Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Kiongozi Gani Anayefaa Leo?

Ni Kiongozi Gani Anayefaa Leo?

Ni Kiongozi Gani Anayefaa Leo?

Mnamo mwaka wa 1940, kulikuwa na tatizo la uongozi katika Bunge la Uingereza. David Lloyd George, mwenye umri wa miaka sabini na saba, ambaye alisikiliza mjadala huo, alikuwa ameongoza Uingereza kushinda Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, na kwa sababu ya kuwa katika siasa kwa miaka mingi aliweza kuchanganua kwa makini kazi ya maofisa wa ngazi za juu. Katika hotuba aliyotoa kwa Bunge la Wawakilishi la Uingereza Mei 8, alisema: “Raia wako tayari kufanya yote wawezayo maadamu tu wana viongozi, mradi tu Serikali inaeleza malengo yake waziwazi na raia wana uhakika kwamba viongozi wao wanafanya yote wawezayo.”

MANENO ya Lloyd George yanaonyesha wazi kwamba watu wanatazamia viongozi wao wawe hodari na wajitahidi kikweli kuboresha mambo. Mwanamke anayeshiriki katika kampeni za uchaguzi alisema hivi: “Watu wanapopiga kura ili kuchagua rais, wao hupiga kura kuchagua mtu ambaye wataweka maisha yao, wakati wao ujao, na watoto wao mikononi mwake.” Ni kazi kubwa sana kudumisha tumaini hilo. Kwa nini?

Ulimwengu wetu una matatizo mengi sana ambayo huonekana kuwa magumu kutatua. Kwa mfano, ni kiongozi gani ambaye amethibitika kuwa mwenye hekima sana na nguvu hivi kwamba anaweza kukomesha uhalifu na vita? Kati ya viongozi wa leo, ni nani mwenye uwezo na huruma ya kumpa kila mwanadamu chakula, maji safi, na matibabu? Ni nani aliye na ujuzi na azimio la kulinda na kurudisha mazingira katika hali nzuri? Ni nani aliye hodari na mwenye nguvu vya kutosha kuhakikisha kwamba wanadamu wote wanaishi maisha marefu na yenye furaha?

Wanadamu Hawawezi Kufanya Kazi Hiyo

Ni kweli kwamba viongozi fulani wamefanikiwa kwa kadiri fulani. Hata hivyo, wanaweza kutumikia kwa miaka michache tu—kisha ni nani anayefuata? Mmojawapo wa viongozi hodari zaidi aliyepata kuishi, Mfalme Sulemani wa Israeli la kale, alitafakari juu ya swali hilo. Alifikia mkataa huu: “Nami, naam mimi, nikachukia kazi yangu yote iliyo ngumu ambayo niliifanya kwa bidii chini ya jua, ambayo ningemwachia mtu ambaye angekuja baada yangu. Na ni nani anayejua kama atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo, atachukua usimamizi wa kazi yangu yote iliyo ngumu niliyoifanya kwa bidii ambayo ndani yake nilitumia hekima chini ya jua. Hilo pia ni ubatili.”—Mhubiri 2:18, 19.

Sulemani hakujua iwapo mwandamizi wake angeendeleza kazi yake nzuri au angeiharibu. Sulemani aliona ule utaratibu wa viongozi wapya kuchukua mahali pa viongozi wa zamani kuwa “ubatili.”

Nyakati nyingine, jeuri hutumiwa ili kubadili viongozi. Viongozi wenye uwezo wameuawa wakiwa katika mamlaka. Pindi moja, Abraham Lincoln, rais wa Marekani aliyeheshimiwa sana aliwaambia wasikilizaji wake hivi: “Nimeteuliwa kuchukua wadhifa muhimu kwa muda mfupi tu, na sasa, mbele yenu, nimepewa mamlaka ambayo itakwisha hivi karibuni.” Kwa kweli, alitumika kwa muda mfupi. Licha ya mambo yote aliyofanya na tamaa yake ya kuwafanyia watu mengi zaidi, Rais Lincoln aliongoza nchi yake kwa miaka minne tu. Mwanzoni mwa muhula wake wa pili, aliuawa na mtu fulani aliyetaka badiliko la uongozi.

Hata viongozi bora zaidi wa kibinadamu hawawezi kuwa na uhakika kuhusu wakati wao ujao. Basi je, unapaswa kuwatumaini wakuhakikishie jinsi wakati wako ujao utakavyokuwa? Biblia inasema: “Msiweke tegemeo lenu katika watu wenye vyeo, wala katika mtu wa udongo, ambaye hana wokovu wowote. Roho yake hutoka, naye hurudi kwenye udongo wake; siku hiyo mawazo yake hupotea.”—Zaburi 146:3, 4.

