‘Walisafiri kwa Mashua Kwenda Kipro’
‘Walisafiri kwa Mashua Kwenda Kipro’
KWA maneno hayo kitabu cha Matendo kinaanza masimulizi yake kuhusu mambo ambayo mishonari Wakristo Paulo, Barnaba, na Yohana Marko walifanya walipotembelea Kipro mwaka wa 47 hivi W.K. (Matendo 13:4) Kama ilivyo leo, wakati huo, kisiwa cha Kipro kilikuwa mahali muhimu sana huko mashariki mwa Mediterania.
Waroma walikitamani sana kisiwa hicho, nao walianza kukitawala mwaka wa 58 K.W.K. Kabla ya hapo, kisiwa hicho kilikuwa na historia yenye matukio muhimu. Kilitawaliwa na Wafoinike, Wagiriki, Waashuru, Waajemi, na Wamisri. Wakrusedi, Wafrank, na wenyeji wa Venice walikuja katika Enzi za Kati, na kufuatiwa na Waturuki. Uingereza ilinyakua kisiwa hicho mwaka wa 1914, na kukitawala hadi kilipopata uhuru mwaka wa 1960.
Sasa utalii ndio tegemeo kuu kiuchumi, lakini wakati wa Paulo kisiwa cha Kipro kilikuwa na mali nyingi za asili, ambazo Waroma walitumia kujaza hazina ya Roma. Shaba ilivumbuliwa mapema katika historia ya Kisiwa hicho, na inakadiriwa kwamba mwishoni mwa utawala wa Waroma, tani 250,000 za shaba zilikuwa zimechimbuliwa. Hata hivyo, kiwanda cha shaba, kilitumia sehemu kubwa ya misitu
mikubwa ili kuyeyusha madini. Misitu mingi ya kisiwa hicho ilikuwa imetoweka Paulo alipofika huko.Kipro Chini ya Waroma
Kulingana na Encyclopædia Britannica, Misri ilipokea kisiwa cha Kipro kutoka kwa Julius Caesar na baadaye, kutoka kwa Mark Antony. Hata hivyo, chini ya utawala wa Augustus, kisiwa hicho kilirudishiwa Roma nacho kilitawaliwa na liwali ambaye aliwajibika moja kwa moja kwa Roma—kama Luka, mwandishi wa kitabu cha Matendo, anavyosema kwa usahihi. Sergio Paulo ndiye aliyekuwa liwali wakati Paulo alipohubiri huko.—Matendo 13:7.
Mkataba wa Amani ya Kimataifa, yaani, Pax Romana, ulifanya migodi iongezeke na viwanda vya Kipro, jambo ambalo lilileta ufanisi katika biashara. Mapato zaidi yalitokana na kuwapo kwa majeshi ya Roma na wasafiri wa kidini waliokusanyika ili kumwabudu Afrodito, mungu aliyelinda kisiwa hicho. Kwa sababu hiyo, kulikuwa na ujenzi wa barabara mpya, bandari, na majengo ya umma yenye fahari. Kigiriki kilibaki kuwa lugha ya serikali, naye maliki wa Roma pamoja na Afrodito, Apolo, na Zeu waliabudiwa na watu wengi. Watu walikuwa na ufanisi mwingi sana, nao walifurahia kuishi katika jamii yenye tamaduni mbalimbali.
Hiyo ndiyo hali ambayo Paulo alikuta alipofika Kipro naye akawafundisha watu kumhusu Kristo. Hata hivyo, Ukristo uliingizwa Kipro kabla ya Paulo kufika huko. Masimulizi ya kitabu cha Matendo yanatuambia kwamba baada ya kifo cha Stefano, ambaye alikuwa mfia-imani wa kwanza Mkristo, baadhi ya Wakristo wa mapema walikimbilia Kipro. (Matendo 11:19) Barnaba, mwandamani wa Paulo, alikuwa mzaliwa wa Kipro, na kwa kuwa alijua kisiwa hicho vizuri, hapana shaka kwamba alimwongoza Paulo vizuri katika safari yake ya kuhubiri.—Matendo 4:36; 13:2.
Kuzirudia Safari za Paulo
Si rahisi kueleza kindani safari za Paulo huko Kipro. Hata hivyo, waakiolojia wanajua kwa kiasi fulani kuhusu barabara bora zilizokuweko wakati wa Waroma. Kwa sababu ya sura ya nje ya kisiwa hicho, hata barabara kuu za kisasa kwa kawaida zinafuata njia zilezile ambazo yaelekea mishonari hao wa mapema walipitia.
