Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Wokovu Una Bwana”

“Wokovu Una Bwana”

“Wokovu Una Bwana”

KUNAPOTOKEA misukosuko ya kitaifa na ya kimataifa, watu hutegemea serikali yao iwalinde. Nazo serikali huzidisha mipango ya kuwachochea watu waungane na waunge mkono serikali. Kadiri programu hizo zinavyochochea hisia za kizalendo, ndivyo sherehe za uzalendo zinavyofanywa mara nyingi na kufurahiwa zaidi.

Msiba wa kitaifa unapotokea, mara nyingi msisimuko wa kizalendo huunganisha watu na kuwaimarisha na huenda ukatokeza ushirikiano na kujali masilahi ya wengine. Hata hivyo, hisia za “kizalendo zinaweza kuwa hatari kama hisia yoyote ile,” yasema makala moja katika The New York Times Magazine, kwa kuwa hisia za kizalendo zinapodhihirishwa kupita kiasi, zinaweza kutokeza madhara makubwa sana.” Uzalendo unaweza kuonyeshwa kwa njia inayoweza kuingilia uhuru wa kijamii na wa kidini wa raia fulani katika nchi. Wakristo wa kweli hasa hukabili mkazo wa kukana imani yao. Wao hufanya nini watu wanapodhihirisha hisia za kizalendo? Ni kanuni gani za Kimaandiko ambazo huwasaidia watende kwa busara na kudumisha uaminifu-maadili kwa Mungu?

“Usivisujudie”

Mara kwa mara, watu hupenda kuonyesha uzalendo wao kwa kuisalimu bendera. Lakini mara nyingi bendera huwa na picha za vitu vilivyo mbinguni, kama vile nyota, na vilevile vitu vilivyo duniani. Mungu alionyesha maoni yake kuhusu kusujudia vitu hivyo alipowaamuru watu wake hivi: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu [“Mungu anayedai ujitoaji usiohusisha wengine,” NW].—Kutoka 20:4, 5.

Je, kweli kuisalimu au kuipigia magoti bendera ambayo huwakilisha Nchi ni kuvunja amri ya Yehova Mungu ambaye hudai ujitoaji usiohusisha wengine? Wakiwa nyikani, Waisraeli wa kale walikuwa na “ishara,” au bendera katikati ya vile vikundi vitatu vya kikabila. (Hesabu 2:1, 2, NW) Ikieleza maneno ya Kiebrania yanayomaanisha bendera hizo, Cyclopedia ya McClintock na Strong inasema: ‘Hata hivyo, hakuna mojawapo ya maneno hayo yanayowakilisha “bendera” ambayo yanatoa maana ya neno bendera kama tunavyolielewa.’ Isitoshe, bendera za Waisraeli hazikuonwa kuwa takatifu, wala hakukuwa na sherehe yoyote iliyozihusu. Zilitumika tu kuwa ishara kuonyesha watu mahali pa kukutania.

Mifano ya makerubi katika tabenakulo na katika hekalu la Solomoni ilitumika hasa kufananisha makerubi wa mbinguni. (Kutoka 25:18; 26:1, 31, 33; 1 Wafalme 6:23, 28, 29; Waebrania 9:23, 24) Jambo linaloonyesha kwamba mifano hiyo ya makerubi haikupaswa kuabudiwa ni kwamba, kwa ujumla watu hawakuwaona makerubi hao nao malaika wenyewe hawapaswi kuabudiwa.—Wakolosai 2:18; Ufunuo 19:10; 22:8, 9.

Pia fikiria nyoka wa shaba ambaye nabii Musa alitengeneza Waisraeli walipokuwa nyikani. Umbo au sanamu hiyo, ilitumika kuwa ishara na ilikuwa na maana ya kiunabii. (Hesabu 21:4-9; Yohana 3:14, 15) Haikuabudiwa au kutumiwa katika ibada. Hata hivyo, karne kadhaa baada ya siku za Musa, Waisraeli walianza kuabudu sanamu hiyo, hata wakaifukizia uvumba. Kwa hiyo, Mfalme Hezekia wa Yuda akaivunja vipande-vipande.—2 Wafalme 18:1-4.

