Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wasikithe—Watu wa Kale Wenye Kushangaza

Wasikithe—Watu wa Kale Wenye Kushangaza

Wasikithe—Watu wa Kale Wenye Kushangaza

WAPANDA-FARASI wa taifa hilo la watu wenye kuhama-hama wawasili mbiombio wakiwa wamejaza mifuko yao midogo mali ya wizi. Watu hao wenye kushangaza walimiliki nyika za Asia na Ulaya kuanzia mwaka wa 700 hivi hadi 300 K.W.K. Kisha wakatoweka. Hata hivyo wanakumbukwa katika historia. Hata wanatajwa katika Biblia. Watu hao ni Wasikithe.

Kwa karne nyingi, wahamaji na makundi ya farasi mwitu walirandaranda kwenye mbuga zinazoanzia Milima ya Carpathia, iliyoko mashariki mwa Ulaya, hadi kusini-mashariki mwa Urusi ya kisasa. Kufikia karne ya nane K.W.K., vita vilivyoanzishwa na Maliki Mchina Hsüan vilifanya Wasikithe wahamie upande wa magharibi. Walihama kuelekea upande wa magharibi na kuwaondosha Wasimeria waliokuwa wakikalia eneo la Caucasus na eneo lililo kaskazini ya Bahari Nyeusi.

Huku wakitafuta utajiri, Wasikithe walipora jiji kuu la Ashuri, Ninewi. Baadaye, waliungana na Ashuri ili kupigana na Wamedi, Wababiloni, na mataifa mengine. Vita vyao vilienea hadi kaskazini mwa Misri. Jiji la Beth-shan lililo kaskazini-mashariki mwa Israel baadaye liliitwa Scythopolis, jambo linaloonyesha kwamba huenda Wasikithe walikalia eneo hilo.—1 Samweli 31:11, 12.

Hatimaye, Wasikithe walianza kuishi kwenye nyika zilizo katika nchi za kisasa za Rumania, Moldova, Ukrainia, na kusini mwa Urusi. Wakiwa huko walitajirika kwa kuwauzia Wagiriki ngano waliyonunua kutoka kwa wakuza ngano wa Ukrainia ya kisasa na wale walio kusini mwa Urusi ya kisasa. Wasikithe waliwauzia Wagiriki nafaka, asali, sufu, na ng’ombe, nao Wagiriki wakawauzia divai, nguo, silaha, na vitu vya sanaa. Kwa hiyo walilundika mali nyingi sana.

Wapanda-farasi Wenye Kutisha

Wapiganaji hawa wa nyikani walitumia farasi sawa na vile watu wanaoishi jangwani wanavyotumia ngamia. Wasikithe walikuwa wapanda-farasi bora sana na walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutumia matandiko na vipandio vya farasi. Walikula nyama na kunywa maziwa ya farasi. Hata walitoa dhabihu za farasi. Mpiganaji Msikithe alipokufa, farasi wake aliuawa na kuzikwa kwa heshima—akiwa na lijamu na matandiko yote.

Kulingana na picha za mwanahistoria Herodotus, Wasikithe walikuwa na utamaduni wenye ukatili mwingi, ambao ulitia ndani kutumia mafuvu ya watu waliowaua kama vikombe. Walipowashinda maadui wao, waliwakatakata kwa panga za chuma, mashoka ya vita, mikuki, na mishale yenye ncha kali iliyorarua ngozi.

Makaburi Yaliwekwa Fanicha za Kudumu

Wasikithe walitumia uchawi na kufuatia dini ya shaman, pia waliabudu moto na mungu wa kike. (Kumbukumbu la Torati 18:10-12) Waliona kaburi kuwa makao ya wafu. Watumwa na wanyama walitolewa kuwa dhabihu kwa bwana-mkubwa aliyekufa. Inadhaniwa kwamba wafanyakazi wa nyumbani pamoja na hazina ziliandamana na watawala kwenye “ulimwengu wa wafu.” Katika kaburi moja la kifalme, watumishi wa kiume watano walipatikana wakiwa wamelazwa miguu yao ikiwa imeelekezwa kwa bwana wao, kana kwamba walikuwa tayari kuamka na kuendelea na kazi zao.

Dhabihu nyingi zilitolewa wakati wa kuwazika watawala, na nyakati za kuomboleza, Wasikithe walimwaga damu yao na kukata nywele zao. Herodotus aliandika hivi: “Walikata sehemu fulani ya masikio yao, wakanyoa nywele zao, wakajikata mikononi, kwenye vipaji na pua zao, na kudunga mikono yao ya kushoto kwa mishale.” Tofauti na hivyo, Sheria ya Mungu kwa Waisraeli walioishi kipindi hichohicho iliamuru: “Msichanje chale yoyote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu.”—Mambo ya Walawi 19:28.

Wasikithe waliacha makaburi (kurgan) mengi sana. Mapambo mengi yaliyopatikana katika kurgan yaonyesha jinsi Wasikithe walivyoishi. Mtawala Mrusi, Peter Mkuu alianza kukusanya vitu hivyo mwaka wa 1715, na sasa mapambo hayo yenye kumetameta yamo katika majumba ya makumbusho huko Urusi na Ukrainia. “Sanaa [hiyo] ya wanyama” inatia ndani farasi, tai, vipanga, paka, chui weusi, kongoni, mbawala, na wanyama (wanaotajwa katika hadithi) wenye mwili wa simba na kichwa na mbawa za tai.

