasa wa 9]

Vifaa vya mradi huo

[Picha katika ukurasa wa 9]

Wafanyakazi mahali pa ujenzi

[Picha katika ukurasa wa 10]

Miradi ilipokamilika, tulifurahia kile ambacho roho ya Mungu ilikuwa imetimiza