Je, bendera za kitaifa ni ishara tu ya sherehe fulani muhimu? Zinawakilisha nini? ‘Bendera ndiyo ishara muhimu zaidi ya kitaifa, nayo huabudiwa,’ akasema mwandishi J. Paul Williams. Kichapo The Encyclopedia Americana chasema: “Bendera ni takatifu kama vile msalaba.” Bendera ni ishara ya Nchi. Kwa hiyo kuisujudia au kuisalimu ni sherehe ya kidini ya kutoa heshima kwa Nchi. Tendo hilo huonyesha kwamba wokovu hutoka kwa Nchi nalo halipatani na yale ambayo Biblia husema kuhusu ibada ya sanamu.

Maandiko husema hivi waziwazi: “Wokovu una BWANA.” (Zaburi 3:8) Wokovu hauwezi kutoka kwa mashirika ya wanadamu au ishara zao. Mtume Paulo aliwashauri hivi Wakristo wenzake: “Wapendwa wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.” (1 Wakorintho 10:14) Wakristo wa mapema hawakushiriki ibada ya Nchi. Katika kitabu Those About to Die, Daniel P. Mannix anasema: ‘Wakristo walikataa kutoa dhabihu kwa maliki Mroma, jambo ambalo sasa ni sawa na kukataa kuisalimu bendera.’ Ndivyo ilivyo na Wakristo wa kweli leo. Ili wampe Yehova ujitoaji usiohusisha wengine, hawaisalimu bendera ya nchi yoyote. Kwa kufanya hivyo, wanamtanguliza Mungu huku wakiheshimu serikali na watawala wake. Kwa kweli, wanatambua daraka lao la kujitiisha kwa “mamlaka zilizo kubwa” za kiserikali. (Waroma 13:1-7) Hata hivyo, Maandiko husema nini kuhusu kuimba nyimbo za kizalendo, kama vile nyimbo za taifa?

Nyimbo za Taifa Ni Nini?

“Nyimbo za taifa ni maneno ya kudhihirisha uzalendo na mara nyingi zinatia ndani kumwomba Mungu awalinde na kuwaongoza raia na watawala wao,” chasema kichapo The Encyclopedia Americana. Kwa kweli, wimbo wa taifa ni sala inayotolewa kwa ajili ya nchi. Ni sala inayotolewa kwa ukawaida kuomba nchi iwe na ufanisi na idumu kwa muda mrefu. Je, Wakristo wa kweli wanapaswa kujiunga na wengine katika sala hiyo?

Nabii Yeremia aliishi miongoni mwa watu waliodai kwamba wanamtumikia Mungu. Hata hivyo, Yehova alimwamuru hivi: “Usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.” (Yeremia 7:16; 11:14; 14:11) Kwa nini Yeremia alipewa amri hiyo? Kwa kuwa jamii hiyo ilijihusisha sana na wizi, mauaji, uzinzi, kuapa kwa uwongo, na ibada ya sanamu.—Yeremia 7:9.

Yesu aliweka mfano aliposema: “Mimi nafanya ombi kuwahusu wao; nafanya ombi, si kuhusu ulimwengu, bali kuhusu wale ambao umenipa.” (Yohana 17:9) Maandiko husema kwamba “ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu” na “unapitilia mbali.” (1 Yohana 2:17; 5:19) Kwa hiyo basi, Wakristo wa kweli wanaotambua jambo hilo wanawezaje kuomba ulimwengu huu ufanikiwe na udumu kwa muda mrefu?

Bila shaka, si nyimbo zote za taifa zinazohusisha dua kwa Mungu. ‘Nyimbo za taifa huwa na maneno tofauti-tofauti. Huenda maneno hayo yakahusu kuombea mtawala fulani, yakagusia vita na uasi wa taifa zima, au hisia za kizalendo,’ chasema kichapo Encyclopædia Britannica. Lakini je, watu wanaotaka kumpendeza Mungu wanaweza kutukuza vita na uasi wa taifa lolote? Isaya alitabiri hivi kuhusu waabudu wa kweli: “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” (Isaya 2:4) Mtume Paulo aliandika hivi: “Ingawa twajiendesha katika mwili, hatufanyi shughuli ya vita kulingana na tulivyo katika mwili. Kwa maana silaha za shughuli yetu ya vita si za kimwili.”—2 Wakorintho 10:3, 4.

Mara nyingi nyimbo za taifa hudhihirisha hisia za utukuzo wa taifa au huonyesha kuwa taifa fulani ni bora kuliko mataifa mengine. Maoni hayo hayapatani na Maandiko. Mtume Paulo alisema hivi katika hotuba yake huko Areopago: “[Yehova Mungu] alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso mzima wa dunia.” (Matendo 17:26) Naye mtume Petro alisema: “Mungu si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.”—Matendo 10:34, 35.

