Usafi Ni Muhimu Kadiri Gani?
Usafi Ni Muhimu Kadiri Gani?
WATU wana maoni mbalimbali kuhusu usafi. Kwa mfano, kivulana anapoambiwa na mamake anawe mikono na uso, huenda akafikiri kwamba kuweka mikono yake chini ya maji ya mfereji tu na kuyapaka kwenye midomo yake kwatosha. Lakini mama yake anajua kufanya hivyo hakutoshi. Yeye anamrudisha kwenye mfereji na kusugua mikono na uso wake kwa sabuni na maji mengi—japo kivulana huyo analia kwa sauti kubwa akikataa kunawishwa!
Ni kweli kwamba viwango vya usafi ni tofauti ulimwenguni, na watu hukua wakiwa na maoni mbalimbali kuhusu usafi. Zamani katika nchi nyingi, shule zenye mazingira safi yaliyotunzwa vizuri yaliwasaidia wanafunzi kusitawisha mazoea mazuri ya usafi. Leo, baadhi ya viwanja vya shule vimejaa takataka na vifusi na vinafanana na mahali pa kutupa takataka kuliko mahali pa kuchezea au kufanyia mazoezi. Nayo madarasa yakoje? Darren, mtunzaji wa shule moja ya upili huko Australia alisema: “Sasa hata kuna uchafu madarasani.” Baadhi ya wanafunzi huona ni kama wanaadhibiwa wanapoagizwa, “Okota takataka hiyo” au “Safisha uchafu huo.” Tatizo ni kwamba walimu fulani huwaadhibu wanafunzi kwa kuwaagiza wasafishe sehemu fulani.
Kwa upande mwingine, watu wazima hawaweki kielelezo kizuri cha usafi katika maisha yao au katika biashara. Kwa mfano, sehemu nyingi za umma huachwa zikiwa chafu na zisizopendeza. Viwanda fulani huchafua mazingira. Hata hivyo, uchafuzi huo husababishwa na watu kwa kuwa viwanda na biashara hazijiendeshi zenyewe. Ingawa kwa kadiri fulani uchafuzi husababishwa na mazoea yasiyo safi ya mtu mmoja-mmoja, yaelekea pupa ndiyo kisababishi kikuu cha tatizo hilo linalotokeza madhara mengi ulimwenguni. Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Jumuiya ya Madola ya Australia alikubaliana na maoni hayo aliposema: ‘Masuala yote ya afya ya jamii yanakazia umuhimu wa kila mmoja katika jamii kuzingatia usafi.’
Hata hivyo, wengine huona usafi kuwa jambo la mtu binafsi lisilopaswa kusumbua wengine. Je, ndivyo ilivyo kweli?
Usafi ni muhimu sana kuhusiana na chakula chetu—tuwe tunakinunua sokoni, tunakila kwenye mkahawa, au tunakila nyumbani kwa rafiki. Wale wanaotayarisha au kupakua chakula tunachokula
wanahitaji kudumisha usafi wa hali ya juu. Mikono michafu—yao au yetu—inaweza kusababisha magonjwa mengi. Namna gani kwenye hospitali—mahali ambapo tunatarajia pawe safi zaidi? Jarida The New England Journal of Medicine lilisema kwamba wagonjwa hupatwa na maambukizo wakiwa hospitalini kwa sababu baadhi ya madaktari na wauguzi hawanawi mikono. Kwa mwaka, maambukizo hayo hugharimu dola bilioni kumi za Marekani kuyatibu. Tuna sababu nzuri kutarajia kwamba hakuna yeyote atakayehatarisha afya yetu kwa mazoea yake machafu.Pia, ni vibaya sana kuchafua maji kimakusudi au kwa kutojali. Je, ni salama kutembea bila viatu kwenye ufuo ambako mtu anaweza kuona sindano zilizotumika ambazo zimeachwa na watumiaji wa dawa za kulevya? Labda hata swali muhimu zaidi ambalo mtu anapaswa kujiuliza ni: Je, tunadumisha usafi nyumbani kwetu?
Suellen Hoy anauliza hivi katika kitabu chake Chasing Dirt, “Je, sisi ni safi kama tulivyokuwa hapo awali?” Anajibu: “Yaelekea sivyo.” Anataja kubadilika-badilika kwa viwango vya jamii kuwa ndiyo sababu kuu ya kutokuwa safi. Wakati ambao watu hutumia nyumbani unazidi kupungua, hivyo wao huajiri mtu wa kuwafanyia usafi. Kwa hiyo, wao hawaoni umuhimu wa kudumisha mazingira safi. “Mimi sisafishi bafu—mimi huoga,” akasema mwanamume mmoja. “Angalau mimi ni safi, hata ingawa nyumba yangu ni chafu.”
Hata hivyo, usafi unamaanisha mengi zaidi ya sura ya nje. Unatia ndani maadili yote yanayohusiana na maisha bora. Usafi pia ni hali ya akilini na ya moyoni inayohusisha maadili na ibada yetu. Na tuone inakuwaje hivyo.