Wasikithe na Biblia

Biblia huwataja Wasikithe mara moja tu. Twasoma hivi katika andiko la Wakolosai 3:11: “Hakuna Mgiriki wala Myahudi, tohara wala kutotahiriwa, mtoka-ugenini, Msikithe, mtumwa, mtu huru, bali Kristo ni yote na katika yote.” Mtume Mkristo Paulo alipoandika maneno hayo, neno la Kigiriki lililotafsiriwa “Msikithe” halikurejezea taifa fulani hasa bali watu wasio na ustaarabu kabisa. Paulo alikuwa akikazia kwamba roho takatifu au kani ya utendaji ya Yehova inaweza kuongoza watu kama hao wajivike utu unaompendeza Mungu.—Wakolosai 3:9, 10.

Waakiolojia fulani wanaamini kwamba jina Ashkenazi linalopatikana katika andiko la Yeremia 51:27 ni sawa na jina la Kiashuri Ashguzai, neno lililotumiwa kurejezea Wasikithe. Mabamba ya kikabari yanaonyesha mapatano yaliyofanywa na watu hao na watu wa Mini kulipotokea uasi dhidi ya Ashuri katika karne ya saba K.W.K. Kabla tu Yeremia hajaanza kutabiri, Wasikithe walipita katika nchi ya Yuda bila kuishambulia wakiwa njiani kwenda na kurudi kutoka Misri. Kwa hiyo, watu wengi waliosikia akitabiri kwamba Yuda ingeshambuliwa kutoka kaskazini huenda walitilia shaka unabii wake.—Yeremia 1:13-15.

Wasomi fulani wa Biblia hufikiri kwamba Biblia hutaja Wasikithe katika andiko la Yeremia 50:42, linalosema: “Wanashika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao inanguruma kama bahari, nao wamepanda farasi; kila mmoja amejipanga kama aendaye vitani, juu yako, Ee binti Babeli.” Lakini mistari hii inawahusu hasa Wamedi na Waajemi, walioshinda Babiloni mwaka wa 539 K.W.K.

Imedokezwa kwamba “nchi ya Magogu” inayotajwa katika kitabu cha Ezekieli sura ya 38 na 39 inarejezea makabila ya Wasikithe. Hata hivyo, “nchi ya Magogu” ina maana ya mfano. Inarejezea ujirani wa dunia, walikotupwa Shetani na malaika wake baada ya vita iliyotokea mbinguni.—Ufunuo 12:7-17.

Wasikithe walihusika kutimiza unabii wa Nahumu uliotabiri kuangushwa kwa Ninewi. (Nahumu 1:1, 14) Wakaldayo, Wasikithe, na Wamedi walipora Ninewi mwaka wa 632 K.W.K., na kuangusha Milki ya Ashuri.

Anguko Lenye Kushangaza

Wasikithe walitoweka, lakini kwa nini? “Ukweli ni kwamba, hatujui kilichotokea,” asema mwakiolojia mashuhuri kutoka Ukrainia. Wasomi fulani wanaamini kwamba kwa sababu Wasikithe walipenda sana utajiri, walijisalimisha katika karne ya kwanza na ya pili K.W.K. kwa kikundi kipya cha wahamaji kutoka Asia, yaani Wasamatia.

Wasomi wengine wanafikiri kwamba zogo lililokuwako miongoni mwa mbari za Wasikithe ndilo lililosababisha milki yao ianguke. Hata hivyo, wasomi wengine wanasema kwamba Wasikithe fulani wanaweza kupatikana miongoni mwa Waoseti wa huko Caucasus. Vyovyote vile, watu hao wa kale wenye kushangaza wanakumbukwa katika historia ya wanadamu—na hivyo jina hilo Msikithe katika Kiingereza lamaanisha ukatili.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

□ Jiji la Kale

• Jiji la Kisasa

Danube

SCYTHIA NJIA WALIYOTUMIA KUHAMA

• Kiev

Dnipro

Dniester

Bahari Nyeusi

MILKIYA

Milima ya Caucasus

Bahari ya Kaspiani

ASHURI ← NJIA ZA UVAMIZI

□ Ninewi

Tigrisi

UMEDI ← NJIA ZA UVAMIZI

MESOPOTAMIA

BABYLONIA ← NJIA ZA UVAMIZI

□ Babiloni

Eufrati

UAJEMI

□ Susa

Ghuba ya Uajemi

PALESTINA

• Beth-shan (Scythopolis)

MISRI ← NJIA ZA UVAMIZI

Naili

Bahari ya Mediterania

UGIRIKI

[Picha katika ukurasa wa 25]

Wasikithe walikuwa watu wa vita

[Hisani]

The State Hermitage Museum, St. Petersburg

[Picha katika ukurasa wa 26]

Wasikithe waliwauzia Wagiriki bidhaa zao nao Wagiriki wakawauzia vitu vya sanaa na wakawa matajiri sana

[Hisani]

Courtesy of the Ukraine Historic Treasures Museum, Kiev