Huenda isiwe rahisi kukubali shauri la kutowategemea viongozi wa kibinadamu. Hata hivyo, Biblia haisemi kwamba wanadamu hawatapata kuwa na viongozi wazuri kamwe. Andiko la Isaya 32:1 linasema: “Tazama! Mfalme atatawala kwa ajili ya uadilifu.” Yehova Mungu, Muumba wa wanadamu ameandaa “mfalme,” Kiongozi ambaye hivi karibuni atakuwa na mamlaka kamili katika mambo ya dunia. Yeye ni nani? Unabii wa Biblia unamtambulisha.

Yule Anayestahili Kikweli Kuongoza

Miaka elfu mbili iliyopita, malaika alimwambia hivi mwanamke mchanga Myahudi anayeitwa Maria: “Utachukua mimba katika tumbo lako la uzazi na kuzaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu. Huyo atakuwa mkuu naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Zaidi; na Yehova Mungu atampa kiti cha ufalme cha Daudi baba yake, naye atatawala akiwa mfalme juu ya nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” (Luka 1:31-33) Naam, Yesu wa Nazareti ndiye Mfalme anayetajwa katika unabii wa Biblia.

Mara nyingi michoro ya kidini huonyesha Yesu akiwa mtoto, mtu dhaifu asiyelishwa chakula cha kutosha, au mtu anayejinyima anasa kabisa ambaye hajitetei hata anapopatwa na jambo lolote. Michoro hiyo haifanyi watu wamtumaini Yesu akiwa Mtawala. Hata hivyo, Yesu Kristo anayetajwa katika Biblia, alikua na akawa mtu mwenye nguvu, mkomavu, mwenye bidii na ubunifu. Naye alikuwa na sifa nyingine zilizofanya astahili kuwa kiongozi. (Luka 2:52) Yafuatayo ni mambo machache kuhusu utu wake wenye kutokeza.

Yesu alidumisha utimilifu kamili. Alikuwa na mwenendo mnyoofu hivi kwamba aliwapinga maadui wake waziwazi watoe shtaka lenye msingi dhidi yake. Hawakuweza. (Yohana 8:46) Mafundisho yake yasiyo ya unafiki yalishawishi watu wengi wanyoofu wawe wafuasi wake.—Yohana 7:46; 8:28-30; 12:19.

Yesu alikuwa amejitoa kabisa kwa Mungu. Alikuwa ameazimia kumaliza kazi aliyopewa na Mungu ambayo hakuna mpinzani yeyote—mwanadamu au roho mwovu—angeweza kumzuia. Hakuogopeshwa na vitisho vya kijeuri. (Luka 4:28-30) Hakuvunjwa moyo na uchovu na njaa. (Yohana 4:5-16, 31-34) Hata ingawa rafiki zake walimwacha, aliendelea kufuatia mradi wake.—Mathayo 26:55, 56; Yohana 18:3-9.

Yesu aliwajali sana watu. Aliwaandalia chakula watu wenye njaa. (Yohana 6:10, 11) Aliwafariji waliovunjika moyo. (Luka 7:11-15) Aliwaponya wasioona, wasiosikia, na wale waliohitaji kuponywa. (Mathayo 12:22; Luka 8:43-48; Yohana 9:1-6) Aliwatia moyo mitume wake waliofanya kazi kwa bidii. (Yohana, sura ya 13–17) Alithibitika kuwa “mchungaji mwema” ambaye aliwajali kondoo wake.—Yohana 10:11-14.

Yesu alikuwa na nia ya kufanya kazi. Aliosha miguu ya mitume wake ili kuwafunza somo muhimu. (Yohana 13:4-15) Alihubiri habari njema akitembea katika barabara zenye vumbi za Israeli. (Luka 8:1) Hata alipopanga kupumzika “mahali pasipo na watu,” umati ulipomtafuta ili kupokea mafundisho zaidi, alikubali kuwafundisha. (Marko 6:30-34) Hivyo, aliwawekea Wakristo wote kielelezo cha kuwa wenye bidii.—1 Yohana 2:6.

Yesu alimaliza mgawo wake na kuondoka duniani. Kwa sababu ya uaminifu wake, Yehova Mungu alimthawabisha kwa kumpa ufalme na uhai usiokufa mbinguni. Biblia inasema hivi kuhusu Yesu aliyefufuliwa: “Kristo hafi tena, kwa kuwa sasa amekwisha kufufuliwa kutoka kwa wafu; kifo si bwana juu yake tena.” (Waroma 6:9) Unaweza kuwa na hakika kwamba yeye ndiye Kiongozi bora zaidi wa wanadamu. Kristo Yesu atakapokuwa na mamlaka kamili juu ya dunia, hakutakuwa na uhitaji wa kumpa mtu mwingine mamlaka, wala hakutakuwa na uhitaji wa kuwa na kiongozi mwingine. Hataondolewa kamwe katika mamlaka yake, nayo kazi yake haitabatilishwa wala kuharibiwa na mrithi asiye stadi. Lakini ni nini atakachofanya hasa ili kuwanufaisha wanadamu?