Kwa sababu ya kuielewa Biblia, wengi huamua kutoisalimu bendera au kuimba nyimbo za kizalendo. Lakini wanafanyaje wanapokabili masuala hayo uso kwa uso?

Jiepushe kwa Heshima

Ili kuimarisha mwungano wa milki yake, Mfalme Nebukadneza wa Babiloni la kale alitengeneza sanamu kubwa ya dhahabu katika uwanda wa Dura. Kisha akapanga sherehe ya uzinduzi na kuwakaribisha maamiri, manaibu, maliwali, makadhi, na maofisa wengine wa ngazi za juu. Baada ya kusikia muziki, wote waliokusanyika walipaswa kuanguka na kuiabudu sanamu hiyo. Vijana watatu Waebrania, Shadraka, Meshaki, na Abednego, walipaswa kuwepo. Walionyeshaje kwamba hawakushiriki sherehe hiyo ya kidini? Muziki ulipoanza na wale waliokusanyika walipoinamia sanamu hiyo, Waebrania hao watatu waliendelea kusimama.—Danieli 3:1-12.

Leo, kwa kawaida watu huisalimu bendera kwa kunyosha mkono au kushika kipaji au moyo. Nyakati nyingine, huenda watu wakawa katika kikao fulani maalum. Katika nchi fulani, watoto wa shule hutakiwa wapige magoti na kuibusu bendera. Kwa kusimama kwa heshima wengine wanapoisalimu bendera, Wakristo wa kweli huonyesha kwamba wanaiheshimu pasipo kushiriki sherehe hiyo.

Namna gani iwapo sherehe ya bendera inaongozwa kwa njia ambayo kusimama kungeonyesha kwamba tumeshiriki? Kwa mfano, tuseme mwanafunzi mmoja shuleni amechaguliwa awakilishe shule nzima kuisalimu bendera mbele ya mlingoti, nje ya darasa huku wanafunzi wengine wakiwa wamesimama wima darasani. Kusimama kungeonyesha kwamba unakubali mwanafunzi aliye nje akuwakilishe katika kuisalimu bendera na pia kungeonyesha kwamba unashiriki ibada hiyo. Wale ambao hawangependa kushiriki sherehe hiyo, wanaweza kuonyesha heshima kwa kuendelea kuketi kwa utulivu. Namna gani sherehe hiyo ikianza wanafunzi wakiwa tayari wamesimama? Katika hali hiyo, mtu hatakuwa ameshiriki sherehe hiyo akiendelea kusimama.

Vipi mtu akiombwa ashike tu bendera kwenye gwaride, darasani, au mahali penginepo, ili wengine waisalimu? Kwa kufanya hivyo mtu hatakuwa ‘ameikimbia ibada ya sanamu,’ kama tunavyoagizwa na Maandiko, bali atakuwa ameshiriki kabisa. Ndivyo ilivyo na kuwa katika gwaride za kizalendo. Kwa sababu kufanya hivyo kungemaanisha kwamba mtu anaunga mkono jambo linalotukuzwa na gwaride hiyo, Wakristo wa kweli wakiongozwa na dhamiri hukataa kushiriki.

Nyimbo za taifa zinapoimbwa, kwa kawaida mtu huonyesha kwamba anaunga mkono maneno ya wimbo huo kwa kusimama. Katika hali hizo, Wakristo huendelea kuketi. Hata hivyo, ikiwa tayari wamesimama wakati wimbo wa taifa unapoimbwa, hakuna haja ya kuchukua hatua ya pekee kwa kuketi. Hawakuwa wameamua kusimama kwa ajili ya wimbo wa taifa. Kwa upande mwingine, ikiwa kikundi fulani kinapaswa kusimama na kuimba basi mtu hatakuwa ameshiriki mawazo ya wimbo huo kwa kusimama tu ili kuonyesha heshima.