Paulo, Barnaba, na Yohana Marko walisafiri kwa meli kutoka Seleukia hadi bandari ya Salami. Kwa nini walisafiri kwenda Salami, na hali Pafosi, ndio uliokuwa mji mkuu na bandari kuu? Ni kwa sababu jiji la Salami lilikuwa kwenye pwani ya mashariki, kilometa 200 tu kutoka jiji la Seleukia, barani. Ingawa nafasi ya Salami kama mji mkuu chini ya uongozi wa Roma ilichukuliwa na Pafosi, Salami iliendelea kuwa kituo cha utamaduni, elimu, na biashara. Salami lilikuwa na Wayahudi wengi, nao mishonari walianza “kulitangaza neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi.”—Matendo 13:5.
Leo, jiji la Salami limebaki magofu tu. Hata hivyo, uvumbuzi wa akiolojia unaonyesha kwamba jiji hilo lilikuwa maarufu na lenye ufanisi.
Yaonekana eneo la soko, ambalo lilikuwa kituo cha siasa na utendaji wa kidini, ndilo lililokuwa soko kubwa zaidi la Kiroma la mikutano kuwahi kuchimbuliwa katika eneo la Mediterania. Magofu yake ambayo ni ya tangu wakati wa Augustus Caesar, yameonyesha mchanganyiko wenye kutatanisha wa sakafu, kumbi za kufanyia mazoezi, madimbwi makubwa yenye kuvutia, uwanja wa michezo, ukumbi wa maonyesho, makaburi yenye fahari, na jumba kubwa la maonyesho linaloweza kutoshea watu 15,000! Karibu na magofu hayo kuna hekalu lenye fahari la Zeu.Lakini Zeu hangeweza kuzuia jiji hilo lisiharibiwe na matetemeko ya nchi. Katika mwaka wa 15 K.W.K., tetemeko kubwa liliharibu sehemu kubwa ya Salami, ingawa baadaye Augustus alilijenga tena. Liliharibiwa tena na tetemeko la nchi mwaka wa 77 W.K., lakini likajengwa tena. Katika karne ya nne, Salami liliharibiwa na mfululizo wa matetemeko ya nchi, nalo likapoteza kabisa umaarufu wake wa kwanza. Kufikia Enzi za Kati, bandari yake ilikuwa imejaa mchanga na kuacha kutumiwa.
Hatujui jinsi watu wa Salami walivyoitikia mahubiri ya Paulo. Lakini Paulo alipaswa pia kuhubiria watu wengine. Baada ya kuondoka Salami, mishonari hao walipaswa kuchagua kati ya njia tatu kuu: moja kuelekea pwani ya kaskazini, kupitia milima ya Kyrenia; nyingine kuelekea magharibi kuvuka bonde la Mesaoria kupitia sehemu kuu ya kisiwa hicho; na ya tatu ni ile inayoelekea kusini mwa pwani.
Kulingana na kawaida ya usafiri wakati huo, Paulo alifuata njia ya tatu. Njia hiyo inapita kwenye mashamba yaliyo na udongo mzuri mwekundu na wenye rutuba. Kilometa 50 hivi kusini-magharibi, njia hiyo huingia katika jiji la Larnaca kabla ya kujipinda kwenda kaskazini kuelekea katikati mwa kisiwa hicho.
“Katika Kisiwa Chote”
Baada ya muda mfupi, barabara hiyo kuu ilifika kwenye jiji la kale la Ledra. Nicosia ambalo leo limejengwa mahali palipokuwa na jiji la Ledra, ndio mji mkuu kwa sasa. Hakuna uthibitisho wowote kuhusu kuwepo kwa ufalme wa jiji hilo la kale. Katikati ya jiji la Nicosia kuna njia nyembamba inayoitwa Barabara ya Ledra ambayo ina shughuli nyingi. Barabara hiyo imezungukwa na kuta zilizojengwa miaka ya 1500 kwa mtindo wa Venice. Hatujui kama Paulo alisafiri kwenda Ledra au la. Biblia inasema tu kwamba walipita “katika kisiwa chote.” (Matendo 13:6) Kichapo The Wycliffe Historical Geography of Bible Lands kinasema kwamba “bila shaka hili linamaanisha kutembelea kikamili jamii za Wayahudi wa Kipro.”
Bila shaka, Paulo alitaka kuzungumza na watu wengi iwezekanavyo huko Kipro. Hivyo, huenda ikawa alifuata njia iliyo kusini mwa Ledra, kupitia Amathus na Kourion—majiji mawili ya kimataifa yenye wakaaji wenye ufanisi.
