Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Imani Inadumu Kuliko Dhahabu Safi

Imani Inadumu Kuliko Dhahabu Safi

Imani Inadumu Kuliko Dhahabu Safi

DHAHABU hutafutwa sana kwa sababu ya uzuri wake na inadumu sana. Inapendwa kwa sababu mng’ao wake huonekana kana kwamba unadumu milele. Hiyo ni kwa sababu dhahabu haiwezi kuharibiwa na maji, oksijeni, salfa, na vitu vinginevyo. Vitu vingi vya zamani vilivyotengenezwa kwa dhahabu ambavyo hupatikana katika meli zilizozama na kwingineko, huwa bado zinang’aa hata baada ya mamia ya miaka.

Hata hivyo, ajabu ni kwamba Biblia inasema kuwa kuna kitu kinachodumu zaidi na chenye “thamani kubwa zaidi sana kuliko dhahabu ambayo huharibika ijapokuwa kuthibitishwa kwayo na moto.” (1 Petro 1:7) Dhahabu ambayo ‘imethibitishwa’ au kusafishwa kwa moto au kwa njia nyinginezo inaweza kuwa safi sana. Lakini hata dhahabu iliyosafishwa huharibika, au huyeyuka inapotiwa katika mchanganyiko wa asidi ya haidrokloriki na asidi ya nitrati. Hivyo, Biblia ni sahihi kisayansi inaposema ‘dhahabu huharibika.’

Kinyume cha hilo, imani ya kweli ya Kikristo ‘huhifadhi hai nafsi.’ (Waebrania 10:39) Wanadamu wanaweza kumwua mtu mwenye imani yenye nguvu, kama walivyomwua Yesu Kristo. Lakini wale walio na imani ya kweli wamepewa ahadi hii: “Jithibitishe mwenyewe kuwa mwaminifu hata kufikia kifo, nami hakika nitakupa taji la uhai.” (Ufunuo 2:10) Watu wanaokufa wakiwa waaminifu hubaki katika kumbukumbu ya Mungu, naye atawafufua. (Yohana 5:28, 29) Hakuna kiasi chochote cha dhahabu kiwezacho kutimiza hilo. Kwa hiyo, ni kweli kwamba imani ina thamani kubwa zaidi kuliko dhahabu. Hata hivyo, ili imani iwe na thamani kubwa hivyo, ni lazima ithibitishwe au ijaribiwe. Kwa kweli, ‘ubora wa imani yetu uliojaribiwa’ ndio ambao Petro alisema una thamani zaidi kuliko dhahabu. Mashahidi wa Yehova watafurahi kukusaidia kujifunza Biblia ili usitawishe na kudumisha imani yenye nguvu katika Mungu wa kweli, Yehova, na Mwana wake, Yesu Kristo. Kulingana na Yesu, imani hiyo itakuwezesha kupata “uhai udumuo milele.”—Yohana 17:3.