“Iweni na Dhamiri Njema”

Baada ya kuonyesha ubatili wa vitu vinavyotengenezwa na kuabudiwa na wanadamu, mtunga-zaburi alisema: “Wazifanyao watafanana nazo, kila mmoja anayezitumainia.” (Zaburi 115:4-8) Bila shaka, waabudu wa Yehova hawawezi kukubali kuajiriwa kazi yoyote ya kutengeneza vitu vinavyoabudiwa na wanadamu, kutia ndani bendera za taifa. (1 Yohana 5:21) Huenda kukatokea hali fulani kazini ambapo Mkristo ataonyesha kwa heshima kwamba haabudu bendera wala kitu kinachowakilishwa nayo, ila Yehova peke yake.

Kwa mfano, huenda mwajiri akamwomba mwajiriwa apandishe au ashushe bendera kwenye jengo fulani. Mtu ataamua iwapo atakubali au atakataa ikitegemea jinsi anavyoona hali hiyo. Ikiwa kupandisha au kushusha bendera kunaambatana na sherehe maalum, watu wakiwa wamesimama wima au wakisalimu bendera, basi kuipandisha ni kushiriki sherehe hiyo.

Kwa upande mwingine, ikiwa hakuna sherehe inayoambatana na kupandisha au kushusha bendera, basi kufanya hivyo ni sawa na kutayarisha jengo ili litumiwe, kufunga na kufungua milango na madirisha. Katika hali kama hizo, bendera ni ishara tu ya Nchi, na hivyo kuipandisha au kuishusha au kufanya kazi nyingine za kawaida kunategemea dhamiri ya mtu iliyozoezwa kwa Biblia. (Wagalatia 6:5) Huenda mtu fulani akachochewa na dhamiri yake kumwomba mkubwa wake amwambie mwajiriwa mwingine apandishe na ashushe bendera. Huenda Mkristo mwingine akahisi kwamba dhamiri yake inamruhusu kupandisha au kushusha bendera maadamu hakuna sherehe inayohusika. Hata waamueje, waabudu wa kweli wanapaswa ‘kuwa na dhamiri njema’ mbele ya Mungu.—1 Petro 3:16.

Maandiko hayapingi kufanya kazi au kuingia katika majengo ya umma, kama vile ofisi za manispaa, na shule, ambapo bendera hupeperushwa. Pia huenda stempu, mabamba ya namba ya gari, au vitu vingine vinavyotolewa na serikali vikawa na bendera. Kutumia vitu hivyo si kushiriki ibada. Jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa hapa si bendera, au mfano wa bendera, bali ni jinsi mtu anavyojiendesha kuielekea.

Mara nyingi bendera hupeperushwa kwenye madirisha, milango, magari, dawati, au vitu vingine. Huenda nguo zenye picha ya bendera zikauzwa madukani. Katika nchi fulani ni kinyume cha sheria kuvaa nguo hizo. Hata kama kuvaa nguo hizo hakungekuwa kinyume cha sheria, kungeonyesha mtu ana msimamo gani kuelekea ulimwengu? Yesu Kristo alisema hivi kuhusu wafuasi wake: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:16) Pia tunapaswa kufikiria jinsi kitendo kama hicho kinavyoweza kuathiri waamini wenzetu. Je, kinaweza kuumiza dhamiri ya wengine? Je, kinaweza kudhoofisha imani yao? Paulo aliwashauri Wakristo hivi: ‘Hakikisheni mambo yaliyo ya maana zaidi, ili mpate kuwa bila dosari na kutowakwaza wengine.’—Wafilipi 1:10.

“Mwanana Kuelekea Wote”

Kadiri hali za ulimwengu zinavyozidi kuzorota katika ‘nyakati hizi za hatari,’ yaelekea hisia za kizalendo zitazidi. (2 Timotheo 3:1) Wale wanaompenda Mungu wasisahau kamwe kwamba wokovu una Yehova peke yake. Anastahili ujitoaji usiohusisha wengine. Walipoambiwa wafanye jambo lisilopatana na mapenzi ya Yehova, mitume wa Yesu walisema hivi: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”—Matendo 5:29.

“Mtumwa wa Bwana hahitaji kupigana, bali ahitaji kuwa mwanana kuelekea wote,” akaandika mtume Paulo. (2 Timotheo 2:24) Hivyo, Wakristo hujitahidi kuwa wenye amani, heshima, na waanana huku wakitumia dhamiri yao iliyozoezwa kwa Biblia kufanya maamuzi ya kibinafsi kuhusu kuisalimu bendera na kuimba wimbo wa taifa.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Waebrania watatu waliokuwa imara lakini wenye heshima, waliamua kumpendeza Mungu

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mkristo atendeje wakati wa sherehe ya kizalendo?