Mambo Atakayofanya Mfalme Huyo Mpya

Zaburi ya 72 inatupa habari fulani za kinabii kuhusu jinsi Mfalme huyo mkamilifu asiyeweza kupatwa na kifo atakavyotawala. Katika mstari wa 7 na 8, tunasoma: “Katika siku zake aliye mwadilifu atachipuka, na wingi wa amani mpaka mwezi utakapokuwa haupo tena. Naye atakuwa na raia kutoka bahari mpaka bahari na kutoka ule Mto mpaka miisho ya dunia.” Chini ya utawala wake wenye kunufaisha, wakaaji wa dunia watafurahia uzima wa milele na usalama wa kudumu. Ataharibu silaha zote zilizopo na hata kuondoa katika mioyo ya wanadamu ile tamaa ya kupigana. Wale ambao leo huwashambulia wengine kama simba walafi au ambao huwatendea jirani zao kama dubu wakali, watakuwa wamebadili mtazamo wao kabisa. (Isaya 11:1-9) Amani itakuwa nyingi.

Zaburi ya 72 inaendelea kusema hivi katika mstari wa 12 hadi 14: “Atamkomboa maskini anayelilia msaada, pia mwenye kuteseka na yeyote ambaye hana msaidizi. Atamsikitikia mtu wa hali ya chini na maskini, naye ataziokoa nafsi za maskini. Ataikomboa nafsi yao kutoka katika ukandamizaji na katika jeuri, nayo damu yao itakuwa na thamani machoni pake.” Watu wa hali ya chini, maskini, na waliotaabishwa watakuwa sehemu ya familia ya kibinadamu iliyoungana chini ya uongozi wa Mfalme Yesu Kristo. Wataishi maisha yenye shangwe, si yenye maumivu na kukata tamaa.—Isaya 35:10.

Mstari wa 16 unaahidi hivi: “Kutakuwa na wingi wa nafaka duniani; juu ya milima kutakuwa na mafuriko.” Mamilioni ya watu duniani leo wanaathiriwa na njaa. Mara nyingi, siasa na pupa hufanya chakula kisigawanywe kwa njia ya haki, na hivyo watu wengi, hasa watoto, hufa njaa. Lakini chini ya utawala wa Yesu Kristo, tatizo hilo halitakuwepo tena. Dunia itatokeza mavuno mazuri ya chakula kitamu. Wanadamu wote watalishwa vizuri.

Je, ungependa kupata baraka hizo za kiongozi mzuri? Ikiwa ndivyo, tunakutia moyo ujifunze mengi zaidi kuhusu Kiongozi ambaye hivi karibuni atakuwa na mamlaka kamili juu ya dunia yote. Mashahidi wa Yehova watafurahi kukusaidia kufanya hivyo. Hutakatishwa tamaa, kwa kuwa Yehova Mungu mwenyewe anasema hivi kumhusu Mwana wake: “Mimi, naam, mimi nimemweka mfalme wangu juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.” —Zaburi 2:6.

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

KUONDOLEWA MAMLAKANI KWA GHAFULA

Kwa kawaida, mtawala hutarajia raia zake wamheshimu na kumuunga mkono ikiwa atawaletea amani ya kiasi fulani na hali nzuri ya maisha. Hata hivyo, watu wakikosa imani naye kwa sababu yoyote ile, huenda baada ya muda mfupi mtu mwingine akachukua nafasi yake. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya hali fulani zilizofanya watawala wenye nguvu waondolewe mamlakani kwa ghafula.

Hali za maisha zisizoridhisha. Kufikia karne ya 18, raia wengi Wafaransa walilazimika kulipa kodi za juu na kupata chakula kidogo. Hali hizo zilisababisha Mapinduzi ya Ufaransa, ambayo mwaka wa 1793, yalifanya Mfalme Louis wa Kumi na Sita anyongwe.

Vita. Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, vilikomesha baadhi ya maliki wenye nguvu zaidi katika historia. Kwa mfano, mnamo 1917, ukosefu wa chakula uliosababishwa na vita huko St. Petersburg, Urusi, ulibadilika na kuwa Mapinduzi ya Urusi. Mapinduzi hayo yalimwondoa mamlakani Mtawala Nicholas wa Pili na kutokeza utawala wa Kikomunisti. Mnamo Novemba 1918, Wajerumani walitaka amani, lakini washirika wao hawakutaka kuacha vita mpaka badiliko la utawala lifanywe. Kwa sababu hiyo, Maliki wa Ujerumani Wilhelm wa Pili, alilazimika kukimbilia uhamishoni huko Uholanzi.

Kutamani serikali za aina tofauti. Mwaka wa 1989, Pazia la Chuma liliondolewa. Serikali zilizoonekana kuwa ngumu kama mawe ziliporomoka, nao raia zake wakakataa Ukomunisti na kuanzisha tawala za aina mbalimbali.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Yesu aliwalisha wenye njaa, akawaponya wagonjwa, na kuweka kielelezo kizuri kwa Wakristo wote

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

Lloyd George: Photo by Kurt Hutton/Picture Post/Getty Images