Jiji la Kourion lilikuwa upande wa juu zaidi wa bahari, kwenye miteremko inayoshuka moja kwa moja kwenye fuo. Jiji hilo lenye fahari la Wagiriki na Waroma liliharibiwa na tetemeko la nchi lilelile lililoharibu Salami mnamo mwaka wa 77 W.K. Kuna magofu ya hekalu lililojengewa Apolo kuanzia mwaka wa 100 W.K. Uwanja wa michezo ungeweza kutoshea watazamaji 6,000. Nakshi maridadi za mawe zilizorembesha sakafu za nyumba za kifahari za watu binafsi zinaonyesha kwamba watu wengi huko Kourion waliishi maisha ya starehe.
Wasafiri Kwenda Pafosi
Kutoka Kourion barabara hiyo nzuri inaelekea magharibi kupitia eneo linalozalisha mvinyo, kisha hatua kwa hatua inapanda juu, na bila kutazamiwa kabisa, barabara hiyo inayopita katikati ya mandhari nzuri inateremka kwa kujipinda-pinda hadi chini kuelekea fuo zenye mchanga. Kulingana na hekaya za Wagiriki, hapo ndipo mahali mungu wa kike, Afrodito, alipotokea baada ya kuzaliwa baharini.
Afrodito alikuwa ndiye mungu maarufu zaidi kati ya miungu ya Wagiriki huko Kipro, naye aliabudiwa kwa bidii hadi karne ya pili W.K. Jiji la Pafosi ndilo lililokuwa kitovu cha ibada ya Afrodito. Kila wakati wa masika, sherehe kubwa ilifanywa katika jiji hilo ili kumtukuza. Wasafiri wa kidini kutoka Asia Ndogo, Misri, Ugiriki, na nchi ya mbali ya Uajemi walikuja Pafosi kwa ajili ya sherehe hizo. Kipro ilipokuwa ikitawaliwa na Watolemi, wenyeji wa Kipro walianza pia kuabudu Mafarao.
Pafosi ulikuwa mji mkuu wa Kipro huko Roma na makao ya liwali, nao ulipewa mamlaka ya kutengeneza pesa za shaba. Mji huo uliharibiwa na tetemeko la nchi la mwaka wa 15 K.W.K., na kama alivyofanya kuhusu jiji la Salami, Augustus alitoa pesa ili lijengwe upya. Uchimbuzi mbalimbali wa mji wa Pafosi umeonyesha maisha ya starehe ya matajiri wa karne ya kwanza—barabara kubwa za jiji, nyumba za kifahari za watu binafsi zilizopambwa vizuri, shule za muziki, kumbi za kufanyia mazoezi, na ukumbi wa maonyesho.
Huo ndio mji wa Pafosi ambao Paulo, Barnaba, na Yohana Marko walitembelea, na ni katika mji huo Sergio Paulo—“mwanamume mwenye akili”—‘alitaka kulisikia neno la Mungu’ licha ya upinzani mkali wa Elima mlozi. Liwali huyo “alistaajabishwa na fundisho la Yehova.”—Matendo 13:6-12.
Baada ya kumaliza kwa mafanikio kazi yao ya kuhubiri Kipro, mishonari hao waliendelea na kazi yao huko Asia Ndogo. Safari hiyo ya kwanza ya umishonari iliyofanywa na Paulo ilikuwa muhimu sana katika kueneza Ukristo wa kweli. Kitabu St. Paul’s Journeys in the Greek Orient hutaja safari hiyo kuwa “mwanzo halisi wa kazi ya Kikristo na . . . wa kazi ya umishonari ya Paulo.” Kinaongeza: “Kwa kuwa Kipro lilikuwa katikati ya njia za bahari zinazoelekea Siria, Asia Ndogo, na Ugiriki, kisiwa hicho kilikuwa kituo cha kwanza cha safari ya umishonari.” Lakini hiyo ilikuwa tu hatua ya kwanza. Karibu miaka 2,000 baadaye, kazi ya Kikristo ya umishonari inaendelea, na kwa kweli inaweza kusemwa kwamba habari njema ya Ufalme wa Yehova imefika kihalisi “sehemu ya mbali zaidi ya dunia.”—Matendo 1:8.
[Ramani katika ukurasa wa 20]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KIPRO
NICOSIA (Ledra)
Salami
Pafosi
Kourion
Amathus
Larnaca
MIL. YA KYRENIA
UWANDA WA MESAORIA
MIL. YA TROODOS
[Picha katika ukurasa wa 21]
Akiwa amejawa na roho takatifu, Paulo alimpofusha Elima mlozi huko Pafosi